Zaidi ya miongo mitatu baada ya matukio tuliyoyazungumza katika sura chache zilizopita, kama itatubidi tuviamini vyombo vya habari, Zanzibar hivi sasa inaonekana kuwa imepiga hatua kubwa sana kuelekea kwenye mafanikio. Sasa, nini kilichobadilika? Na nini kilichobaki vile vile?
Hebu natuangalie kwa ufupi katika baadhi ya mabadiliko muhimu ya kisiasa katika kipindi cha miaka 39 iliyopita. Mwezi Februari 1977 chama cha ASP kiliungana na TANU na kuunda Chama cha Mapinduzi (CCM) na kuanzia wakati huo hadi hivi sasa Visiwani na Bara wameendelea kuwa chini ya utawala wa CCM. Mwaka 1992 mfumo wa vyama vingi ulianzishwa na kuundwa chama kipya cha CUF. Chama cha CUF kilijitangaza kuwa ndiyo sauti ya wananchi wa visiwani – lakini hakikuwakilisha wananchi wote. Eneo lake la uchaguzi, ijapokuwa lina nguvu, limebaki karibu kuwa kama lile la mchanganyiko wa ZNP-ZPPP ambao Muingereza aliuacha madarakani kabla ya mapinduzi ya 1964. Tokea mwaka 1992, kila uchaguzi umeambatana na vurugu na tuhuma za udanganyifu.
Babu alieleza kwa muhtasari juu ya hali ya baada ya uchaguzi wa mwezi Oktoba 1995 kama ifuatavyo:
Mtu hataacha kuona mshabaha wa kutisha wa kihistoria na ule wa miaka ya 1960. Tofauti na Bara, Zanzibar mlingano wa nguvu za kisiasa haukubadilika hata kidogo…. Ikiwa Bara takriban wanachama wote wa vyama vya upinzani waliiacha CCM kwasababu za kiitikadi au sababu nyengine zozote, Zanzibar hali ilikuwa tofauti … Hapa mgawanyiko wa zamani wa kivyama na utiifu … vimebaki vile vile kama ilivyokuwa mwaka 1964 … Kama CUF ni mtoto wa ZNP-ZPPP, CCM ya Zanzibar ni ASP katika kanzu mpya ikiongozwa na mchanganyiko wa uongozi wa wanaotaka maendeleo na wanaopinga maendeleo … Hata mabishano ya kisiasa yanaendeshwa kwa lugha ile ile ya zamani ya uhasama na ghadhabu. (Babu, 1995: 12)
Mwaka 2000 vurugu za baada ya uchaguzi ziliongezeka, huku serikali ikiyapiga risasi makundi ya waandamanaji na kuua watu 35 na kujeruhi 600. Uchaguzi wa mwaka 2005 nao pia ulishuhudia matukio ya vurugu kubwa. Lakini uchaguzi wa 2010 ulikuwa tofauti; hapajakuwepo na vurugu na kusema kweli, ni matokeo ya mfululizo wa maendeleo makubwa ya kisiasa, hivi sasa Zanzibar ina Serikali ya Umoja wa Kitaifa inayowajumuisha viongozi wa CCM na CUF. Vipi mabadiliko haya yamepatikana? Kwa nini vyama viwili hivi ambavyo viongozi wake wamekuwa mahasimu wakubwa, vimekuja pamoja? Na ishara gani inatupa uingiliaji kati wa Marekani na Uingereza katika mambo ya Zanzibar katika miaka ya 1960 kutusaidia kuielewa hali ya sasa ya kisiasa? Haya ndiyo maswali tutakayojaribu kuyaeleza kwa ufupi katika sura mbili zijazo na kuzieleza kwa mukhtadha wa kubadilika kwa umbo la nguvu za ubeberu hivi sasa.
Kwa mujibu wa maelezo rasmi yote, kufikiwa kwa ‘makubaliano’ kati ya CCM na CUF ilikuwa ni kazi ngumu. Mwezi Machi 2010, Baraza la Wawakilishi la Zanzibar lilipitisha azimio lililoweka muundo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa na kuweka utaratibu wa kupiga kura ya maoni kuwauliza wananchi wa Zanzibar kuchagua kwa kura ya ndiyo au hapana juu ya makubaliano kati ya vyama viwili vikubwa, kuwa vyovyote matokeo ya uchaguzi yatakavyokuwa serikali nyengine itakayokuja madarakani itakuwa ni ya mseto. Baadaye iliundwa Kamati ya Watu Sita kutekeleza ‘makubaliano’ hayo.
Tarehe 30 Julai 2010 ilifanyika kura ya maoni iliyoshirikisha asilimia 71.9 ya wapiga kura na asilimia 66.4 walipiga kura ya ndiyo. Wakati katika chaguzi zilizopita pamekuwepo na watazamaji wa kimataifa, mara hii pamekuwepo na mradi, Mradi wa Kusaidia Uchaguzi 2010, uliofadhiliwa na kusimamiwa na nchi za wafadhili na wawekezaji na mashirika ikiwa ni pamoja na Kanada, Denmark, Tume ya Ulaya, Finland, Uholanzi, Norway, Sweden, Uswisi, Uingereza na Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa. Uliendeshwa chini ya uzimamizi wa Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa Tanzania.
Hatimaye, tarehe 31 Oktoba uchaguzi wa rais ulifanyika. Ulizaa serikali ya mseto iliyotayarajiwa. CCM kilikuwa na kura zaidi, kwa hivyo mgombea wa CCM Dk. Ali Mohamed Shein akawa rais wakati mgombea wa CUF Seif Sharif Hamad akawa makamo wa rais. Na baadae, tarehe 28 Februari 2011 viongozi walipongezwa na Marekani. Balozi wa Marekani Alfonso Lenhardt alitoa tunzo ya Martin Luther King kwa ‘Kamati ya Watu Sita’ ambayo kwa mujibu wa maneno ya balozi huyo kamati hiyo ilikuwa ni ‘kundi la vyama viwili la wananchi walioweka pembeni siasa za vyama ili kufanya kazi ngumu ya kuyatekeleza masikilizano’ (Mjasiri, 2011).
