Raia wa nchi za Uarabuni waliokuwa wakiendesha

Toleo lililopita tuliona askari wa Iddi Amin waliobakia katika mji wa Kampala walivyohaha kutoroka bila kujulikana. Waliingia mitaani maeneo ya raia wakiwa ama mmoja mmoja au katika makundi ya askari wachache wakitafuta nguo za kiraia, chakula na—la maana zaidi kwao—magari ambayo wangeweza kuyatumia kukimbia mji.
Pia walitumia silaha walizokuwa nazo kufanya uporaji na raia ambao hawakutii matakwa ya askari hao na wengine ambao hawakupewa nafasi ya mjadala, waliuawa. Hata hivyo hatimaye walielemewa. Sasa endelea...
UKIACHA uporaji uliokuwa ukiendelea na mtupiano wa risasi wa hapa na pale uliokuwa ukifanywa na askari wa Iddi Amin waliokuwa wanatafuta njia ya kuikimbia Kampala, baadhi ya wapiganaji wa Jeshi la Ukombozi wa Uganda (UNLA) nao walijikuta wakilipiza visasi kwa vibaraka wa Amin.
Baadhi ya waliokuwa wameukimbia utawala wa Iddi Amin lakini sasa wakawa wamerudi walianza kuwawinda na kuwaua wale ambao wao walidhani kuwa waliwasaliti au familia zao miaka iliyopita katika utawala wa Amin. Askari wengine wa UNLA waliua kila Mnubi au Mkakwa waliyekutana naye.
Usiku wa Jumanne ya Aprili 10 kuamkia Jumatano, siku ambayo Kampala ilikombolewa, wafuasi wa Amin waliyakimbia makao makuu ya polisi wake wa siri (State Research Bureau—SRB) yaliyokuwa eneo la Nakasero. Lakini wakati wanaondoka walirusha mabomu ya mkono kwenye vyumba walimokuwa ‘wafungwa’ ambao awali walikuwa wamenusurika kufa kwa njaa, mateso na adhabu za vifo.
Ilipofika asubuhi ya kesho yake maeneo ya maegesho ya magari kwenye ofisi za SRB yalikuwa yamefurika raia waliofika kuangalia kama kuna ndugu zao waliokuwa wanashikiliwa humo.
Baadhi ya walionusurika kufa walikuwa wamekonda kupita kiasi. Wapo wengine waliotoka walijikuta wakipata tabu juani kutokana na kuona jua kwa mara ya kwanza katika kipindi cha muda mrefu kwa sababu walikuwa wamefungiwa ndani.
Kwa mujibu wa kitabu cha Escape from Idi Amin’s Slaughterhouse cha Wycliffe Kato, miili ya raia waliokuwa wanashikiliwa katika makao hayo makuu ya SRB ilikuwa imetapakaa karibu kila eneo. Harufu kali ya miili iliyooza ilielekea kutovumilika. Raia wa Uganda waliingia ndani ya vyumba vya mateso vya SRB kutafuta miili ya wapendwa wao.
Miili mingine ilikuwa ni ya watu ambao ndiyo kwanza walikuwa wameuawa saa chache kabla ya askari wa Amin kukimbia wakati mingine ilikuwa ni ya muda mrefu uliokuwa umepita. Mingine ilikuwa imekatwa mikono na miguu.
Kitabu cha War in Uganda kinasema kwenye sakafu ya chini ya ardhi ya jengo hilo kulikuwa na silaha kali za kivita na mabomu yaliyokuwa na uwezo wa kuangamiza mji mzima.
Ikiwa mabomu hayo yangetumiwa kuvunja madaraja ya kusini mwa Uganda huenda yangewachelewesha askari wa Tanzania kwa miezi kadhaa kuifikia miji iliyoteka.
Ghorofa ya juu ya jengo hilo kulikuwa na kompyuta kadhaa na majalada yaliyokuwa na habari muhimu za kiitelijensia na nyingine zisizo za muhimu zilizohusu shughuli za maelfu kwa maelfu ya Waganda waliokuwa ndani na nje ya nchi na utiifu wao kwa Serikali ya Uganda.
