Brigedia Jenerali Hashim Mbita bado anaendelea kuheshimika kama shujaa wa harakati za ukombozi barani Afrika, anaheshimika sana Afrika nzima kutokana na uaminifu wake na kujitolea katika kuhakikisha mataifa ya Afrika yaliyokuwa bado chini ya utawala wa Kikoloni yanapata uhuru. Jina la Hashim Mbita ni lenye kuheshimika ndani na nje ya mipaka ya bara la Afrika kuanzia Msumbiji, Sao tome na Principe, Zimbabwe, Angola na Afrika Kusini. Maisha ya Hashim Mbita yanamgusa kila mtu anayeishi katika mataifa hayo ama awe anajua au hajui. Uaminifu na kujituma kwa Mtanzania huyu mzaliwa wa Mkoa wa Tabora katika harakati za ukombozi barani Afrika kuliifanya Tanzania kujivunia na hata kutembea kifua mbele kama moja wapo ya nchi zilizotoa mchango mkubwa katika ukombozi wa bara hili.
Brigedia Jenerali Mstaafu Hashim Mbita alikuwa katibu mtendaji wa kamati ya ukombozi ya Umoja wa nchi za Afrika kwa muda wa miaka ishirini na mbili kuanzia mwaka 1972 hadi mwaka 1994 pale harakati za ukombozi zilipokamilika baada ya kufanyika uchaguzi wa kidemokrasia nchini Afrika Kusini, uchaguzi uliopelekea Waafrika weusi wakiongozwa na Nelson Rolihlahla Mandela kushika hatamu ya uongozi.
Alitunukiwa medali ya Seretse Khama ( Sir Seretse Khama medal )na Jumuiya ya maendeleo ya nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), tuzo ya Mtoto wa Africa (Son of Africa award) kutoka Umoja wa Afrika (AU) mwaka 2014 na tuzo ya Munhumutapa ambayo ni ya heshima ya juu ya Taifa la Zimbabwe anayoweza kupewa raia wa kigeni. Hashim Mbita alipewa tuzo hiyo kwenye mkutano wa SADC uliofanyika kwenye mji wa Victoria falls nchini Zimbabwe mwaka 2014 ikiwa ni kutambua mchango wake katika mapambano ya ukombozi wa bara la Afrika. Kwa kupewa tuzo hiyo aliingia katika orodha ya watu sita pekee kuwahi kutunukiwa tuzo hiyo ambapo ukimtoa Hashimu Mbita wengine ni marais waasisi Mwalimu Julias Nyerere (Tanzania), Augustino Neto (Angola), Seretse Khama (Botswana), Samora Machel (Mozambique) na Kenneth Kaunda (Zambia). Maandishi katika tuzo ya munhumutapa aliyotunukiwa Hashim Mbita yanasomeka kama ifuatavyo:-
"Kwa jukumu muhimu alilotekeleza katika ukombozi wa kikanda pamoja na ushirikiano wakati wa uongozi wake wa miaka 20 kama Katibu Mtendaji wa Kamati ya ukombozi ya Umoja wa nchi huru za Afrika (OAU) - mtangulizi wa Umoja wa Afrika (AU).”
Kamati hiyo ya Ukombozi ya umoja wa Afrika iliendesha shughuli zake ikitokea jijini Dar es salaam kwa mwaliko wa rais wa kwanza na Baba wa Taifa la Tanzania hayati Julius Kambarage Nyerere ambaye alikuwa mwalimu , mshauri na kamanda wa Hashimu Mbita. Kamati hiyo ya ukombozi ilifanya kazi ya kuratibu misaada ya vifaa kwa ajili ya wanapigania uhuru kwa kipindi cha miaka thelasini kuanzia mwaka 1963 hadi mwaka 1994 ambapo inaelezwa kuwa bila hiyo misaada baadhi ya nchi za kusini mwa Afrika zingeendelea kuwa chini ya utawala wa Kikoloni.
Mara baada ya kuteuliwa kuongoza kamati ya ukombozi, ambayo moja ya kazi zake ilikuwa ni kutafuta vikundi vya ukombozi katika mataifa ya Afrika yaliyokuwa yakitawaliwa na wakoloni, Brigedia Jenerali Hashim Mbita alishiriki kuvijenga vikosi vya SWAPO(Namibia), MOLINACO (Comoro), PAIGC (Guinea Bissau na Cape Verde), Frelimo (Msumbiji), ANC (Afrika Kusini), ZANU-PF (Zimbabwe) na MPLA (Angola)n.k. Aliviandaa vikosi hivi kupambana na majeshi makubwa yenye silaha nzito za kisasa kwa wakati huo. Alichochea hamasa kubwa katika mapambano ya ukombozi kusini mwa Afrika kwa kutembelea maeneo yaliyokombolewa kaskazini ya Msumbiji yaliyokuwa chini ya chama cha Frelimo (Mozambique Liberation Front au kwa Kireno “Frente de Libertação de Moçambique”) akitaka kushuhudia kwa macho yake hali ilivyokuwa katika uwanja wa mapambano na kuangalia ni aina gani ya mahitaji yaliyokuwa yakihitajika.