Ali Mzee Ali, mwenyekiti wa CCM wa Baraza la Wawakilishi ambaye mwaka mmoja tu kabla aliwaambia watumishi wa serikali ya Marekani kwa siri kuwa CUF ‘hakikuwa chama halisi bali ni kundi la wana CCM waliojitenga wenye kupigania maslahi yao binafsi’ (Ubalozi wa Marekani, 2009b), alitoa hotuba ya kuikubali tunzo hiyo kwa niaba ya Kamati. Alisema kuwa ‘uongozi wa viongozi wa Zanzibar wa vyama vyote CCM na CUF uliweza kuzisoma alama za wakati ili kuyaepuka mapinduzi yanayotokea katika Afrika ya Kaskazini. Alisema pia, huku akichekesha juu ya utaratibu huo, kuwa serikali mpya ilikuwa ni urithi na dira ya Marehemu Abeid Amani Karume ambaye siku zote amekuwa akitambua umuhimu wa usawa, maelewano na umoja nchini Zanzibar’. Zanzibar, alisema ‘tayari ni asasi na mfano wa demokrasia kwa nchi nyengine kuiga!’ (Mjasiri, 2011).
Kusema kweli, haikuwa Kamati ya Watu Sita peke yake iliyofanyakazi kwa bidii ili kuweza kupata matokeo haya. Kama zinavyoonyesha nyaraka za siri za Marekani zilizopatikana kutoka WikiLeaks, Wamarekani na wenzao wa Ulaya, wakiwa na wasiwasi na rasilimali zao walizoziwekeza katika kanda hii na hasira za wale wanaokandamizwa na vikundi vilivyotengwa katika jamii, walifanyakazi kwa bidii vile vile, huku kwa mfululizo wakifuatilia na kuyasawazisha mambo. Katika sura hii na sura ifuatayo tunaangalia baadhi ya nyaraka hizi na kuzichunguza ili kujua zinatuambia nini kuhusu wasiwasi mkubwa wa Marekani uliopo hivi sasa na kuhusu mabadiliko na uendelezwaji wa mikakati ya wabeberu katika Afrika ya Mashariki.
‘Maendeleo’ Zanzibar na Tanzania Bara Hivi Sasa
Zanzibar bado ni mahali muhimu lakini sio tena kituo muhimu cha uchumi kinachoshamiri na kujiamini kama ilivyokuwa katika miaka ya 1960. Viwanda na kilimo vyote vimeporomoka. Biashara ya karafuu imekufa. Utalii una maana ya kuwa ardhi nzuri iliyo katika fukwe za bahari imechukuliwa na mahoteli, ukivuruga maisha ya kimila ya wananchi na badala yake kuwaletea tija ndogo sana.
Mpango wa Kupunguza Umasikini wa Zanzibar ulioanzishwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa na Idara ya Maendeleo ya Kimataifa ya Uingereza (DfID) mwaka 2003 ni jukwaa la wafadhili ambalo shughuli zake zimejikita katika kufungua ofisi kwa ajili ya watumishi, kuandaa utaratibu wa ‘kufuatilia umasikini’ na kuweka miundombinu ya kusimamia misaada. Umasikini bado ni mkubwa na umezagaa. Pemba ambayo kwa kiasi fulani ilikuwa na neema kabla ya miaka ya udikteta wa Karume hivi sasa imekuwa aghasi kuliko Unguja, ikiwa ina rasilimali hafifu na miundombinu michache. Kwa mujibu wa Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali ya Zanzibar, asilimia 74 ya watu katika wilaya iliyo masikini kuliko zote za Pemba, Micheweni, wanaishi chini ya kiwango cha mahitaji muhimu kabisa cha umasikini (Wizara ya Kazi, Vijana, Watoto na Maendeleo ya Wanawake, Zanzibar, 2007).
Kusema kweli, leo kama ilivyokuwa katika miaka ya 1990, Tanzania kwa jumla ni moja ya kanda zilizokuwa masikini sana duniani ambapo asilimia 42 ya watoto walio chini ya umri wa miaka 5 Bara, wamedumaa (TDHS, 2004/05; 218) na kwa kila vizazi 100,000, wanawake 578 wanakufa kwa uzazi, moja kati ya viwango vikubwa sana vya vifo vya uzazi katika Afrika (TDHS, 2009/10).
Nchi bado inategemea sana kilimo, na miaka 50 baada ya uhuru mazao ya biashara ya kikoloni bado yanawakilisha asilimia 85 ya bidhaa zinazosafirishwa nje.
Visiwani Zanzibar, watu mara nyingi husema kuwa Zanzibar imetengwa katika maendeleo wakati Bara inaneemeka. Lakini ukweli ni kuwa hakuna iliyoneemeka, si Bara wala si Visiwani. Awamu ya Nyerere ya Azimio la Arusha imeuharibu sana uchumi, kama tulivyoona. Katikati ya miaka ya 1980 kutokana na shinikizo la Shirika la Fedha la Kimataifa, Benki ya Dunia na wafadhili, serikali ikiwa chini ya mrithi aliyemteua Nyerere mwenyewe, Ali Hassan Mwinyi, ilianza mchakato wa kubinafsisha uchumi. Sera za kurekebisha uchumi, zilipelekea nchi kupunguza huduma za jamii na taratibu kufungua milango yake kwa rasilimali ya dunia chini ya usimamizi wa Shrika la Fedha la Kimataifa. Hata hivyo, mara serikali ilianza kutuhumiwa kwa kukosa kuwa na nia thabiti ya ‘kuleta mabadiliko’. Ilipofika mwaka 1994, mahusiano na mashirika ya misaada, asasi za fedha na Shirika la Fedha la Kimataifa yaliharibika sana; kwa kiasi fulani, kwasababu ya uzembe wa serikali uliosababisha ishindwe kuyafikia matakwa yao.
