MPANGO wa kuingia Lukaya ulizishirikisha brigedi tatu ambazo ni 201, 207 na 208. Brigedi ya 201 iliyoongozwa na Brigedia Imran Kombe ilikuwa imejaa wanamgambo ambao wengi wao walikuwa hawajawahi kukabiliana na mapambano ya silaha za moto. Kile kikosi cha Waganda waliompiga Amin kilichoongozwa na David Ojok kiliingizwa pia katika brigedi hii.
Alfajiri Jumamosi ya Machi 10, 1979 vikosi vya Tanzania viliushambulia mji wa Lukaya kwa makombora na kuuchakaza. Kisha wakasubiri kupambazuke. Lakini bila kutambua, kikosi kikubwa cha jeshi la Libya na askari wa Idi Amin walikuwa wamekusanyika upande wa Kaskazini wa Kinamasi na walikuwa wamepewa amri na Idi Amin mwenyewe kuurejesha mji wa Masaka mikononi mwa Uganda ndani ya saa tatu au chini ya hapo.
Askari wa Libya walikuwa wameingia Uganda jana yake, wakiwa na ndege kadhaa ambazo pia zilibeba silaha ndogo na kubwa kama vifaru na mizinga, zilijaza mafuta Nairobi, Kenya kabla ya kuingia Uganda.
Ndani ya ndege hizo yalikuwamo pia magari ya kijeshi kama Land Rover. Lakini silaha iliyotisha zaidi ni “Katushka” ambayo ilitumika kufyatua makombora makubwa. Silaha hiyo ilitengenezwa Korea Kaskazini na haikuwa imetumiwa vitani kabla ya hapo. Jeshi hilo lilikuwa na maelfu ya askari wa Libya na waasi wachache wa PLO. Lilisemekana kuwa ni kikosi kikali katika vita.
Jeshi la Amin na Gaddafi liliingia kazini saa za magharibi wakati giza lilipoanza kutanda. Walipoona brigedi ya Imran Kombe, askari wa Libya wakaanza kufyatua roketi za Katushka. Ingawa roketi hizo hazikuwapiga wanajeshi wa Tanzania, milio mikubwa iliyotokana nazo na miale mikali na mwanga uliotokana nazo zilivyopita juu ya vichwa vya wapiganaji wa Tanzania ilitosha kabisa kuwatia kiwewe wapiganaji wa brigedi ya Kombe ambao wengi hawakuwahi kukutana na mapigano ya risasi, achilia mbali makombora makali kama Katushka.
Baadhi ya wapiganaji katika brigedi hiyo walikimbia. Hata waliobaki, walijikuta hawawezi kufanya chochote. Hata hivyo, hakuna hata mmoja aliyeuawa. Lakini Amin sasa akawa ameurejesha na kuukalia mji wa Lukaya.
Kama askari wa Amin na wale wa Libya wangeendelea na mashambulizi makali zaidi, wangeweza kuyasogeza majeshi ya Tanzania na hata kuutwaa mji wa Masaka kwa sababu kwa wakati huo kilichokuwako katikati ya mji wa Lukaya na Masaka ni vifaru vitatu tu vya Tanzania ambavyo visingeweza kupambana na Katushka ya Libya. Lakini kwa kuzubaishwa na kile walichoona kuwa ni ushindi wa kuurejesha mji wa Lukaya, wao waliamua kupumzika Lukaya.
Mara moja amri ikatolewa kwa vikosi vyote vya Tanzania kubadili mbinu za kivita ili kuichukua tena Lukaya kabla hali haijawa hatari zaidi. Brigedi ya 208, ambayo sasa ilikuwa umbali wa kilomita 60 Kaskazini-Magharibi mwa Lukaya, ilipewa amri ya kugeuka na kurudi kuelekea Lukaya kwa kasi yoyote iliyowezekana na kuvunja mawasiliano ya barabara kati ya majeshi ya Amin na mji wa Kampala.