Alibaini kuwa kikwazo kikubwa kilichowasumbua wapiganaji wa Frelimo ni mashambulizi ya anga dhidi yao yaliyokuwa yakifanywa na ndege za kivita za wakoloni wa Kireno. Hivyo alifanya juhudi za kuwapatia wapiganaji silaha zilizowawezesha kukabiliana na mashambulizi hayo, hivyo kuviwezesha vikosi vya Frelimo kusonga mbele zaidi hatua iliyofanya maofisa wa kijeshi wa Ureno kutambua kuwa hali katika medani ya vita imeshabadilika na kwamba wasingeweza tena kushinda vita vya ukoloni barani Afrika.
Hali hii iliwalazimu Wareno kusalimu amri na kuanzisha majadiliano na chama cha Frelimo kwa ajili ya kuunda serikali ya mpito iliyochukua madaraka mwaka 1974 na hatimaye kupelekea uhuru kamili wa Msumbiji mwezi Juni, mwaka 1975. Mipango madhubuti ya Kamati ya ukombozi ya umoja wa nchi za Afrika chini ya Hashimu Mbita ilipelekea kupatikana kwa uhuru wa Sao Tome na Principe mwezi Julai mwaka 1975, Angola mwezi November mwaka 1975, Uhuru wa Zimbabwe mwaka 1980, uhuru wa Namibia mwaka 1990 na hatimaye uchaguzi wa kidemocrasia huko Afrika ya kusini mnamo mwaka 1994.
Kwenye mkutano uliofanyika Arusha mwezi August mwaka 1994 kwa ajili ya kuhitimisha shughuli za kamati ya ukombozi, Brigedia jenerali Hashim Mbita alisoma hotuba iliyopewa jina “Jukumu limekamilika” kupitia hotuba hiyo Mpambanaji Hashim Mbita hakusita kuwaenzi mashujaa wenzake katika harakati za ukombozi barani Afrika waliopatwa na umauti kabla ya kushuhudia uhuru katika mataifa waliyokuwa wakiyapigania. Mashujaa hao ni Amilcal Cabral (Guinea Bissau), Herbert Chitepo, Jason Ziyaphapha Moyo, Josiah Tongogara (Zimbabwe), Eduardo Mondlane (Msumbiji), Steve Biko, David Sebeko aliyejulikana kama "Malcolm X wa Afrika Kusini”, Solomon Mahlangu, Christ Hani, Duma Nokwe ambaye alikuwa katibu mkuu wa ANC kati ya mwaka 1958 hadi 1969, Johnny Makatini na Oliver Reginald Kaizana Tambo (Afrika Kusini), mwingine ni Kamanda Peter Nanyemba wa Namibia.
Hashim Mbita, ambaye baba yake alikuwa karani wa shirika la reli la Tanganyika, alizaliwa mwaka 1933 mkoani Tabora na kupata elimu yake kwenye shule ya watoto wenye vipaji ya Tabora boys. Alijiunga na chama cha TANU mwaka 1958 na kuhamia Dar es salaam mwaka mmoja kabla ya uhuru wa Tanganyika wakati huo vijana hasa wanaume wakiajiriwa kwenye mafunzo ya huduma katika utumishi wa kiraia ikiwa ni katika hatua za maandalizi ya uhuru wa Tanganyika mwezi December 1961.
Alipangiwa kazi kwenye kitengo cha habari cha wizara ya habari na muda mfupi baadaye aliteuliwa kuwa mwandishi wa habari wa Rais Julius Kambarage Nyerere akiandaa mikutano na waandishi wa habari hasa nyakati za ziara rasmi za viongozi wa Serikali kutoka nje ya Tanzania. Moja wapo ya mikutano yake na waandishi wa habari yenye kukumbukwa sana ni ule alioandaa wakati wa ziara ya Waziri mkuu wa China Zhou Enlai (tamka Chou En-lai) mwezi June mwaka 1965.
Hashimu Mbita alipanda cheo ndani ya chama na serikali hadi kuwa Katibu mtendaji Mkuu wa TANU kabla Rais Julius Nyerere kumpeleka katika Jeshi la Ulinzi la Wananchi kuwa mkuu wa kitengo cha siasa (political commissar). Alipata mafunzo ya kijeshi hapa Tanzania na baadaye alipelekwa Uingereza kutoka Ikulu kwa lengo la kusaidia kulijenga Jeshi la Wananchi Tanzania liwe la kizalendo baada ya maasi ya mwaka 1964.
Baadaye rais Julius Kambarage Nyerere alimuandaa kwa jukumu muhimu zaidi kuliko yote, nalo ni kazi ya katibu mtendaji wa kamati ya ukombozi ya umoja wa nchi za Afrika. Kazi ambayo aliifanya kwa moyo na kujituma na hatimaye kumtambulisha kitaifa na kimataifa kama alama ya ukombozi (Liberation icon) ya Tanzania na Afrika.
Mwanadiplomasia Hashim Mbita ambaye aliwahi kuwa balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe alifariki siku ya Jumapili, tarehe 26 April mwaka 2015 akipatiwa matibabu kwenye hospitali kuu ya Jeshi Lugalo Jijini Dar es salaam akiwa na umri wa miaka 81 na kuzikwa kwenye makaburi ya Kisutu, jijini Dar es salaam. Mwenyezi Mungu ailaze mahala pema roho ya marehemu Brigedia Jenerali Hashim Mbita.
Makala hii nimeiandika kwa msaada mkubwa wa taarifa kutoka Southern African Research and Documentation Centre (SARDC). Shukrani za dhati ziende kwa rafiki yangu ndugu Hillary A. Silayo aliyeniomba kuandika makala hii.
Ukinakili Makala zangu kumbuka kufanya acknowledgment.