Mrithi wa Mwinyi, Benjamin Mkapa, naye pia alichaguliwa na Nyerere mwenyewe, ambaye ingawa alikuwa amestaafu lakini bado alikuwa ni mtu mwenye udhibiti mkubwa wa siasa za Tanzania mpaka kufa kwake mwaka 1999. Mkapa alifanikiwa katika kutii amri za asasi za fedha za kimataifa. Alibinafsisha mashirika ya umma kwa ari kubwa na kupora, kwa kushirikiana na aliyekuwa waziri wake wa fedha, mgodi wa makaa ya chuma wa Kiwira uliokuwa, wakati huo wenye kuingiza fedha nyingi (Kaijage, 2012). Kwaubinafsi shaji sehemu kubwa ya Tanzania iliuzwa kwa majambazi mabwanyenye wanaomiliki rasilimali za dunia. Uporaji wa ardhi na rasilimali za Tanzania uliofuatia tokea wakati huo ni wa kiwango kikubwa sana.
Dhahabu ni sehemu moja tu ya uporaji huu. Tanzania ni ya tatu kati ya nchi zenye dhahabu nyingi katika Afrika baada ya Afrika ya Kusini na Ghana, na kilichozikumba rasilimali hizo chini ya utawala wa Mkapa ni mfano hai wa kile kinachoitwa mfumo huru mambo leo katika nchi hii. Mwaka 1975 machimbo ya kwanza yaligunduliwa na wachimbaji wadogo wadogo katika eneo la Bulyanhulu la Tanzania. Mwanzoni serikali iliwashajiisha wachimbaji hao kuchimba. Hata hivyo, pale shirika la Canada la Sutton Resources lilipoonesha nia ya kulitaka eneo hilo, serikali ilipeleka kikosi cha wanajeshi kuwaondoa wachimbaji hao, juu ya kuwepo amri ya Mahakama Kuu iliyotambua haki yao ya kuchimba katika eneo hilo. Muda mfupi baadae Sutton Resources, kwa idhini ya serikali walipeleka tingatinga kuufunga mgodi huo. Hii ilisababisha kuwepo tuhuma ya mauaji ya wachimbaji wadogo wadogo waliokwama ndani ya mgodi (Lissu, 2002).
Mwaka 1999 Shirika la Barrick Gold liliuchukua mgodi huo. Hatua hii ilifuatiwa na uwekezaji wa Dola za Kimarekani milioni 280 na benki za kimataifa; na bima ya kujikinga na matukio ya hatari za kisiasa ya Dola za Kimarekani milioni 345 na Idara ya Bima kwa Sekta Binafsi ya Benki ya Dunia, Shirika la Mataifa Mbalimbali la Kutoa Uhakika wa Uwekezaji (MIGA) na Shirika la Serikali ya Canada la Kuendeleza Usafirishaji wa Bidhaa Nchi za Nje. Mwaka 2000 mgodi wa dhahabu wa Geita nao pia ulianza uzalishaji, mwanzoni ukiwa ni mradi wa ubia wa AngloGold na Ashanti na baadae kuungana kwa makampuni hayo mawili mwaka 2004 chini ya umiliki wa AngloGold Ashanti (AGA). Yote haya yalikuwa ni kwa mujibu wa makala ya kitaalamu ya mwaka 1992 juu ya Mkakati wa Afrika Kuhusu Uchimbaji wa Migodi, yaliyoandikwa na Benki ya Dunia na Shirika la Fedha la Kimataifa na Sheria ya Uchimbaji Madini ya 1998 ya Tanzania iliyoandikwa na wawekezaji na kufuatiliwa na Benki ya Dunia (Mgamba, 2012).
Sasa, Tanzania imepata nini kutokana na yote hayo? Mali iliyotengenezwa na Barrick Gold na AngloGold Ashanti nchini Tanzania kutoka mwaka 2004 hadi 2009 inatoa dalili za kimwelekeo. Katika kipindi hiki Dola za Kimarekani bilioni 2.5 kwa njia ya dhahabu zilisafirishwa nje, hasa kwa kupitia makampuni mawili haya lakini serikali ilipata kiasi cha wastani wa Dola za Kimarekani milioni 21-22 tu kwa mwaka. Kusema kweli, Barrick walishindwa kuonyesha malipo ya mrabaha na kodi kwa serikali huku meneja mkuu wake Greg Walker akitangaza mwaka 2008 kuwa kampuni ’itaanza kulipa kodi za makampuni mwaka 2014 tutakapoanza kupata faida’! (Sharife, 2009). AGA inazalisha wakia milioni 3 za dhahabu kutoka katika mgodi wa Geita, zenye thamani ya Dola za Kimarekani bilioni 1.43 kwa mujibu wa bei ya dhahabu ya hivi sasa, na walilipa kodi ya wastani wa Dola za Kimarekani milioni 13 kwa mwaka, kiasi ambacho ni kasoro ya asilimia 0.001 ya mapato yote (Sharife, 2009). Ikiwa hazina ya Tanzania ilikuwa na inaendelea kuibiwa mabilioni ya Dola za Kimarekani, unyonyaji wa dhahiri wa thamani ya ziada inayozalishwa na wafanyakazi wa Tanzania mashambani na katika migodi ni jambo la kushtusha zaidi. Ikiwa wastani wa marudisho ya rasilimali katika nchi zenye uchumi ulioendelea ni kiasi cha asilimia 5 (kutokana na unyonyaji wa wafanyakazi katika nchi hizi), katika nchi kama Tanzania katika sekta kama zile za uchimbaji wa dhahabu, mafuta na gesi, hata katika mwaka 1982, ilikuwa ni kiasi cha asilimia 40 hadi kupindukia asilimia kadha (Babu, [1982b] 2002).