Vifaru vya Tanzania viliamriwa kusonga mbele na kuanza kushambulia vikali zaidi. Wakati madereva wa vifaru hivyo walipoanza kuonesha hali ya kusita kwenda kushambulia bila kuwa na askari wa kikosi cha miguu, Jenerali Msuguri alimtuma ofisa mwandamizi wa JWTZ kwenda uwanja wa vita kuhakikisha kuwa amri yake inatekelezwa.
Kikosi cha Amin kikisaidiwa na Libya kilikuwa na silaha kali na kingeweza kushinda katika mchezo lakini hakikuwa kimejipanga.
Kwenye njia ya kuelekea Lukaya kulikuwa na Watanzania, askari wa kuikomboa Uganda, majeshi ya Idi Amin pamoja na askari wa Libya. Watu walikuwa wakipishana. Lakini kwa kuwa usiku huo mwanga pekee uliokuwapo ni mbalamwezi, ilikuwa ni vigumu kutambuana.
Kama vile ni aina fulani ya kituko, kikundi cha Kikosi Maalumu (cha kuikomboa Uganda) kilichokuwa kinaongozwa na David Ojok nacho kilipita barabara hiyo kama walivyopita askari wa Amin na wale wa Tanzania na wale wa Libya. Kwa wakati mmoja wote hawa walipita barabara hiyo bila kutambuana.
Askari wa Ojok, wakati wakiwa katika barabara hiyo, waliweza kuwasikia watu wakizungumza Kiswahili na kuwachukulia kuwa hao walikuwa marafiki. Ghafla mmoja miongoni mwao akazungumza Kiluo—lugha ambayo haitumiki Tanzania.
Alisikika akisema “Subiri kupambazuke na tutawaponda hawa Waacholi wajinga.” Kusikia hivyo, Ojok akaamuru wapiganaji wake washambulie. Kwa sababu ya kiza na mwanga hafifu wa mbalamwezi hawakuwa na hakika kama walilenga shabaha zao. Katika mapigano ya usiku huo mmoja, Watanzania wanane na askari mmoja wa Ojok walipoteza maisha.
Wakati hayo yakiendelea, Brigedi ya 208 ilikuwa ikisonga mbele kwa kasi kuelekea Lukaya. Kulipokaribia kupambazuka ilianza kushambulia na kuwarudisha tena nyuma askari wa Amin na wale wa Libya. Mizinga mikubwa ya Tanzania ikaanza kuwasambaratisha Walibya. Wanajeshi wa Idi Amin waliogopa sana kiasi kwamba hawakuthubutu hata kufyatua risasi. Kwa jinsi askari wa Libya walivyochanganyikiwa, walilazimika kukimbia.
Mashambulizi yalipokoma baadaye, askari wa Tanzania walihesabu maiti wakakuta karibu askari 500 wa adui wameuawa katika tukio hilo moja. Miongoni mwa hao waliouawa, zaidi ya 200 walikuwa ni askari wa Libya. Ni askari mmoja tu wa Libya ambaye hakuuawa. Alikamatwa na kuchukuliwa mateka.
Pamoja na ushindi huo, makamanda wa JWTZ waliichukulia Lukaya kuwa ni sehemu ya maafa kwa Watanzania. Kama isingekuwa ni ama uzembe au kutokujimudu kwa jeshi la adui, kwa hakika jeshi la Tanzania lingeondolewa kabisa katika ardhi ya Uganda.
Lakini wakati ikikabiliana na matatizo ya Lukaya, jeshi la Tanzania pia lilikuwa linakabiliwa na hali ngumu katika eneo la Sembabule ambalo likikuwa kiasi cha kilomita 60 Kaskazini-Magharibi mwa mji wa Masaka.

VITA VYA KAGERA : Utekaji wa kwanza wa ndege kielektroniki duniani wafanywa na Jeshi la Wananchi


Katika toleo lililopita tuliona wanajeshi wa Tanzania walivyopata shida katika mji wa Lukaya kiasi kwamba waliamua kuutangaza kuwa nI sehemu ya maafa kwa Watanzania. Eneo la Sembabule nalo lilileta changamoto nyingine kubwa kwa askari wa JWTZ.
