Baada ya Jiji la Kampala kuangukia mikononi mwa majeshi ya Tanzania, hali haikutulia kama ilivyotazamiwa. Usiku wa Jumanne ya Aprili 10 kuamkia Jumatano ya Aprili 11, 1979, maelfu ya wanajeshi wa Tanzania walikuwa wakivinjari katika jiji la Kampala.
Vikosi kadhaa vya Brigedi ya 208 iliyokuwa chini ya Brigedia Mwita Marwa vilikuwa kusini mwa mji huo. Brigedi ya 207 ya John Butler Walden (Black Mamba) ilikuwa upande wa magharibi mwa jiji, na Brigedi ya 201 chini ya Brigedia Imran Kombe ilikuwa imeweka kizuizi upande wa kaskazini.
Hadi mapambazuko ya Jumatano ya Aprili 11, 1979, wanajeshi wa Tanzania wakawa katika kila kona ya kila barabara iliyoingia katika Jiji la Kampala, ikiwa ni pamoja na barabara iliyoelekea Jinja. Askari yeyote wa Idi Amin ambaye alikuwa amesalia katika mji wa Kampala sasa alikuwa anawindwa na waliopatikana waliuawa.
Mapema Jumatano asubuhi, wapiganaji wa ukombozi wa Uganda, pengine kutokana na wengi wao kulewa usiku wa jana yake, walianza kuwaghasi raia waliokuwa wakipita na magari yao mitaani. Lakini kiongozi wao, Kanali David Oyite Ojok alilazimika kuingia kwenye studio za Redio Uganda kuwatangazia waache kuwasumbua watu.
Kanali Ojok alitaka kutimiza ndoto yake ya kuwatangazia Waganda kuwa sasa wako huru dhidi ya Iddi Amin. Lakini Profesa Yusuf Kironde Lule, kiongozi wa Umoja wa Kuikomboa Uganda (UNLF), akitambua ukaribu uliokuwapo kati ya Kanali Ojok na Dk Milton Obote, alihofia kuwa Ojok angetangaza kuwa Obote amerejea madarakani nchini Uganda.
Kanali Ojok alipokuta simu iliyokuwa ikifanya kazi katika studio za Redio Uganda, aliitumia kwa kupiga simu mbili jijini Dar es Salaam. Simu moja alimpigia Rais Julius Nyerere na simu ya pili alimpigia Obote. Ojok alikuwa amemwahidi Obote kuwa angempigia simu mara atakapokuwa amefika Kampala, na sasa alikuwa anatimiza ahadi yake.
Mwalimu Nyerere hakuwa ofisini kwake wakati Kanali Ojok akimpigia simu, lakini Ojok akaacha ujumbe kwa ofisa usalama aliyepokea simu hiyo kwamba Kampala imedhibitiwa. Alipozungumza na Obote, Kanali Ojok alimwambia kuwa amenuia kutangaza kukombolewa kwa Kampala “kwa jina la UNLF”. Obote alimjibu kwamba hilo ni jambo jema.
Ingawa Kampala ilikuwa imeshakombolewa kutoka kwa Iddi Amin, milio ya risasi ya hapa na pale ilikuwa ikisikika mitaani na wakati mwingine milio ya mabomu nayo ilisikika. Pamoja na yote hayo, mafundi mitambo wa Redio Uganda walifika kazini na kuendelea na kazi zao kama kawaida.
Ojok aliamua kutoa matangazo yake kupitia Redio Uganda. Alitangaza kuwa utawala wa Amin nchini humo umeondolewa na kwamba sasa Kampala ilikuwa mikononi mwa UNLF.
Ojok alinukuliwa na jarida la Tarehe Sita akisema: “Tunauomba umma wa Waganda kuamka na kuungana pamoja kuwaondoa kabisa wauaji wachache waliobakia.”