Hivi sasa nguvukazi ya Tanzania inauzwa kwa rasilmali ya kimataifa kwa namna mpya ya unyonyaji mbaya zaidi kwa njia ya kuanzishwa kwa maeneo mahasusi ya kiuchumi na maeneo ya kutengeneza bidhaa za kusafirisha nchi za nje. Katika maeneo haya ambayo mara nyingi huchukua ardhi nzuri sana yenye rutuba ya kilimo, mishahara ni midogo, kuna kanuni chache za afya na usalama, vyama vya wafanyakazi na sheria zote za kazi zimepigwa marufuku, na ikiwa uzoefu wa katika sehemu nyengine za dunia ni kitu cha kuweza kujifunza – basi wafanyakazi mara nyingi, wengi wakiwa wanawake – wanakabiliwa na unyanyaswaji na udhalilishaji wa kijinsia wa mara kwa mara. Simu za upepo za Marekani (zilizofichuliwa na WikiLeaks) zinafurahia ukweli kuwa nchini Tanzania uwekezaji wa kigeni wa moja kwa moja katika maeneo yenye ‘ardhi nzuri’ unaruhusiwa kupitia sheria za Maeneo Mahasusi ya Kiuchumi (Ubalozi wa Marekani, 2008b). Hii ina maana kuwa, mashirika ya kimataifa yataweza kuingia Tanzania ili kujenga viwanda vipya na /au ghala wakati wakipata ruzuku, msamaha wa kodi na vivutio vingine vya kiuchumi
Zaidi ya hayo, makampuni haya yanahamishia faida katika benki za nje zenye (off shore) kutoza kodi ndogo na zisizofungamanishwa na sheria za nchi jambo linalosababisha serikali kupoteza sehemu kubwa ya mapato. Mwaka 2009/10 fedha zilizohamishwa zinakisiwa kuwa shilingi 695 bilioni sawa na bajeti yote ya sekta ya afya kwa kipindi hicho (Mutarubukwa, 2011).
Ufisadi umekithiri (na umekuwepo kwa muda wa miongo miwili iliyopita) na wote, mapebari wa nchi za nje na wanasiasa na wafanyabiashara wa Tanzania wamekuwa wakishiriki katika ufisadi huo kwa shauku kubwa. Hili si suala la uasilia wa jamii za Kiafrika tu kama vile baadhi ya wakati inavyodaiwa, bali lipo pia Marekani na Uingereza. Nchini Tanzania kama ilivyo katika nchi nyengine, ni miundo ya kifedha iliyoanzishwa na rasilimali za kimataifa ndiyo iliyozaa na kushajiisha ufisadi.
Katika kipindi cha mwongo wa kwanza wa miaka ya 2000 kinyang’anyiro kipya cha kugombania rasilimali za Afrika kilianza na Tanzania ilikabidhi kwa nchi za kigeni ardhi na maeneo ya bahari yenye utajiri wa mafuta na gesi, dhahabu, almasi na madini mengine kwa malipo ya ujira mdogo, na utozaji kodi hafifu huku ukiwepo uhamishaji mkubwa wa faida kwenda nchi za nje.
Kama ulivyobainisha Ubalozi wa Marekani katika kukubaliana na hayo, kwenye simu ya upepo kwa waziri wa mambo ya nje na ofisi zao nyengine za ubalozi za Afrika ya Mashariki:
Kituo cha Uwekezaji cha Tanzania kilichoanzishwa kwa mujibu wa Sheria ya Uwekezaji ya Tanzania ya 1997 ni kituo muhimu kwa habari zote zinazohitajiwa na wawekezaji na kurahisisha mambo yanayohusiana na masuala ya kuanzishwa kwa miradi… Kampuni zenye vyeti vya kustahiki vivutio vya kituo hicho zinaruhusiwa umiliki wa kigeni wa asilimia 100, msamaha wa kodi na ushuru wa kuingiza bidhaa ndani ya nchi na kuhamisha asilimia 100 ya faida, gawio na rasilimali baada ya kulipiwa kodi na malipo mengine. Vivutio kama hivyo vinatolewa pia kwa wawekezaji Zanzibar kwa kupitia Shirika la Kuendeleza Uwekezaji la Zanzibar. (Ubalozi wa Marekani, 2009c)
Kwa mujibu wa makisio ya serikali, Tanzania ina hekta milioni 44 za ardhi yenye rutuba. Takriban asilimia kumi ya ardhi hiyo imetakiwa na wawekezaji kutoka Uingereza, Ujerumani, Sweden, Uholanzi na Marekani ili kupanda mibono, malighafi ya nishati asilia. Kama alivyoeleza Dk. Felician Kilahama, mkuu wa Ufugaji Nyuki na Misitu wa Tanzania. ‘Mibono itainufaisha vipi Tanzania? Tabaan, kusema kweli, hatuna majibu, tunahitaji chakula kwanza, siyo mibono’ (Mutch, 2010).
Makampuni ya kutoka India yanakodi ardhi kwa mikataba ya muda wa miaka 50 na pengine hadi miaka 99 kwa bei ya kutupa, ili kupanda chakula cha nafaka kwa soko la India na la dunia.
Misaada na Hali ya Utegemezi
Kwa ajili ya sera zake za kupendelea nchi za magharibi, Tanzania imekuwa kwa muda mrefu kipenzi cha wafadhili wa nchi na mashirika mbalimbali (ukiachilia mbali kushuka kwa muda mfupi ‘kwa imani ya wafadhili’ katika kipindi cha katikati ya miaka ya 1980). Kama alivyoripoti balozi mdogo wa Marekani Michael Owen:
Nchi za Skendinevia, zina mpango wao wa msaada wa maendeleo ulio mkubwa hapa kuliko yote duniani; na Uingereza, Uholanzi, Ujerumani na Japan, nao pia wana mipango yao mikubwa sana. Canada sasa inajiandaa kuifanya Tanzania kuwa moja ya mpokeaji mkubwa wa misaada yake. [ Hata hivyo, msaada huu umesababisha] hali ya ‘utegemezi kwa wafadhili’. (Ubalozi wa Marekani, 2005b).
