Luteni Kanali Benjamin Msuya alikuwa akiongoza mapambano hayo akiwa na askari kiasi cha 800. Hawa walikuwa wakielekea katikati ya Kampala. Wakati huo, Brigedi ya 207 ilikuwa inashambulia kutokea Magharibi mwa Kampala wakati Brigedi ya 201 ikiweka vizuizi Kaskazini kuwakabili wanajeshi wa Amin waliokuwa wanakimbia. Upande wa Mashariki uliachwa kuruhusu Walibya kukimbilia Jinja na kuondoka Uganda.
Mashambulizi ya mji wa Kampala yalianza asubuhi ya Jumanne ya Aprili 10, 1979. Majeshi ya Tanzania yalifanikiwa kushinda kila aina ya upinzani wa majeshi ya Amin waliokutana nao, licha ya kukabiliana na hali mbaya ya hewa.
Aprili 10 ni siku ya kihistoria Tanzania na Uganda. Inapaswa kuandikwa katika vitabu vya historia kwa ajili ya vizazi vijavyo vya Waganda.
Majeshi ya Amin yaliyojaribu kupambana na majeshi ya Tanzania yalijikuta yakielemewa. Kwa mfano, katika eneo moja la Barabara ya Jinja, wanajeshi wa Amin waliojaribu kupambana na majeshi ya Tanzania kuvuka vizuizi vilivyowekwa na Brigedi ya 201 iliyokuwa ikiongozwa na Brigedia Imran Kombe, walidhibitiwa. Hadi kufikia jioni askari wanane wa Amin walikuwa wameuawa na magari yao kadhaa yaliharibiwa.
Kutokea upande wa Magharibi mwa Kampala, Brigedi ya 207 iliyokuwa chini ya Brigedia John Butler Walden ilikuwa inaukaribia mji wa kampala. Ilipofika asubuhi kikosi cha Brigedia Walden kikawa tayari kimeteka mji wa Natete na sasa kilikuwa kinaelekea Rugaba. Maeneo ya Kilima cha Kasubi na makaburi ya Kabaka nayo yakawa yametumbukia mikononi mwa majeshi ya Tanzania.
Wakati Luteni Kanali Msuya akijiandaa kupeleka vikosi vyake kupita barabara kuu ya kuelekea Kampala kutokea Kusini, vikosi vingine vya Brigedi ya 208 tayari vilikuwa njiani kuelekea Kampala kupitia Port Bell na gereza lililokuwa na sifa mbaya la Luzira.
Wakati huo mvua ilikuwa imepungua na angalau mawingu mazito nayo yalikuwa yameanza kupungua na anga kufunguka.
Kadiri Kampala ilivyokaribiwa, ndivyo—kwa mara ya kwanza—raia walivyokuwa wakiongezeka na kuwa makundi makubwa barabarani huku wakiwa na majani na matawi ya miti wakiwapungia wanajeshi wa Tanzania waliokuwa wakielekea katikati ya jiji la Kampala. Walijua kuwa mara baada ya Kampala kutekwa, enzi ya Amin Uganda ingekuwa imefikia mwisho.
Luteni Kanali Msuya alikuwa na wasiwasi kuwa katikati ya Jiji la Kampala kwenye majengo marefu huenda kungekuwa na wadunguzi. Hata hivyo, hakuwa na la kufanya kwa sababu raia wengi walikuwa wanaingia mitaani kuwalaki wanajeshi wa Tanzania.
Walipokaribia mzunguko wa Makindye, karibu na Gereza la Makindye lililotumiwa na Amin kama kambi ya mateso, umbali wa kilomita mbili kutoka katikati ya kampala, adui walishambulia. Wakati makundi ya raia wakishangilia, ghafla zilisikika risasi za SMG.
Katika hali ya kushtukiza namna hiyo ilikuwa ni vigumu kwa raia na wanajeshi kupata mahali pa kujificha. Kwa hiyo raia walibaki wakishangaa kinachoendelea. Wanajeshi wengi waliwahi kujificha kwenye mitaro ya maji machafu.
Milio ya risasi iliendelea kuongezeka. Pamoja na mashambulizi hayo, mara moja Luteni Kanali Msuya alitoka na mkuki wake kwa kasi kuelekea mbele bila kujikinga. Alipofika mstari wa mbele kabisa alielezwa kuwa risasi hizo zilielekezwa kwa wanajeshi wa Tanzania kutokea nyuma ya soko lililokuwa eneo hilo. Hata hivyo, hakuna mwanajeshi wala raia aliyepatwa na risasi hizo.
Wakiwa wanatafakari hilo, mara wakaona gari aina ya Mercedes Benz likija kwa kasi kuingia barabarani kuelekea walipokuwa wanajeshi wa Tanzania. Ndani ya gari hilo kulikuwa na askari watano waliokuwa wamevalia kiraia, mmoja ndiye aliyekuwa akiendesha na wengine wakiwa wamening’inia kwenye madirisha ya gari huku wakifyatua risasi.