Pia kulikuwa na maelfu kwa maelfu ya majalada yenye taarifa za wageni waliokuwa wakiishi Uganda au walioitembelea Uganda.
Kwa mujibu wa kitabu hicho, jalada moja lilionyesha kuwa wakala mmoja wa SRB alikuwa akilipwa posho ya Dola 58,500 za Marekani kwa ajili ya kumwezesha kupata taarifa.
Kitabu cha War in Uganda kimeandika kuwa faili moja katika maelfu ya mafaili yaliyokutwa katika ofisi hizo lilikuwa na muhtasari wa vikao vya siri vya baraza la mawaziri la Tanzania, moja likiwa na kiambato kilichosema “Rafiki yetu wa Dar es Salaam anataka 5,000 nyingine mwishoni mwa mwezi ... Inawezekana kilicho tatizo zaidi katika ghorofa ya juu ya ofisi za SRB ni nakala ya waraka wa siri wa jeshi la Tanzania ukieleza kinaganaga mpango wa kuishambulia Kampala. Waraka huo ulionyesha njia zitakazotumika na kila mahali ambako kila kikosi kitakuwa ... muda uliowekwa katika mkakati huo ni wiki mbili hadi kuingia mji mkuu wa Uganda.”
Kwa jeshi lililokuwa likiulinda mji wake kama hilo la Amin, halikuwa na kitu cha thamani zaidi ya kupata mbinu za siri za jeshi la uvamizi.
Kwa jeshi lolote duniani ambalo lilikuwa limeshaupata mpango wa siri wa jeshi la adui ingekuwa ni rahisi kwao kuweka mtego na kuliangamiza jeshi la adui.
Lakini jeshi la Idi Amin halikuweza kutumia taarifa hizo za kiitelijensia. Huenda walizipata taarifa hizo wakiwa tayari wameshaelemewa na hivyo haikuwa rahisi kwao kuzitumia ilivyopaswa. Isitoshe, taarifa hizi hazikukutwa jeshini bali zilikutwa kwa polisi wa siri wa Amin.
Ilionekana kuwa SRB walikuwa mbali sana katika kukusanya taarifa za kiitelijensia. Pengine tatizo lilikuwa katika kuzichanganua taarifa hizo na kuzifanyia kazi.
Kwa upande mwingine, Kanali Salim Hassan Boma na askari wake walifika kwenye Gereza la Luzira ambalo lilikuwa na sifa mbaya kwa mateso. Liko kwenye viunga vya Kampala.
Maofisa na walinzi wote wa gereza hilo walikuwa wameshakimbia wakiwaacha wafungwa wakiwa wamefungiwa ndani ya gereza bila chakula na bila kujua kilichokuwa kikiendelea nje ya gereza. Kanali Boma aliamuru gereza hilo lifunguliwe na wafungwa waondoke.
Miongoni mwa wafungwa hao alikuwamo kapteni wa ndege za kijeshi aliyepata mafunzo nchini Urusi.
Baada ya kuendesha ndege aina ya MiG-21 katika zile siku za mwanzo za vita, aligoma kuendelea na kazi na baadaye akakimbilia kijijini kwake ambako baadaye aligundulika na kukamatwa.
Mahakama ya kijeshi ilimhukumu kifo na Jumatano ya Aprili 11, 1979—siku ambayo Kampala ilikombolewa na majeshi ya Tanzania—ndiyo ilikuwa tarehe iliyokuwa imepangwa yeye kuuawa kwa kupigwa risasi.
Aliposikia vishindo vya nyayo za miguu vikielekea lango la gereza alilokuwamo asubuhi ya Aprili 11, hakuwa na namna yoyote ya kujua kama hao waliofika gerezani hapo ni wauaji wake wamewasili kumchukua. Lakini kwa mshangao akakuta ni binadamu waliokuja kumweka huru.
Askari wa Tanzania walihisi hawakuwa na la kufanya zaidi ya kuwaachia huru kila mfungwa waliyemkuta katika Gereza la Luzira kwa sababu hawakuwa na namna ya kuwalisha maelfu ya wafungwa na wakati huohuo wakiendelea na mapambano ya kumaliza vita.