Je! Misaada inazaa chochote zaidi ya kuifanya nchi kuwa tegemezi? Kama alivyoandika Babu mwaka 1994:
Mahitaji ya misaada yamekuwa ni kiambatisho muhimu katika mahusiano yetu ya kibiashara na nchi zenye uchumi ulioendelea; tunafanya nao biashara, tunakula hasara, tunawaomba misaada, na misaada zaidi. Misaada inawaharibu wote, wanaotoa na wanaopokea. Katika matukio mengi, hasa matukio ya mashirika ya kujitolea, msaada hutolewa kwa nia njema ili kufanya mema na kujisikia vyema. Hata hivyo, mfadhili anayetoa msaada haelewi kuwa kiwango chake cha juu cha hali ya maisha kinadumishwa kutokana na unyonywaji wa nchi zinazopokea misaada ambazo bidhaa zake rahisi zinazosafirishwa kwenye nchi zinazoendelea zinatokana na kazi zenye ujira uliojikita katika mfumo wa kitumwa. Natuchukue mfano mmoja ulio wazi, Bob Geldof, mwanamuziki wa Kiingereza alihuzunishwa sana na njaa ya Uhabeshi ya 1984 kiasi kwamba alianzisha kampeni kubwa ya hisani dunia nzima ambayo iliwezesha kukusanywa Dola za Kimarekani milioni 400. Bila shaka ilikuwa ni kampeni ya ukarimu, lakini kiasi hicho kilichoweza kukusanywa kilikuwa ni sawa na mahamisho ya siku mbili ya mali kutoka Afrika kwenda Ulaya na Amerika … kwa kujua au bila ya kujua, kusema kweli, misaada husaidia katika kuufanya wizi huu mkubwa ukubalike. (Babu [1994] 2002)
Maria Baaz ameonyesha kuwa misaada si kama inawafanya wanaotoa misaada ‘wajisikie vizuri’ tu lakini inawawezesha vile vile kuwalaumu raia wa kawaida wa nchi inayopokea misaada. Wafanyakazi au wakulima ambao nguvukazi yao inanyonywa kwa kiasi kikubwa sana ili kuufanya uchumi wa nchi zilizoendelea kubariki zaidi, mara kwa mara huelezwa katika mihadhara juu ya maendeleo kuwa ni watu tuli na wakati huo huo, na kwa namna ya utata, wenye njama na wizi (Baaz, 2005: 134-47). Benjamin Mkapa ameukubali na kuufanya mtazamo huo kuwa ni wake, kama alivyobainisha Michel Owen: ‘Rais Mkapa … mara kadha amewasihi Watanzania “tusimame kwa miguu yetu wenyewe.” Na “tusitarajie sadaka milele” (Ubalozi wa Marekani, 2005b).
‘Kito Kwenye Taji la Tanzania’
Juu ya mabilioni yanayotengenezwa na mashirika yanayochimba migodi kutokana na dhahabu ya Tanzania, kwa nchi za Magharibi, na hasa Marekani, hivi sasa dhahabu siyo rasilimali yenye thamani kubwa sana kuliko rasilimali nyengine zote nchini Tanzania. Sasa ni mafuta na gesi. Nchini Libya, wakati wakipeperusha bendera ya Nyota na Milia katika Tripoli “iliyokombolewa” … Balozi wa Marekani Gene Cretz aliropoka: “Tunajua kuwa mafuta ni kito kwenye taji la rasilimali za Libya” (Pilger, 2001). Tanzania, karibu nayo itahesabiwa kuwa na kito kama hicho kwenye taji lake.
Mapema mwaka 2012, Mustafa Mukulo, wakati huo akiwa waziri wa fedha (ambaye ameondolewa kutokana na minong’ono ya kuwepo kwa ufisadi), aliviambia vyombo vya habari kuwa kuvumbuliwa hivi karibu kwa gesi asilia nchini Tanzania, kunaifanya nchi iwe imepangika katika ‘uchumi wa gesi’, huku ikithibitishwa kuwepo kwa futi za ujazo trilioni 28 za gesi na kuwepo matumaini kuwa kiwango hiki kinaweza kuzidi na hadi kufikia hata futi za ujazo trilioni 60. Kwa muda sasa, Tanzania imekuwa ikizalisha kiwango kidogo cha gesi kutoka katika kisiwa cha Songo Songo kwa ajili ya matumizi ya ndani ya nchi, lakini gesi hii mpya iliyovumbuliwa, nyingi ikiwa nchi kavu ni ya kiwango kikubwa. Hivi sasa, takriban makapuni makubwa yote ya gesi na mafuta – Shell, BP, AGIP, Antrim, Amoco,Texaco, Ophir, British Gas, Tullow, Artumas, Maurel & Prom, Statoil na makampuni ya India Reliance na Essar – yanafanya shughuli zake au yanafanya majadiliano nchini Tanzania, na nchi inaweza ikapata Uwekezaji wa Moja kwa moja kutoka Nchi za Kigeni (FDI) utakaozidi kiasi cha Dola za Kimarekani bilioni 22 kwa mwaka. Kampuni ya kimataifa ya gesi ya Uingereza, British Gas International imeshatangaza mpango wake wa kuwekeza utakaozidi Dola za Kimarekani bilioni 10 katika nusu ya pili ya mwongo huu. (Ratio Magazine, 2012).
Miongoni mwa nchi nyengine, Norway, kwa muda sasa, imekuwa ikiutazama kwa macho mawili uwezekano wa kupatikana mafuta Tanzania na hasa Zanzibar (Chachage, 2009), na kampuni ya Norway ya Statoil hivi sasa ni mshindani mkubwa katika kinyang’anyiro kipya cha kugombania Afrika. ‘Kwetu, hivi sasa Afrika Mashariki ni moto’, alitamka Tim Dodson, Makamo wa Rais Mtendaji wake anayehusika na utafutaji wa mafuta (Williams, 2012).