Ni dhahiri kwamba askari hao walikuwa wamejitoa mhanga. Haikujulikana hasa kwa nini hao wanaume watano waliamua kupambana na jeshi la zaidi ya askari 800 lenye vifaru na silaha nyingine nzito za kivita.
Hata hivyo ndani ya sekunde chache walikuwa tayari wameuawa na wanajeshi wa Tanzania kabla hata hawajaufikia mzunguko wa Makindye kwa gari lao kulipuliwa katika mapigano yaliyodumu kwa dakika 10 tu.
Muda mfupi baadaye askari wachache walitumwa kwenda kupekua eneo la soko ambamo gari lile lilitokea. Lakini hawakukuta chochote cha kutiliwa shaka. Wanajeshi wa Tanzania wakaanza kuimba “Kamata Kampala” ... “Kamata Kampala”, kisha wakaanza tena kutembea kuelekea katikati ya Jiji la Kampala. Raia walirejea tena kwenye makundi yao na kuungana na wanajeshi wa Tanzania na ‘gwaride’ likaanza tena kuelekea Kampala kana kwamba hakuna lolote lililotokea.
Kabla ya kufika katikati ya Kampala kulikuwa na matukio kadhaa ambayo askari wa Amin katika maeneo fulanifulani walijaribu kuwarushia risasi askari wa Tanzania kabla ya kukimbilia mafichoni. Lakini katika matukio yote haya hakuna risasi iliyompata hata mmoja.
Ilipofika saa 11 jioni askari wa JWTZ wakafika eneo la Clock Tower katikati ya Kampala. Hili ni eneo ambalo Septemba 1977 Amin aliwaua kwa kuwapiga risasi watu 12 wa kabila la Langi na Acholi—akiwamo Askofu Janani Luwumu—akiwatuhumu kula njama za kuipindua serikali yake.
Luteni Kanali Msuya na wapiganaji wake hawakuwa na ramani ya kampala, na sasa zilikuwa zimebakia saa mbili tu kabla giza halijaingia. Jambo la kwanza ambalo alipanga kulifanya ni kukiteka kituo cha Redio Uganda.

VITA YA KAGERA: Msuya ashangilia kuiteka Kampala


BAADA ya kuzunguka mjini kutokana na kukosa ramani ya mji wa Kampala, huku wakikumbana na mtupiano wa risasi wa hapa na pale kutoka kwa askari wa Iddi Amin waliokuwa wamejificha kwenye majengo fulani fulani katika mji huo, hatimaye walifika katika kituo cha Redio Uganda.
Wanajeshi wa Tanzania waliliendea jengo la redio hiyo kwa uangalifu sana huku askari wengine wakililinda jengo refu la ghorofa lililokuwa upande wa pili wa barabara. Askari wa Tanzania hawakuona ishara yoyote ya kuwapo kwa adui katika eneo hilo na Luteni Kanali Benjamin Msuya na baadhi ya askari wengine walikwenda moja kwa moja kufungua milango ya kituo hicho cha redio huku wengine wakivinjari mitaani.
Msuya alikuwa amepewa maelekezo ya kwamba asitoe matangazo yoyote ya redio iwapo atakuwa amekiteka kituo hicho cha redio. Hata hivyo aliamua hatatangaza chochote, lakini alikwenda kwenye jengo la studio za redio hiyo kuona kama vifaa vyake vilikuwa vinafanya kazi.
Kwa uangalifu mkubwa, Msuya na baadhi ya askari wake waliingia ndani ya jengo hilo. Ilionekana kuwa jengo lilikuwa na chanzo chake cha umeme kwa sababu lilikuwa na umeme wakati sehemu nyingine za Jiji la Kampala hazikuwa na umeme.
Msuya na askari wake walianza kuchunguza vifaa vya studio hiyo. Na wakati wakifanya hivyo, milio ya risasi ilisikika kwa sauti kubwa. Ilikuwa ni vigumu kujua mara moja kama milio hiyo ilikuwa ikitoka ndani au nje ya jengo hilo.
Hata hivyo baadaye ikajulikana kuwa risasi hizo zilikuwa zikipigwa kutoka kwenye jengo refu. Askari wa Tanzania walijibu mapigo kwa kulishambulia jengo hilo. Mapigano hayo yalidumu kwa muda wa takribani sekunde 30 na yalipokoma baadaye ni ama askari hao wa Iddi Amin walikuwa wameuawa au walijificha kwa sababu hawakuonekana tena.
Sasa giza lilikuwa limeshaingia na bado kulikuwa na vilima viwili kati ya saba vilivyoizunguka Kampala ambavyo vilitakiwa kutekwa usiku huo. Maeneo ya mji wa Kampala ambayo yalikuwa hayajatekwa ni kilima cha Nakasero ambako kulikuwa na makao makuu wa polisi wa siri wa Iddi Amin waliojulikana kama State Research Bureau’, makazi ya Amin na kilima cha Kololo.