Aliendelea kusema, “Tunawaomba wapenda amani wote wa dunia hii kuwaunga mkono wakombozi wa Uganda na waulaani utawala uliopita wa kifashisti.”
Ojok aliwataka raia wa Kampala kuwa watulivu na kisha akawataka askari wa Iddi Amin “…popote walipo nchini Uganda wajisalimishe mara moja.”
Ingawa alitangaza hayo, mjini Dar es Salaam Profesa Lule ambaye alikuwa akiyasikiliza matangazo hayo ya Kanali Ojok kupitia Redio Tanzania Dar es Salaam (RTD), ambayo iliyarudia matangazo ya Ojok ya Redio Uganda, hakuyapenda sana—huenda ni kwa sababu hakusikia jina lake likitajwa katika matangazo yenyewe. Aliamini kuwa huu ndio wakati wake wa kusikika—wakati wa kihistoria katika maisha yake na historia ya Uganda.
Kiuhalisia, Profesa Lule alikuwa hotelini mjini Dar es Salaam wakati Ojok na wengine wakiwa katika uwanja wa mapambano dhidi ya utawala wa Iddi Amin kwa kipindi cha miaka kadhaa na sasa walifanikiwa kupigana hadi kuitwaa Kampala.
Profesa Lule aliamua kuandaa tangazo lake mwenyewe ambalo lingetolewa na Redio Uganda. Tangazo hilo lilirekodiwa kwenye mkanda wa kaseti mjini Dar es Salaam na baadaye likatumwa Kampala, Uganda kwa ajili ya Redio Uganda. Ingawa hivyo, tangazo lililonukuliwa na vyombo vya habari vya kimataifa ni lile la Kanali Ojok na si lile la Profesa Lule.
Katika mkanda wa kaseti uliorekodiwa Dar es Salaam na kupelekwa Kampala, kwa mujibu wa jarida la Summary of World Broadcasts: Non-Arab Africa la Ijumaa ya Aprili 13, 1979, Profesa Lule alisema: “Najisikia heshima na faraja kuwatangazia muundo wa Serikali ya mpito kwa nchi yenu (Uganda). Serikali yenu itakuwa kama ifuatavyo....”
Baada ya kujitaja mwenyewe kama Rais wa Serikali ya mpito ya Uganda na mawaziri wake aliowateua akiwa mjini Dar es Salaam, Profesa Lule alitaka kuwapo na utawala wa sheria, kisha akaahidi kuwa utafanyika Uchaguzi Mkuu nchini Uganda “mapema kadri hali itakavyoruhusu”.
Miongoni mwa waliotajwa katika baraza lake la mawaziri ni pamoja na Sam Sabagareka, Otema Alimadi, Paulo Mwanga, Dk Arnold Bisasi, A. Biararuha, Mathias Ngobi, Profesa Asavia Wandira (Elimu), Dani Wadada Nabudere (Utamaduni na Maendeleo ya Jamii), George Wilson Kanyeihamba (Sheria) na Luteni Kanali William Omaria.
Lakini siku moja baada ya matangazo hayo Iddi Amin alijibu. Katika matangazo yake Amin alimjibu Ojok na si Profesa Lule. Amin alikuwa akizungumza kutokea mahali fulani magharibi mwa Uganda. Inawezekana alikuwa akizungumza kupitia kituo fulani cha idhaa ya nje ya Redio Uganda au kwa kutumia magari ya matangazo ya redio aliyoyanunua kwa gharama akiwa madarakani.
Kwa mujibu wa gazeti la The Washingtong Post la Aprili 12, 1979 chini ya kichwa cha habari Uganda Capital Cuptured, Iddi Amin alinukuliwa akisema: “Mimi Rais Iddi Amin Dada wa Jamhuri ya Uganda, napenda kukanusha matangazo yaliyotolewa na aliyekuwa Luteni Kanali wa jeshi, Oyite Ojok, kwamba eti Serikali yangu imepinduliwa na eti Serikali ya uasi imeundwa Uganda...” Nini kilitokea?