Hivi sasa, serikali ya Tanzania inajenga miundombinu kwa ajili ya uchimbaji wa mafuta pamoja na kuandaa mfumo wa kisheria; sheria mpya ya (Utafutaji na Uzalishaji) wa mafuta, na Mpango Mkuu wa Gesi Asilia, ikiwa ni pamoja na kuandaa na kupitishwa Mswada wa Kusimamia Mapato ya Gesi/na Mafuta utakaokuwa pamoja na utaratibu wa utozaji kodi na namna yatakavyoshughulikiwa mapato ya gesi. Masharti hasa ya mikataba bado yanasubiriwa. Je! Mikataba hii itakuwa na maana kuwa makampuni ya mafuta yatatoa pesa kwanza kwa Tanzania na badaye kunyonya sehemu kubwa ya faida? Hivi ndivyo ilivyokuwa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Kwa mfano watakuwa tayari kulipa gharama za uharibifu utakaosababishwa na uvujaji wa mafuta? Au watalipa kiasi kidogo tu huku hasara zikifumbiwa macho. Platform London, kwenye utafiti wake wa mikataba ya mafuta, migogoro, uharibifu wa mazingira na umasikini katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, umelielezea hilo kuwa, ‘Serikali wenyeji mara nyingi huvutiwa na malipo ya kutia saini kwa kuwa huwa ni ya fedha taslim mwanzo. Mijadala mingi juu ya mikataba inatilia maanani zaidi malipo ya aina hii badala ya kuangalia masharti yaliyo muhimu zaidi’ (Platform, 2010: 9).
Wakati visima vya gesi asilia hiyo vimegundulikana nchi kavu na baharini upande wa Tanzania Bara, huko Zanzibar mafuta yamegundulikwa hasa kule kunakoitwa Vitalu vya Bahari Kuu na. 9, 10, 11 na 12 ambavyo vinaizunguka Pemba na Unguja. Kiwango na aina ya mafuta haya haijulikani lakini hatua za utafutaji wa kutosha na uchimbaji vimecheleweshwa kwasababu ya mgogoro kati ya Zanzibar na Tanzania bara.
Kwa mujibu wa simu ya upepo iliyotumwa na balozi mdogo wa Marekani Tulinabo Mushingi kwa waziri wa mambo ya nje na Wizara za Nishati na Biashara mjini Washington:
Baadhi ya wawakilishi wa kampuni ndogo za mafuta hapa nchini, kama vile Paddy Hoon ya Heritage Oil, 2 wanazungumzia uwezekano wa kupatikana kiasi kikubwa cha mafuta. Akilinganisha kiasi cha mafuta ya nchi kavu ya Tanzania na yale ya Nigeria, Hoon amejaribu kuwashawishi wote wale ambao wanaotaka kumsikiliza kuwa mafanikio makubwa yapo karibu. Lakini Halfani wa [Shirika la Maendeleo ya Petroli la Tanzania] anaamini kuwa hakuna mafuta karibu na visiwani. (Ubalozi wa Marekani, 2009i)
Hata hivyo, Mushingi aliendelea:
Ijapokuwa hakuna maendeleo kuhusiana na utafutaji wa mafuta, na uwezekano mkubwa kuwa utafutaji hautagundua vitalu vitavyokuwa na manufaa ya kiuchumi, uwezekano wa kupatikana mafuta umekuwa upo katikati ya mjadala wa kisiasa kati ya Zanzibar na Bara. Wazanzibari wengi wanajihisi kuwa wao ni Taifa huru lililoungana kwa hiari na Bara na kuunda Muungano wa Tanzania. Suala la kuwa na udhibiti kamili wa rasilimali zozote zitakazoingiza kipato kikubwa ni suala nyeti kwa wanasiasa wote wa Kizanzibari. Katika kikao cha mwezi April 2009 cha baraza pekee la Zanzibar, Baraza la Wawakilishi, wajumbe kutoka vyama vyote, kwa kauli moja walipitisha azimio lililowasilishwa na chama tawala cha CCM – Zanzibar, likieleza kuwa sheria za kuanzishwa kwa Shirika la Maendeleo ya Petroli la Tanzania na shughuli za utafutaji wa mafuta nchini havikuridhiwa na Bunge la Zanzibar. Kwa hivyo, kwa mujibu wa mkataba wa Muungano, shughuli za shirika hilo hazitambuliwi Zanzibar. Azimio hilo lilitilia mkazo maoni kuwa mkataba wa mwaka 1968 juu ya mgawanyo wa mapato kati ya Zanzibar na serikali ya Muungano hauhusiani na nishati na kutilia mkazo kuwa gawio la Zanzibar kutoka Bara ni dogo. Azimio hilo lilipendekeza kuwa Zanzibar iunde shirika lake lenyewe litakalolingana na Shirika la Maendeleo ya Petroli la Tanzania na kuwa utafutaji wowote ule katika Maeneo ya Kiuchumi Yaliyotengwa ufanyike kwa pamoja. Uratibu wake utakabidhiwa kwa kamati ya taifa iliyo chini ya ofisi ya Makamo wa Rais inayoshughulikia masuala ya Muungano, lakini azimio hilo limesisitiza kuwa nishati, mafuta na gesi kama yalivyokuwepo Zanzibar na katika bahari yake si mambo ya Muungano. Inavyoonekana kuwa Shell haiwezi kutafuta mafuta katika vitalu ilivyokabidhiwa mwaka 2002 kwasababu ya mvutano huo.
Kuna dalili kuwa mambo huenda yakabadilika huku Shell ikiwa imepewa ruhusa kuchimba mafuta katika vitalu ilivyokabidhiwa vilivyoizunguka Zanzibar.
