Nimemaliza kusoma kitabu cha INTO AFRICA: The Dramatic Retelling Of The Stanley - Livingstone Story cha Martin Duggard. Ukweli ni kwamba, Chuma na Susi hawakufika kamwe Uingereza.
Chuma na Susi waliufikisha mwili wa Dr. David Livingstone pwani ya Bagamoyo mwezi Februari 1874. Dr. David Livingstone alifariki usiku wa manane panapo Mei 1, 1873. Alifariki akiwa amepiga magoti akisali.
Chuma alifahamu juu ya mauti ya mmishenari na mpelelezi huyo maarufu zaidi majira ya saa 10 alfajiri.
Mtu mwingine aliyekuwa kwenye msafara wa Dr. Livingstone akifahamika kwa jina la Farijala aliutoboa mwili wa Dr. Livingstone juu kidogo ya sehemu zake za siri. Kwa uangalifu mkubwa sana, akauvuta utumbo hadi alipofanikiwa kuutoa moyo wake. Akaweka chumvi ndani kwenye shimo kuzuia mwili kuharibika.
Daktari aliyeufanyia uchunguzi mwili wa Dr. Livingstone baada ya kuwasili Uingereza mwezi Aprili 1874 alistaajabishwa sana na maarifa yaliyotumika maporini huko Afrika kuuhifadhi mwili wa mvumbuzi huyo maarufu.
Akauhifadhi kwenye sanduku la chuma ambalo Dr. Livingstone alilitumia kuhifadhi nyaraka zake. Moyo ulizikwa chini ya mti pahala hapo. Farijala, akisaidiana na Chuma, Susi na wengineo, akaikunja miguu ya Dr. Livingstone ili iwe rahisi kuibeba.
Sababu ya kuamua kuurudisha mwili badala ya kuuzika papo hapo, ni moja. Dr. Livingstone katika siku za mwisho za uhai wake, alikuwa na shauku kubwa ya kurudi kwao Uingereza.
Lakini, kwa kuwa Dr. Livingstone alikuwa na mapenzi makubwa na Afrika, moyo wake ulibaki Afrika.
Susi akabaki Bagamoyo na mwili. Chuma akavuka hadi Zanzibar kwa minajili ya kumfahamisha Balozi wa Uingereza, John Kirk. Hakumkuta. Kirk alikuwa likizo.
Akakutana na msaidizi wake, Kepteni W. F. Prideaux. Kepteni akaagiza meli ya HMS Vulture iende Bagamoyo kuutwaa mwili wa Dr. Livingstone.
Mwili ulipowasili Unguja, Prideaux akawafukuza kazi Chuma, Susi na timu nzima iliyousafirisha mwili wa Dr. Livingstone kutoka kijiji cha Chifu Chitambo huko Ilala, Zambia hadi Bagamoyo. Wala hakujali miezi 9 ya mateso kwa watu hao wakiusafirisha mwili wa Dr. Livingstone.
Hivyo, wawili hao, Chuma na Susi hawakuhudhuria mazishi ya Dr. Livingstone yaliyofanywa Westminster Abbey, London nchini Uingereza siku ya Jumamosi, Aprili 18, 1874.
Mazishi hayo yaliyohudhuriwa na Malkia Victoria, ndiyo yaliyokuwa mazishi makubwa zaidi ya wakati huo.
Kwa nyongeza, safari ya Henry Morton Stanley kumtafuta Dr. Livingstone inaelezwa kuwa mapinduzi ya kwanza makubwa ya habari za uchunguzi.
Huku, kazi za Dr. David Livingstone zilileta matokeo makubwa miaka 10 baada ya kifo chake pale ugawanywaji Afrika ulipofanyika.
Dr. David Livingstone ndiye binadamu pekee aliyepata kuishi ambaye maeneo mengi zaidi yameitwa kwa jina lake ikiwamo mitaa, vyuo, miji na kadhalika.
Dr. Livingstone alipata mtoto mmoja wa kiume akiwa Afrika, na mwanamke wa Kimanyema (Dr. Livingstone aliwasifia sana wanawake wa Kimanyema katika maandishi yake). Alikuwepo hata wakati wa kifo chake. Lakini, Dr. Livingstone hakuandika popote habari za huyo mtoto wake 'half caste'. Hivyo, habari zake zimeendelea kuwa hazijulikani kwa kina.
Hitimisho:
Chuma na Susi hawakupewa heshima wala shukrani waliyoistahili.
Chuma na Susi hawakupewa heshima wala shukrani waliyoistahili.
0 Comments