Katika toleo hili tutaona namna mabadiliko ya uongozi katika Brigedi ya 205 yalivyoleta tofauti kubwa na hatimaye JWTZ ikaibuka mshindi. Katika kuipanga upya Brigedi ya 205, Brigedia Herman Lupogo aliondolewa akaingia Brigedia Muhidin Kimario. Endelea…
HATA baada ya Tanzania kuiteka Masaka, Idi Amin alisikika katika Redio Uganda akijigamba kuwa Watanzania walikuwa wanazingirwa. Kusikia hivyo, Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lilianza kuchunguza taarifa zao.
JWTZ iligundua kulikuwa na kikosi kizima chini ya kanali kilichoitwa Tiger Regiment kilichokuwa Mubende, katikati ya Masaka na Mbarara.
JWTZ haikuwa imeweka mpango wowote wa kukishughulikia. Kwa kuzingatia alichosema Amin, wachambuzi wa masuala ya kijeshi wakaamini kuwa huenda kikosi hiki kilikuwa kinaelekea kusini ambako kingeanza kuwazingira Watanzania.
Brigedi ya 205 chini ya Brigedia Herman Lupogo iliamriwa kuondoka Masaka kwenda kukabiliana na Tiger Regiment. Haukupita muda mrefu hadi Lupogo alipogundua kilipo kikosi hicho ambacho hadi sasa kilikuwa kimeongezewa nguvu na wapiganaji kutoka Kituo cha Mafunzo ya Kijeshi cha Kabamba na kilijichimbia eneo la Sembabule.
Vita kali ambayo ilidumu kwa wiki tatu ikaanza. Tanzania ilipigana kutwaa eneo moja, lakini wakashtukia kesho yake eneo hilo limetwaliwa tena na majeshi ya Idi Amin.
Hata baada ya kutwaa tena eneo ambalo walinyang’anywa na askari wa Amin, wanajeshi wa Tanzania walikuwa wakikuta maiti za Watanzania katika eneo waliloliteka upya.
Baadaye wapiganaji wa Tanzania wakajikuta wakiogopa na kuvunjika moyo. Vikundi na vikosi vidogo sasa vilikuwa vikikimbia wakati majeshi ya Amin yakishambulia.
Katika kuipanga upya Brigedi ya 205, Brigedia Lupogo aliondolewa katika kikosi hicho na akaletwa Brigedia Muhidin Kimario. Awali Kimario alionekana ni mwanasiasa zaidi kuliko mwanajeshi. Wakati mmoja alikuwa mbunge wa Moshi na kabla vita havijaanza alikuwa mkuu wa Mkoa wa Mwanza.
Alipowasili Sembabule aliikuta Brigedi ya 205 ikiwa shaghalabaghala. Kiasi cha askari 20 au zaidi wa brigedi hiyo walikuwa wameuawa. Wengine walikata tamaa. Makabidhiano ya brigedi kutoka kwa Lupogo kwenda kwa Kimario yalifanyika wakati brigedi ikiwa inashambuliwa na askari wa Amin.
Mara moja Kimario aliwaita askari wake na kuwaahidi kuwa kila atakapotoa amri ya kwenda kwenye mapambano atakwenda nao bega kwa bega.
Kimario aliamua kuacha mbinu za matumizi ya vitengo vidogo vidogo katika brigedi iliyokuwa ikitumiwa na Brigedia Lupogo na badala yake akaamua kuipeleka brigedi nzima mbele kushambulia.
Mbinu ya Kimario ilizaa matunda. Ari mpya ikarudi kwa wapiganaji wa Brigedi ya 205. Ingawa mapigano yalidumu kwa muda fulani, hatimaye Tiger Regiment ikaelemewa. Katika mapigano ya mwisho ambayo katika hayo kikosi hicho cha Idi Amin kilikimbia, brigedi ya Kimario iliua askari 25 wa Amin.
Wakati wote wa mapigano ya Lukaya na Sembabule yakiendelea, Rais Nyerere alikuwa akienda Bukoba mara kwa mara kupata picha halisi ya kinachoendelea vitani badala ya kukaa ofisini na kutegemea taarifa alizokuwa akiletewa. Baada ya ziara yake moja alirejea Dar es Salaam na hofu—ushiriki mkubwa wa Libya katika Vita ya Kagera.