Bila ya kuangalia ubora na kiwango cha mafuta ya Zanzibar na vipi mapato kutokana na mafuta hayo yatagawanywa, kilichotokeza Tanzania (pia Uganda na Kenya vile vile) kimeibadilisha kwa kiwango cha juu hadhi na nafasi ya Zanzibar katika mukhtadha wa ubeberu wa Kimarekani, kama tutakavyoona katika sura ifuatayo. Ikiwa ni sehemu ya kanda ya Afrika ya Mashariki yenye utajiri wa mafuta na gesi, inayoambaa kutoka Msumbiji hadi Somalia, itavutiwa karibu zaidi na mitandao ya kijendawazimu ya Marekani inayofuatilia na kukusanya habari za kijasusi na kuwaona raia wa kawaida kuwa ni watu wanaoweza kuwa magaidi.
Wananchi wa vijijini Bara, kule ambako gesi imepatikana, hata wale wasiokuwa Waislamu, wanaweza kuyahisi hayo. Hawana matarajio mema juu ya kunufaika kwao na mafuta na gesi ya nchi yao. Kama taarifa ya Thembi Mutch ilivyoeleza kutoka katika kijiji kimoja miongoni mwa vingine vingi vyenye uzoefu kama huo:
Katika kijiji kidogo cha Mikindani, pwanipwani mwa kusini-mashariki ya Tanzania, barabara zilizogharamiwa na Benki ya Dunia zipo karibu na matumbawe yaliyovurugika kwasababu ya uvuvi wa kutumia baruti na miundombinu mibovu ya maji taka. John, mwenye umri wa miaka 15 anaonyesha kidole kwenye meli nne zilizopo mbali. ‘Zote zile zipo hapa kwasababu ya mafuta na gesi’, alisema. ‘Wakati mwengine Wazungu wanakuja kwa helikopta. Hawaruhusiwi kukutana na sisi; kuna ukanda wa utenganisho wa maili kumi unaozunguka eneo lao pindipo kama watatekwa nyara. (Mutch, 2012)
Wazee wa kijiji wa Mikindani wanaelewa kuwa kiwango cha juu cha ukosefu wa ajira katika mkoa huo (ni asilimia 8 – 10 tu ya wananchi ndio wenye ajira) hakina dalili za kuweza kuboreshwa kwa kuwa uchimbaji wa mafuta hautazalisha kazi nyingi kwa wenyeji.
Hofu ya Marekani kwa China
Wakati wa kipindi cha vita baridi nchini Zanzibar na baadae Tanzania Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilikuwa ikisumbuliwa na hofu ya wakomunisti wa China, ‘Chikoms’, hivi sasa ugaidi wa Kiisilamu umechukua nafasi ya ukomunisti na kuwa ni zimwi kwa Marekani. Juu ya hilo, wasiwasi wa Marekani kuhusu China na uhusiano wa China na nchi za Afrika bado haukuondoka. Hivi sasa, mahubiri ya Marekani kuhusu China katika nchi za Afrika, yakielezwa ama kwa simu za upepo za siri kwenda na kutoka Wizara ya Mambo ya Nje au katika makala yanayoandikwa katika majarida na wasomi wa Kimarekani, yanaonyesha hofu inayozidi kukua kwa kuimarika kwa nguvu za kiuchumi za China na kuongezeka kwa biashara kati yake na nchi za Afrika.
Katika mwongo wa kwanza wa karne hii, China ilizidisha biashara yake na Tanzania. Jumla ya biashara yote kati ya China na Afrika kwa pamoja, ni Dola za Kimarekani bilioni 166.3 mwaka 2011, ukilinganisha na Dola za Kimarekani bilioni 10 mwaka 2000 (Liu Guangyuan, 2012). Kwa kubadilishana na bidhaa zinazozalishwa na viwanda vidogo vidogo, ambazo watu wengi wanasema kuwa ni za viwango duni vya chini, China kwa shauku kubwa, imekuwa ikichukua malighafi na ili kulirahisisha jukumu lake hili la kiuchumi imekuwa ikijenga na kuendeleza miundombinu – madaraja, barabara, na reli. China inaipatia Tanzania mkopo wa Dola za Kimarekani bilioni 1.2 kujenga bomba la kusafirishia gesi asilia lenye urefu wa kilomita 230 ili kuviunganisha vitalu vyake vya gesi viliopo Mtwara na Dar es Salaam.
Kinyume yake, mikakati ya Marekani katika Afrika imo katika kutafuta njia ya kujenga udhibiti mpya na kamili wa kiuchumi na kijeshi katika sehemu kubwa ya bara hili. Kwa hivyo, wakati magazeti ya Tanzania yanaandika habari za askari jeshi wa Kimarekani wakifungua skuli na kutoa misaada ya kibinadamu, nyuma ya mgongo wa tabasamu na ahadi za misaada, askari jeshi hawa ni ishara ya, kama zinavyoonyesha nyaraka za WikiLeaks, sura ya parapaganda ya kikosi kipya katili cha uvamizi, ambacho madhumuni yake makubwa ni kurahisisha uporaji wa malighafi kwa Marekani na makampuni ya kimataifa ya Ulaya.