Lakini kuachiwa kwa wafungwa hao kwa ujumla wao kulikuja kusababisha matatizo baadaye. Baadhi ya wengine walioachiwa walikuwa wahalifu sugu ambao baadaye walichangia kuongezeka kwa uhalifu nchini Uganda.

VITA YA KAGERA: Profesa Lule aapishwa kuwa Rais wa Uganda

JIONI ya Jumatano ya Aprili 11, 1979 Kanali Benjamin Msuya alipokuwa akitafakari juu ya uporaji na vurugu za jumla kumzunguka, alipokea ujumbe wa kutatanisha kutoka kwa Jenerali David Msuguri.
Jenerali Msuguri alimtaka Kanali Msuya kufanya maandalizi ya kuapishwa kwa Rais mpya wa Uganda kesho yake jioni—Alhamisi. Kanali Msuya hakuwahi kufanya jambo kama hilo maishani mwake. Alilazimika kuwauliza Waganda kadhaa maeneo ambayo walidhani yanafaa kwa ajili ya kazi ya kumwapisha Rais. Wengi waliona mahali palipofaa zaidi ni mbele ya jengo la Bunge.
Asubuhi ya Alhamisi ya Aprili 12, Msuya alikuwa mbele ya jengo la Bunge. Hakujua kwa hakika afanye nini kwa sababu mbali na kupata shida ya itifaki, hata viti vya kukalia havikuwapo kwa sababu vilikuwa vimeporwa. Waporaji walikuwa wameshapora hadi meza na vipaza sauti. Hata lango la kuingia katika jengo la Bunge nalo lilikuwa limefunguliwa na waliokuwa wanapora.
Zaidi ya hilo, bado Kampala haikuwa salama na wasiwasi aliokuwa nao Msuya ni kwamba askari wa Iddi Amin au hata wafuasi wakewangeweza kushambulia wakati Profesa Yusuf Lule akiapishwa.
Wakati akitafakari kuhusu viti, aliona waporaji wakipita mitaani wamebeba viti. Hadi kufikia hatua hii, baada ya waporaji kupora madukani, sasa walihamia kwenye ofisi za Serikali. Walionekana mitaani wamebeba mashine za kupigia chapa, makabati ya kuhifadhia mafaili, madawati na viti.
Kanali Msuya aliwachukua baadhi ya askari wake wakasimama barabarani kuwaangalia waporaji. Kila aliyepita na kiti kizuri alinyang’anywa ili kitumiwe katika kuapishwa. Ingawa havikupatikana viti vya kutosha, angalau wageni muhimu wangepata vya kukalia.
Mafundi mitambo wa Redio Uganda ambao walikuwa na uzoefu na hotuba za viongozi, walipatikana kusaidia kazi hiyo muhimu. Spika na vipaza sauti vilipatikana kutoka kwenye studio ya redio hiyo.
Tatizo lililobaki sasa ilikuwa ni mambo gani yalipaswa kufanyika katika hafla hiyo. Msuya na wenzake hawakuwahi kufanya jambo hilo kabla ya hapo. Hawakujua utaratibu ulitaka nini. Baadaye akapatikana Paul Sozigwa ambaye walimtumia kama mshauri wa itifaki. Sozigwa alikuwa mkurugenzi wa Redio Tanzania Dar es Salaam (1967-1972) baada ya kupokea kijiti kutoka kwa Martin Kiama (1967-1972). Baada ya Sozigwa alikuja David Wakati (1972-1979).
Ingawa naye Sozigwa hakuwa na uhakika sana wa mambo yaliyokuwa yakiendelea, angalau aliwahi kuhudhuria dhifa kadhaa za kitaifa na kimataifa zinazohusu marais wa nchi. Kwa hiyo pamoja na kwamba hakuwa bora kwa jambo hilo, angalau alikuwa bora kuliko wote waliokuwapo kwa wakati huo.
Ilipofika mchana wa Alhamisi kundi kubwa la watu lilikuwa limeanza kujikusanya na kuendelea kuongezeka kuwa umati mkubwa. Kila aliyekuwa akiingia eneo hilo la Bunge alipekuliwa vya kutosha. Wapekuzi walikuta silaha kama bastola, visu na hata mabomu ya kurusha kwa mkono. Upekuzi uliofanyika kwenye Hoteli ya International ulimpata mfanyakazi mmoja wa hoteli hiyo akiwa na mabomu matano ya kurushwa kwa mkono.
