Jina lake ukamilifu ni Abeid Amani Karume. Alizaliwa Agosti 4, 1905 katika kitongoji cha Pongwe huko Mwera Wilaya ya Magharibi “A” Zanzibar.

Moja ya matukio muhimu ya kihistoria yaliyowahi kutokea ndani ya Zanzibar ambayo hata mtoto wa darasa la kwanza anatambua ni kifo cha Mzee Abeid Amani Karume ambaye aliuawa Aprili 7, 1972, siku ambayo sio rahisi kuisahau.
Mzee Karume alikuwa nani?
Jina lake ukamilifu ni Abeid Amani Karume. Alizaliwa Agosti 4, 1905 katika kitongoji cha Pongwe huko Mwera Wilaya ya Magharibi “A” Zanzibar.
Ni mtoto wa kwanza kuzaliwa katika familia ya watoto watano ya Amani Karume na Amina bint Kadir (Amina Kadudu). Kati ya ndugu zake hao wanne wa baba mmoja na mama mmoja, wanaume walikuwa wawili na wanawake wawili na wote walifariki kabla ya Mzee Karume kuuawa mwaka 1972.
Ndoa ya Karume
Kwa mara ya kwanza ya Mzee Karume alifunga ndoa na Pili Bint Ahmed Ambari mwanzoni mwa miaka ya 40. Mke wa pili alikuwa Ashura bint Maisara. Baada ya kutengana na wake hao wawili, Karume alifunga ndoa na Fatma bint Gulamhussein Ismail (Fatma Karume) mwishoni mwa Novemba 1944.
Harusi ya wawili hao ilifanyika Bumbwini Misufini na makazi ya Mzee Karume na mkewe yalikuwa mtaa wa Kisimajongoo, nyumba No 18/22 Mjini Unguja.
Fatma Karume alizaliwa Bumbwini mwaka 1929 katika familia ya Gulamhussein Ismail na Mwanasha Mbwana Ramadhani.
Harakati za elimu
Kama ilivyokuwa kwa binadamu katika kutafuta elimu, Mzee Karume alikuwa hivyo hivyo, kwa mujibu wa mwalimu wa Chuo cha Habari Zanzibar, Ali Shaabani, Mzee huyo alianza masomo yake mwaka 1909 katika shule ya Mwera mwaka ambao ndio aliofariki baba yake mzazi.
Katika mwaka 1913 wakati akiwa na umri wa miaka minane, mama yake, Amina alimpeleka mjini Unguja kuendelea na masomo ambapo alitumia miaka mitatu tu hadi kumaliza hadi darasa la saba.
Harakati za kazi
Baada ya Mzee Karume kumaliza masomo yake ya darasa la saba, alionekana kuvutiwa na kazi za Bandari na wakati huo Bandari ya Zanzibar ndio ilikuwa kubwa Afrika Mashariki na kituo kikuu cha biashara katika eneo zima la Afrika Mashariki.
Lakini pia meli za Marekani, Uingereza, Ufaransa na Italia zilitia nanga Zanzibar kupakia na kupakuwa bidhaa mbalimbali, huku meli nyingine zilifika kuchukua maji safi ya kunywa yatokayo katika chemchem ya Mwanyanya.
Mzee Karume kwa vile alipendelea kazi ya ubaharia alimuomba Mzee Juma afuatane naye ili kumuunganishia kazi japo ya kibarua katika meli zinazofika bandarini Zanzibar. Ombi lilikubaliwa na alichukuliwa na kupata ajira ya muda.
“Kutokana na kazi yake hiyo Karume alikutana na mabaharia wa nchi mbalimbali na hivyo kuvutiwa na uzuri wa maisha ya ubaharia hali ambayo ilimfanya kuomba ruhusa kwa mama yake ili afanye kazi melini.
Mwanzoni mama yake alikataa ombi hilo, lakini baadae alikubali baada ya kuambiwa kuwa mwanawe hatasafiri maeneo ya mbali ya Zanzibar,” anasema Ali Shabani mwalimu wa chuo cha habari Zanzibar.
Katika mwaka 1920, Karume alikubaliwa kuwa baharia na kufanya kazi katika meli ya Golden Crown pamoja na kampuni nyingine mbalimbali.
Mzee Karume aliendelea kufanya kazi hiyo mpaka mwaka 1938 alipoacha kazi hiyo baada ya kupokea ushauri wa mama mzazi kuacha kazi hiyo kutokana na kuzorota kwa hali ya usalama duniani.
Harakati za ukombozi
Kwa mujibu wa mwalimu wa chuo cha habari Zanzibar, Ali Shabaani harakati za Mzee Karume za kuanza kwa ukombozi kwa wanyonge zilianza rasmi mwaka 1939.
Baada ya kuwashauri wenzake, Karume alipata watu sita waliokubali kujiunga naye katika chama cha mabaharia wa Unguja na Pemba.