Wakati Msuya akimaliza kukagua kituo cha redio, kikosi kingine kutoka kwenye brigedi yake kilikuwa kikiandaa shambulio. Gari aina ya Land Rover likilivuta gari jingine aina ya Land Rover yote yakiwa na silaha yalionekana barabarani.
Inaelekea kuharibika kwa gari mojawapo kulisababisha kuchelewesha mpango wa askari wa Iddi Amin waliokuwa wakikimbia mji. Shambulizi kutoka kwa askari wa Tanzania liliyafanya magari hayo yasimame na askari watatu waliovalia kiraia waliruka kutoka kwenye magari hayo, lakini waliuawa mara moja.
Katika gari mojawapo askari wa Tanzania walikuta mpango wa kivita kwa eneo lote la Kampala. Katika mpango huo mji wa Kampala ulikuwa umegawanya katika sehemu nyingi ndogondogo na kila sehemu ilikuwa imekabidhiwa kikosi chake cha kulinda, lakini wengi wa askari wa vikosi hivyo tayari walikuwa wamekwishakimbia.
Ilionekana pia kwamba hata Iddi Amin alikuwa katika mji huo jana yake. Ilijulikana kuwa alizuru Hospitali ya Mulago na kuwaambia askari waliojeruhiwa na kulazwa katika hospitali hiyo kwamba wasiwe na wasiwasi kwa sababu mambo yote yalikuwa yanakwenda vizuri.
Njia ambayo Rais Nyerere alisema ibaki wazi ili Walibya wapate mwanya wa kupitia hiyo na waweze kuondoka Uganda ndiyo hiyohiyo aliyoitumia Amin kuondokea katika zile dakika za mwisho za utawala wake nchini Uganda.
Maofisa wengine wakubwa wa Serikali ya Amin walikuwa wamekimbia mapema zaidi kabla ya Amin mwenyewe.
Kila ofisa aliyekuwa anakimbia alimwachia maelekezo wa chini yake aendelee kuilinda Kampala. Mtindo huo ukaendelea hadi walipokosekana maofisa wa kuwaongoza askari wa Amin na hivyo kubaki wakijiongoza wenyewe.
Msuya na askari wake walianza safari ya kuelekea Kololo na kwenye vilima vingine vilivyoizunguka Kampala. Muda mwingi Msuya alikuwa kwenye mawasiliano ya redio kuwaweka askari wake pamoja.
Kila hatua sasa ilichukuliwa kwa uangalifu mkubwa. Askari wa Iddi Amin waliokata tamaa wangeweza kushambulia kutoka upande wowote hata kwenye majengo walimojificha. Giza lilikuwa likiongezeka na Msuya hakujua kilipokuwa kilima cha Kololo. Raia wa Uganda aliyekuwa akisaidia kutoa maelekezo ambaye alijulikana kwa jina moja tu la Godfrey naye hakutoa msaada sana.
Kwa mujibu wa simulizi fulani, askari wa Tanzania wakaweka kizuizi njia ya kuingia mjini ingawa hakukuwa na magari. Baadaye likatokea gari moja ambalo walilisimamisha. Ndani ya gari kulikuwa na mwanamke na mwanamume. Alipohojiwa na Msuya ikajulikana kuwa alikuwa ofisa wa polisi wa Uganda. Alipoulizwa aliko Iddi Amin, akasema hajui. Msuya akampiga kofi na kumuuliza tena, ni askari wangapi wa Amin wamebaki hapa mjini? Akajibu kuwa hajui. Akapigwa kofi jingine.
Mwanamke naye akaulizwa maswali, naye ikaonekana hana majibu. Lakini hakupigwa. Akamwamuru aende nyumbani na asitoke. Lakini yule ofisa wa polisi akashikiliwa kwa dakika nyingine kumi. Baada ya kuona hana majibu ya maswali aliyoulizwa, naye aliruhusiwa kuondoka zake.
Wakiwa na njaa na kiu, askari wa Tanzania walielekea Kololo. Baada ya kulitafuta eneo hilo kwa muda mrefu, hatimaye walilikuta. Huko walijipanga na kuanza kuchimba mahandaki. Saa tano usiku Msuya aliwaita maofisa wake na kupongezana kwa kuutwaa mji wa Kampala.
Wakazi wa Kololo walikuwa wamejifungia kwenye nyumba zao bila kutambua kuwa tayari mji wa Kampala ulikuwa umekombolewa na majeshi ya Tanzania. Walipokuwa wakisikia milio ya buti za askari wakitembea walidhani ni askari wa Amin waliokuwa wakifanya doria katika maeneo yao.
Milio ya vifaru vilivyokuwa vikipita iliwatia hofu zaidi kiasi kwamba waliogopa kuwasha hata mishumaa na vibatari vyao. Umeme ulikuwa umekatika maeneo yote ya viunga vya mji wa Kampala.
Itaendelea kesho