VITA YA KAGERA: Uporaji washamiri jijini Kampala




Ingawa ilitazamiwa kuwa baada ya Uganda kukombolewa mambo yangekuwa shwari, hali ilikuwa tofauti na matarajio. Uporaji ulianza na kisha kuenea maeneo yote—hususan katika mji wa Kampala.
Waporaji walionekana wajasiri sana na waliingia mitaani mapema Jumatano ya Aprili 11, 1979 pamoja na kwamba bado kulikuwa na milio ya risasi na mabomu katika mitaa ya Kampala na wanajeshi wa Jeshi la Kuikomboa Uganda (UNLA) walielekezwa kumpiga risasi mtu yeyote aliyekuwa mitaani ambaye hakuwa amevaa sare.
Kufikia jioni ya siku hiyo ikawa imeshakuwa kawaida kuona makundi ya waporaji wakitembea mitaani huku wamebeba mikononi na vichwani mwao mali walizopora. Kabla ya giza halijaingia mitaa mingi ikawa imefurika watu kiasi kwamba hata magari yalishindwa kupita.
Maeneo yaliyowavutia zaidi waporaji ni nyumba zilizokimbiwa za maofisa wa Iddi Amin. Lakini baada ya kumaliza kupora katika nyumba hizo, walihamia na kwenye maeneo mengine.
Askari wa Tanzania walibaki wakitazama hali inavyokwenda, lakini Luteni Kanali Benjamin Msuya alikerwa na hali hiyo na ingawa aliona ni lazima afanye chochote, hakuwa na namna ya kuweza kuzuia hali hiyo ya uporaji hata kama ingekuwa ni kwa kuwafyatulia risasi waporaji hao kwa sababu kwa kufanya hivyo askari wake wangelazimika kuwafyatulia risasi idadi kubwa ya raia.
Jambo ambalo Msuya hakulitaka ni kujenga chuki kati ya raia wa Uganda na askari wake. Aliwaamuru askari wake kuwasaidia raia kuingia katika majengo ili kuweka vizuri mali zilizokuwamo. Lakini hali ikawa kinyume kabisa


Askari wa Tanzania walipovunja mlango wa mojawapo ya maghala mjini Kampala lililokuwa karibu na njia ya reli walikuta kulikuwa na hifadhi kubwa ya sukari.
Kulikuwa na uhaba mkubwa wa sukari nchini Uganda kwa zaidi ya mwaka mmoja kabla ya Vita vya Kagera havijazuka.
Kwa mujibu wa jarida la New African Yearbook, kutokana na vibandiko vilivyokuwa kwenye mifuko iliyofungasha sukari hiyo, Amin alikuwa akiisafirisha kwenda Libya kwa kubadilishana na silaha zilizotumika vitani nchini humo.
Jarida la Africa News liliandika kuwa sukari hiyo ilikuwa imeandaliwa tayari kusafirishwa kupelekwa Libya.
Kitabu cah Ethnicity, Nationalism, and Democracy in Africa cha Bethwell Allan Ogot kinasema bidhaa za walaji kama sukari na chumvi zilikuwa adimu nchini Uganda kiasi kwamba haikushangaza baada ya utawala wa Amin kuanguka ndizo zilizoporwa zaidi.
Taarifa za kupatikana kwa sukari katika ghala hilo zilisambaa kwa haraka. Ndani ya dakika chache raia wengi wakawa wamepata taarifa hizo na maelfu wakawa wamefika eneo hilo ndani ya nusu saa ili nao wajipatie sehemu yao.
Kitabu cha War in Uganda kinasema katika uporaji huo, mama mmoja aliyekuwa amemfunga mwanawe mgongoni kwa kanga huku naye akijitahidi kujipatia sehemu yake katika uporaji wa sukari hiyo, mtoto huyo aliuawa baada ya kubanwa katika purukushani.