Profesa Yusuf Lule na mawaziri wake waliondoka Dar es Salaam kwa ndege kupitia Mwanza. Lakini ndege aliyopanda ilipotua Mwanza, maofisa usalama wa Tanzania walianza kutilia shaka kama kweli kuna usalama wa kutosha mjini Kampala. Iliamuliwa kuwa ndege ya Profesa Lule izuiwe kwanza.
Umati mkubwa wa watu waliokuwa wamekusanyika mbele ya jengo la Bunge hawakujua kuwa mwanadamu waliyekuwa wakimsubiri ili aje aapishwe kuwa Rais wa Uganda bado alikuwa Tanzania. Shamrashamra zilikuwa kubwa kiasi kwamba hata wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Makerere waliandamana kutoka chuoni kwao hadi eneo la Bunge wakiimba nyimbo za kumsifu Profesa Lule.
Umati mkubwa wa watu kwenye eneo la Jengo la Bunge walikuwa wakiimba ingawa kuimba kwao kulikuwa kukikatizwa mara kwa mara na matangazo yaliyokuwa yanatolewa kwenye vipaza sauti yakielezea kila kilichokuwa kikiendelea. Umati huo wa watu uliendelea kusubiri hadi jioni bila Lule kutokea.
Baadaye jioni Kanali Msuya alipokea ujumbe wa redio kutoka Entebbe ukimwambia kuwa Profesa Lule asingefika tena kuapishwa kwa sababu za kiusalama, na kwamba sherehe za kuapishwa kwake ziahirishwe hadi siku inayofuata. Tangazo la kuahirishwa kwa uapishwaji huo likatolewa, lakini umati haukuelezwa sababu ya kweli ya kuahirishwa huko. Umati uliambiwa kuwa sababu za kuahirishwa huko ni tufani iliyotokea katika Ziwa Victoria ambayo iliizuia ndege ya Profesa Lule kusafiri kwenda Entebbe.
Umati wa watu uliokuwa eneo la tukio haukuonyesha hali yoyote ya kuvunjika moyo, na waliendelea kuimba kwa zaidi ya saa moja zaidi kabla hawajatawanyika.
Siku iliyofuata, Ijumaa ya Aprili 13, 1979, upekuzi ulifanyika kama kawaida. Kila aliyeingia eneo la jengo la Bunge alipekuliwa. Hakuna silaha zaidi zilizopatikana kama ilivyokuwa jana yake. Hakuna hata mmoja miongoni mwa waliokusanyika ambaye alipatikana na silaha ya aina yoyote. Watu walianza kukusanyika na kuimba kuanzia mapema asubuhi. Wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Makerere walifika kwa maandamano wakiimba wakiwa wamevalia nguo zao nyekundu za chuo.
Kama ilivyokuwa jana yake, Aprili 12, watu walisubiri sana. Profesa Lule na mawaziri wake walifika jioni badala ya mchana. Waliingia kwa kasi wakiwa katika msafara wa magari kadhaa, mengi ya hayo yakiwa ni ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ). Maofisa wa usalama wa Tanzania walimzingira Lule alipokuwa anaingia jukwaani.
Kwa mujibu wa vyanzo fulani, hafla ya kuapishwa kwake ilikuwa ni fupi. Baada ya kuapishwa, Lule alitoa hotuba fupi. Wakati mmoja akizungumza Kibaganda, jambo lililowakera maofisa wa Tanzania waliokuwapo. Inasemekana kuwa iwapo maofisa wa Tanzania wangejua kile ambacho Lule alimaanisha alipozungumza kikabila, huenda wangekereka zaidi ya ilivyokuwa. Ujumbe wa Lule kwa Wabaganda ulikuwa “sasa ni zamu yetu.”
Tangazo hilo la kikabila lilimkera hata Mwalimu Nyerere. Hata hivyo Profesa Lule hakudumu sana madarakani. Urais wake ulidumu kwa siku 68 tu. Alijikuta akiondolewa madarakani Jumatano ya Juni 20, 1979. Nini kilitokea hadi akaondolewa?