Watu hao ni Bakar Jabu, Miraji Mselem, Juma Maalim, Ismail Mbarouk, Mbaruku Salim na Kitwana Suwedi. Chama kilipata usajili Agosti 30, 1949 na makao makuu yake yalikuwa Kisima Majongoo.
Ushiriki katika siasa
Kuundwa kwa Chama cha Zanzibar Nationalist Party (Hizbu) mapema katika miaka ya 50 na kutolewa kwa mapendekezo ya kufanyika uchaguzi mkuu wa kwanza wa Zanzibar katika mwaka 1957, kuliwafanya viongozi wa Jumuiya ya Waafrika, Afrika Association waone umuhimu wa kushirikiana.
Viongozi hao waliona ulazima wa kuungana kuwa kitu kimoja kupigania uhuru, hivyo Jumuiya ya Shirazi Association ilimtuma Haji Hatibu aliyekuwa rafiki mkubwa wa Abeid Karume apeleke wazo la kuunganisha Jumuiya ya Waafrika na jumuiya ya Washirazi.
Kabla ya kukutana kila Jumuiya ilifanya kikao cha faragha kujadili ajenda ya mkutano walikubaliana kupendekeza jina la Abeid Karume kutoka African Association kuwa Rais wa chama kilichokuwa kinaundwa.
African Association walipanga kupendekeza jina la Sheikh Ameir Tajo kutoka Shirazi Association kuwa Rais wa chama kipya, viongozi wa Jumuiya hizo walikubaliana kukutana kuanzia Febuari 1 mpaka 5, 1957.
Mkutano ulifanyika kama ulivopangwa hapo Muembekisonge nyumbani kwa Karume chini ya mwenyekiti Muhidini Ali Omar. Kwa wakati huo, nyumba hiyo ya Abeid Karume aliishi Hija Saleh na Haji Ali Mnonga.
Mkutano huo ulimalizika jioni ya Febuari 5, 1957 kwa viongozi hao kukubaliana kuunganisha Shirazi Association na African Association na kuunda chama kilichoitwa Afro-Shirazi Union badaye chama hicho kiliitwa Afro-Shirazi Party (ASP).
Chama cha Afro-Shirazi Party kilimteua Karume kuwa Rais wa chama, Mtoro Rehan Kingo kuwa Makamu na Thabit Kombo Jecha kuwa Katibu Mkuu.
Mwaka 1947 ziliundwa serikali za mitaa na Baraza la Manispaa lilianzishwa mwaka 1954, Abeid Karume alichaguliwa kuwa diwani. Juni 1957, Karume alikwenda Ghana kuhudhuria sherehe za uhuru wa taifa hilo. Safari hiyo ilikuwa ni mwaliko wa kiongozi wanchi hiyo, Kwame Nkrumah kwa vyama vyote vya kupigania uhuru barani Afrika.

+image
Mwaka huo huo alipendekezwa na chama cha ASP kuwa mgombea wa kiti cha baraza la kutunga sheria kwa jimbo la ng’ambo, katika uchaguzi mkuu wa kwanza wa Zanzibar 1957 na alishinda.
Abeid Karume alichaguliwa tena kuwa mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria katika uchaguzi wa pili wa Januari 1961, katika jimbo la Jang’ombe kwa tiketi ya ASP.
Mara tu baada ya kumalizika uchaguzi huo 1961 uliokuwa na utatanishi wa kuunda Serikali ya pamoja, Karume alichaguliwa kuwa Waziri wa Afya na mambo ya kienyeji katika Serikali ya pamoja kwa miezi sita. Uchaguzi mkuu wa tatu wa Zanzibar ulifanyika Juni 1, 1963.
Karume alichaguliwa tena kuwa mjumbe wa Baraza la kutunga sheria katika jimbo la Kwahani na Jang’ombe. Akiwa Waziri wa Afya, Karume alishughulikia afya, ujenzi wa nyumba, ajira, serikali za mitaa na serikali za wilaya.
Wakati wa matayarisho ya mapinduzi 1964, Abeid Karume alikuwa mwenyekiti wa kamati ya watu 14 waliotayarisha mapinduzi hayo kwa siri.
Akiwa na umri wa miaka 59, Karume aliongoza mapinduzi ya mwaka 1964 na alitangazwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi na vilevile kubaki na wadhifa wake wa Rais wa Afro-Shirazi Party.
Mwanahabari nguli, Mzee Enzi Talib anasema Mzee Karume alikuwa na moyo wa pekee na wa huruma kiasi cha kwamba anashindwa kumfananisha na yeyote yule hadi leo.
Anasema mengi ameyafanya kwa maslahi ya kuwakomboa wananchi ambaowalionekana kunyanyasika katika tawala zilizotangulia.
Mzee Karume aliuawa akiwa na umri wa miaka 67, akiwa katika jengo la makao makuu ya ASP Kisiwandui.