Mwanamume mmoja aliyejaribu kubeba mfuko wa kilo 50 kichwani naye alikufa kwa kukosa hewa kutokana na msongamano wa watu ulivyokuwa mkubwa.
Hadi kufikia hatua hii, kinaandika kitabu hicho kuwa askari wa Msuya walikuwa wakitazama waporaji walivyokuwa wakihangaika kujipatia sehemu ya bidhaa.
Siku iliyofuata, Alhamisi ya Aprili 12, 1979, uporaji ulikuwa umefikia hatua ya kutozuilika. Sasa ukawa unafanywa si tu katika zile nyumba zilizokimbiwa, bali hata kwa zile zilizokuwa na watu. Wenye nyumba hizo walishindwa kuwazuia waporaji na hivyo wakabaki wakiwaangalia bila msaada wowote, jinsi mali zao zilivyokuwa zinaporwa. Kila duka, ghala, ofisi na kila nyumba iliporwa.
Wakati uporaji ukiendelea askari wachache wa Amin waliobakia bado walikuwa katika Jiji la Kampala. Lakini sasa walikuwa wanatamani jambo moja tu—kuondoka mjini Kampala kwa njia yoyote inayowezekana na kwa haraka inavyowezekana.
Askari hao walitamani kupata nguo za kiraia ambazo wangevaa waweze kuondoka mjini Kampala bila kutambuliwa kuwa ni wa Amin. Njia pekee ambayo wangeweza kupata nguo hizo ni kwa kuwanyang’anya raia waliokuwa wamezivaa. Njia rahisi zaidi ya kuwanyang’anya raia hao ilikuwa ni kwa kuwaua ikiwa wangekataa kuvua kwa hiari yao.
Hatimaye walianza kuingia mitaani maeneo ya raia wakiwa ama mmojammoja au katika makundi ya askari wachache wakitafuta nguo za kiraia, chakula na—la maana zaidi kwao—magari ambayo wangeweza kuyatumia kukimbia mji. Walitumia silaha walizokuwa nazo kufanya uporaji wa mambo hayo. Raia ambao hawakutii matakwa ya askari hao—na wengine ambao hawakupewa nafasi mbadala, waliuawa.
Askari wa Tanzania waliokuwa wakifanya doria kwa kutembea kwa miguu mitaani na wengine kwenye magari aina ya Land Rover katika maeneo ya raia mara kadhaa walikumbana na askari wa Amin waliokuwa wakipora na kuwaua raia waliowapora. Kurushiana risasi kulisikika mara kwa mara katika mitaa mbalimbali ya mji.
Milio ya risasi iliposikika, waporaji walijificha lakini wakawa wanaibuka tena baadaye. Miili ya waliouawa ilibaki imelala mitaani ikioza na ilipofika mwisho wa wiki miili mingi ya raia wengi ilionekana mitaani.
Kitabu cha War in Uganda kinasema kikundi kimoja cha askari wa Amin kilichokuwa na silaha kiliingia nyumbani kwa watumishi wa Ubalozi wa Ufaransa mjini Kampala kwa nia ya kuwapora gari. Watumishi hao ni Ricarda Hetsch na mumewe, Charles Hetsch.
Wakiwa na silaha zao walifika getini walielekeza silaha kwa Ricarda wakimtaka awakabidhi funguo za gari lake. Kwa kuwa Ricarda naye alikuwa mzoefu wa kutumia silaha na alikuwa na bastola yake, ghafla aliichukua na kufyatua risasi tatu. Askari hao walijikuta wakichanganyikiwa wakaanza kukimbia ovyo.
Wakati Serikali ya mpito ikitangazwa kupitia Redio Uganda, uporaji ulikuwa umeshika kasi kuliko ilivyokuwa awali. Kampala ilikuwa imekombolewa kutoka kwa Iddi Amin, lakini uporaji ulitia fora.
Itaendelea