Sasa Nyerere akaona kuwa ushiriki wa moja kwa moja wa Libya katika vita ya Uganda ni uhalali tosha wa Tanzania kumchakaza Idi Amin. Wapiganaji waliokuwa wakikusanywa na vikundi vinavyompinga Amin havikuwa vimefikia matumaini aliyokuwa nayo Nyerere.
Kwa kukasirishwa na kitendo cha kiongozi wa Libya, Muammar Gaddafi kuliingiza jeshi lake nchini Uganda dhidi ya Tanzana, Nyerere akaiamuru JWTZ kuingia Kampala na kuuteka mji huo.
Wakati huu silaha zaidi na wanajeshi zaidi kutoka Libya walikuwa wakiingia Uganda. Ndege za kijeshi zilizotengenezwa Urusi, Tupelev-22, zilikuwa zikiruka kutoka uwanja wa jeshi wa Nakasongola na kwenda kurusha mabomu vilikokuwa vikosi vya Tanzania kusini mwa Uganda.
JWTZ, kwa kuona ndege za Libya zikawa zinaingia Uganda mara kwa mara, ikaamua kutafuta namna ya kuziteka. Hapo ndipo utekaji wa kwanza wa kielektroniki duniani ulifanyika. Kabla ya hapo hakukuwahi kutokea utekaji mwiingine wa aina hiyo mahali popote duniani.
Usiku wa manane, wanajeshiwa JWTZ wakiwa Mwanza, walisubiri hadi pale walipoona kwenye rada ndege mojawapo ikielekea Entebbe, upande wa Uganda, karibu na Ziwa Victoria.
Waliwasiliana na rubani wa ndege hiyo na kujitambulisha kwake kwamba wao ni waongozaji wa ndege katika Uwanja wa Entebbe na kumwonya kuwa uwanja huo, Entebbe, unashambuliwa vikali na wanajeshi na kwa sababu hiyo haingefaa atue kwenye uwanja huo.
Wasiwasi mkubwa ulimpata rubani huyo kiasi kwamba alilazimika kuomba ushauri. Wanajeshi wa JWTZ wakamshauri kuwa uwanja wa ndege ulio karibu zaidi ni ule wa Mwanza na kwamba kwa sasa ni salama zaidi kutua kwenye uwanja huo.
Rubani alijaribu kuuliza maswali kadhaa. Wanajeshi wa JWTZ walimjibu kwa uangalifu mkubwa. Majibu hayo, na jinsi yalivyotolewa, yalimridhisha rubani huyo. Kwa hiyo akaachana na uamuzi wake wa kwenda kutua Entebbe, akabadilisha mwelekeo akarudi kutua Mwanza.
Mara tu baada ya ndege hiyo kutua kwenye uwanja wa Mwanza ikawa tayari imezingirwa na wanajeshi wa JWTZ ambao, hata hivyo, walishangazwa sana kuona kuwa badala ya kuwa ni ndege ya Libya na yenye silaha, wakakuta ni ndege ya mizigo ya Shirika la Ndege la Ubelgiji, Sabena, iliyokuwa safarini kwenda kubeba kahawa kutoka Uwanja wa Ndege wa Entebbe kupeleka Djibout.
Hakukuwa na namna ya kuiachia ndege hiyo iondoke Mwanza iendelee na safari zake kwa sababu vifaa vya kuisaidia ndege hiyo, Boeing 707, kuondoka uwanjani hapi havikuwapo uwanja wa ndege wa Mwanza.
Nyerere alipigiwa simu kuombwa ushauri. Aliagiza wafanyakazi wa ndege hiyo wapelekwe Mwanza Hoteli na wapewe vyumba na mlo mzuri kadiri ilivyowezekana. Kisha Nyerere akamwita balozi wa Ugelgiji na kumwambia kilichofanyika nin bahati mbaya na hakukuwa na lengo baya.
Kesho yake ndege ya kijeshi ilipeleka vifaa vya ndege hiyo kutoka Dar es Salaam. Sabena iliwashwa na kuendelea na safari zake.
Itaendelea