Vyama vilivyopigania ukombozi bado vinaisaidia Afrika?
Kuanzia miaka ya 1950 hadi kufikia 1990 ajenda kuu kwa nchi nyingi za Afrika ilikuwa kusaka uhuru na kujitawala.
Ingawa baadhi ya nchi katika bara hilo zilikuwa uhuru kabla ya hapo, lakini nyingi ziliendelea kutawaliwa kimabavu na wakoloni kutoka mataifa mbalimbali ya Magharibi.
Miongoni mwa mataifa ya Magharibi yaliyotawala Afrika ni Uingereza, Ujerumani, Ureno, Ufaransa, Ubelgiji na Hispania.
Hstoria inaonyesha kuwa baada ya mkutano wa Berlin wa mwaka 1884-1885 uliokuwa umelenga kuligawa bara la Afrika, nchi nyingi ziliangukia mikononi mwa mataifa hayo.
Sehemu kubwa ya Afrika iliyochelewa kupata uhuru ni ile iliyoko Kusini mwa bara hilo.
Katika makala hii tutavitazama baadhi ya vyama vilivyohusika katika ukombozi wa Afrika kuona katika muda ambao tayari nchi zao zimekuwa zikijitawala ni hatua gani zimeweza kufikiwa kwa ustawi wa jamii ikilinganishwa na wakati ule nchi husika zilipokuwa zikitawaliwa.
ANC
The African National Congress (ANC) cha Afrika Kusini, ni moja ya vyama vikuu vilivyopigania ukombozi Kusini mwa Afrika. Kilianzishwa Januari 8, 1912 huku malengo yake ya awali yakiwa ni kupigania haki ya kupiga kura kwa waafrika weusi na raia wengine wa nchi hiyo.
Baadaye katika miaka ya 1940 chama hicho kilijikita katika mapambano ya kukomesha ubaguzi wa rangi ambao ulikuwa tatizo kubwa katika utawala wa makaburu.
Mwaka 1960 utawala wa makaburu chini ya Charles Swart, ulikipiga marufuku chama hicho kufanya shughuli zake nchini humo, baadaye ANC ilianzisha kikundi cha mapambano walichokiita kwa Kizulu Umkhonto we Sizwe (mkuki wa Taifa) kilichotumia medani za kivita na kufanya hujuma dhidi ya Serikali.
Februari 3, 1990 Rais wa Afrika Kusini wa wakati F. W. de Klerk, aliondoa marufuku iliyowekwa kwa ANC na kumwachia huru Nelson Mandela mfungwa wa kisiasa aliyekuwa akitumikia kifungo cha maisha jela.
ANC kwa kushirikiana na vyama vingine kutoka nchi zilizokuwa mstari wa mbele kupigania ukombozi, ilifanikiwa kuhitimisha safari ya makaburu nchini humo na kuondoa sheria zilizokuwa zikichochea ubaguzi na kwa mara ya kwanza nchi hiyo ikaongozwa na rais Mwafrika, Nelson Mandela, mwaka 1994.
Chama hicho bado kinatawala Afrika Kusini na tangu nchi hiyo ilipopata uhuru, imefanikiwa kuulinda uhuru wake, kuwaunganisha wananchi, kukomesha ubaguzi, kutoa haki ya demokrasia kwa viongozi kupishana madarakani kwa njia ya uchaguzi.
Hata hivyo, bado kuna kelele za rasilimali ya madini yaliyopo kwa wingi nchini humo kutowanufaisha ipasavyo wananchi hususani wa kipato cha chini na mara kadhaa kumeshuhudiwa machafuko katika maeneo ya migodi.
Rais wa nchi hiyo aliyekuwa pia kiongozi wa ANC, Jacob Zuma, Februari, 2018 alilazimika kujiuzulu kutokana na tuhuma za rushwa zilizomwandama.
Frelimo
Chama hicho kilichoongoza mapambano ya ukombozi wa Msumbiji kilianzishwa Juni, 1962 jijini Dar es Salaam baada ya kuungana kwa vyama vya Mozambican African National Union (Manu), National Democratic Union of Mozambique (Udenamo) na the National African Union of Independent Mozambique (Unami).
Harakati za Frelimo zilifanikiwa Juni, mwaka 1975 ilipopata uhuru wake kutoka kwa Ureno iliyoitawala nchi hiyo kwa zaidi ya miaka 400.
Baadaye iliingia katika mfumo wa vyama vingi vya siasa mwaka 1990 na kuruhusu vyama vingine kushiriki katika uongozi wa nchi ingawa bado kumekuwapo na changamoto mbalimbali.
Moja ya changamoto hizo ni madai ya ukandamizaji wa haki.
Mpinzani mkuu wa Frelimo ni chama cha Renamo ambacho miaka na miaka tangu Msumbiji ilipopata uhuru mwaka 1975 kimekuwa kikipingana na Serikali na mara kadhaa kuingia katika mapigano ya wenyewe kwa wenyewe. Chama tawala kimeshindwa kutafuta ufumbuzi wa kudumu.
ZANU PF
Mwaka 1984, Zimbabwe chini ya jemedari wake Robert Mugabe ilifanikiwa kujinasua katika ukoloni na kuwa nchi huru baada ya harakati za muda mrefu.
Vyama kama Frelimo, ANC, Swapo na CCM vilitoa mchango mkubwa ikiwamo kuwasaidia kimafunzo wapiganaji wake, kutoa hifadhi na mambo kadhaa ya msingi hadi Zimbabwe ilipokuwa huru.
Licha ya kuudai kwa muda mrefu uhuru kutoka kwa Waingereza, lakini nchi hiyo bado haijapiga hatua kubwa kiuchumi.
Uchumi wa Zimbabwe, umekuwa katika hali mbaya kwa muda mrefu sasa, sekta ya afya imeendelea kulegalega huku uhusiano wake na baadhi ya nchi za Magharibi ukiwa katika hali tete.
CCM
Inatajwa kuwa kiungo, kiongozi na mhimili muhimu wa ukombozi Kusini mwa Afrika. Katika harakati CCM iliyozaliwa mwaka 1977 baada ya kuungana kwa vyama vya Tanu na ASP, ilishiriki kikamilifu kuzisaidia nchi za Kusini kwa namna mbalimbali ikiwamo kutoa hifadhi kwa wapiganaji wake, mafunzo na hata kuridhia nchi hizo kupitishia silaha zao Tanzania wakati wa mapambano hayo.
Urafiki wa Mwalimu Julius Nyerere (Rais wa kwanza wa Tanzania) na baadhi ya viongozi akiwamo Dk Kenneth Kaunda ‘KK’ (aliyekuwa rais wa Zambia) ulimaanisha urafiki katika kuikomboa Afrika. Vyama vya ukombozi kama Zanu, ANC, Swapo na Frelimo vilihifadhiwa nchini.
Licha ya kazi kubwa iliyofanywa na CCM kupigania ukombozi, kulinda uhuru wake na kuanzisha mfumo wa vyama vingi vya siasa, lakini wakosoaji wanakitazama chama hicho kama kilichoshindwa kufanikisha matunda yanayostahili kutokana na rasilimali zilizopo Tanzania.
Tupe Mtazamo wako mdau
0 Comments