Kati ya mwaka 1998 na 2001 na 2002-05 peke yake, Marekani iliongeza marudufu gharama za matumizi yake ya kijeshi katika Afrika kutoka Dola za Kimarekani milioni 296 hadi Dola za Kimarekani milioni 597 (Yi-chong, 2006). Mwaka 2002 waraka wa serikali uliochapishwa na Kundi la Kuandaa Sera ya Mafuta Afrika (AOPIG) – kundi la ushawishi la Washington lililoanzishwa na jumuiya ya washauri mabingwa wa Kiyahudi, Taasisi ya Taaluma ya Juu ya Mikakati na Kisiasa – ilipendekeza mtazamo ‘mpya wenye nguvu zaidi juu ya ushirikiano wa kijeshi wa Marekani katika Afrika, Kusini mwa Jangwa la Sahara, ambao utakuwa ni pamoja na kuundwa kwa kikosi cha pamoja ambacho kitawezesha upatikanaji wa manufaa makubwa sana katika ulinzi wa rasilimali zilizowekezwa za Marekani [wakati huo huo] … kukabiliana na kuangamiza ugaidi wa kimataifa na wa kikanda’ (Glazebrook, 2013; AOPIG, 2002). Mwezi Disemba 2006 kikosi cha muundo kama huo kiliidhinishwa na serikali ya Marekani. Kiliitwa Kikosi cha Pamoja cha Marekani na Afrika (AFRICOM). Rais Bush alitangaza kuwa kikosi hicho kingelikuwa na Makao Makuu yake Afrika. Hata hivyo, mwaka 2008 uamuzi huo ulikataliwa katakata na Umoja wa Afrika. Katika hali ya kugeuka nyuma kwa kudhalilishwa kwa Bush, makao makuu ya kikosi hicho yaliwekwa Stuttgart, Ujerumani (Glazebrook, 2013).
Moja ya malengo ya kimkakati ya Kikosi hicho cha Pamoja cha Marekani na Afrika lilikuwa ni kukabiliana na ushawishi unaozidi kukua wa Uchina katika bara hili. Utafiti mmoja wa kikosi hiki ulidai, kwa kiwewe cha namna ya siku za vita baridi kuwa, ‘Watabiri wa kihistoria wanatabiri kuwa kukosekana uaminifu na kutokuwa na uhakika kutalileta Jeshi la Ukombozi la Wananchi barani Afrika kwa idadi kubwa ya namna ya kushangaza. (Holslag, 2009 23). Ikiwa hili litatokea au la, hilo ni jambo la kusubiri. Bunge la Marekani linaonekana kugawanyika juu ya namna ya kuzishughulikia harakati za Uchina katika Afrika, na mkakati mpya wa ulinzi wa Rais Obama unaeleza kuwa Bahari ya Pacifik itakuwa ni medani mpya ya mvutano wa kijeshi na uwezekano wa mapambano (Wizara ya Ulinzi ya Marekani, 2012). Hata hivyo, sera ya Marekani ya vita na uporaji Barani Afrika haina dalili ya kuweza kubadilika katika siku za karibu. Kama alivyoandika John Pilger, Marekani inapeleka vikosi vya jeshi lake katika nchi 35 za Afrika, ikianza na Libya, Sudan, Algeria, na Niger – kitu kipya ambacho ingawa ‘kimeripotiwa na Associated Press siku ya Krismasi … hakikukaririwa katika vyombo vya habari vingi vya Uingereza na Marekani’ (Pilger, 2013).
Hofu ya Marekani kwa Iran
Katika matamko mengi yanayoweza kukumbukwa ya Dwight Eisenhower, mawili yanahusiana sana na hali ya hivi sasa. La kwanza ni yale aliyoyaandika katika kitabu cha kumbukumbu mwaka 1951 kabla hakuwa rais: ‘Mungu ndiye ajuae tutafanya nini bila ya mafuta ya Iran’; na tamko la pili alilitoa miaka miwili baadae katika mkutano wa Baraza la Usalama la Taifa tarehe 4 Machi, 1953, aliposema kuwa ni suala linalofadhaisha sana kuwa ‘tunaonekana kushindwa kuzifanya baadhi ya hizi nchi dhaifu kutupenda badala ya kutuchukia’ (Robarge, 2008). Miezi michache baadae Shirika la Ujasusi la Marekani liliandaa makupuzi ya serikali ambayo yalimpindua waziri mkuu wa Iran, mwananchi aliyechaguliwa na aliyekuwa akipendwa sana, Mohammad Mossadeq, ambaye aliyataifisha mafuta ya Iran, na badala yake waliiweka madarakani serikali kandamizi ya vibaraka iliyoongozwa na Shah Mohammad – Reza Pahlavi.
Hivi sasa, ijapokuwa Iran ina serikali iliyo tofauti kabisa na ile ya Mossadeq, wasiwasi wa Marekani ni ule ule. Wanadiplomasia wa Kimarekani katika ‘nchi dhaifu’ za dunia nzima wameshughulika wakijaribu kuizuia Iran isianzishe mahusiano ya kirafiki na nchi hizo, wakati Shirika la Ujasusi la Marekani, kwa mujibu wa maelezo ya wanasiasa wa Iran, limeshughulika huko Iran (Dehghan, 2011).
Kuhusu Tanzania, katika kipindi cha miaka michache iliyopita Marekani imekuwa na wasiwasi na mambo mawili. La kwanza ni hofu ya Mashia ‘wenye siasa kali’ kuwa na ushawishi kwa Waisilamu wa nchi hiyo na la pili ni wasiwasi wake kuhusu msimamo wa Tanzania kuhusiana na tuhuma za mpango wa Iran wa silaha za nyuklia. Katika juhudi zao za kuifanya Tanzania iambatane na msimamo wa Marekani katika Umoja wa Mataifa, tumewaona wanadiplomasia wa Kimarekani wakibembeleza na hata kutoa vitisho chini kwa chini wakati wanasiasa wa Tanzania wakikubali au kujaribu kutoa maelezo kuhusu msimamo wao bila ya kushambulia.
Kwa mfano, mwezi Januari 2006, Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam ulituma simu ya upepo Washington ikieleza kuwa Balozi Liberata Mulamula, mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa Mambo Mbalimbali cha Wizara ya Mambo ya Nje ya Tanzania anaamini kuwa:
Mazungumzo juu ya kulipeleka suala la Iran kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa yanahitaji kusubiri mpaka hapo Shirika la Kimataifa la Nguvu za Nyuklia (IAEA) litakapokutana na kutoa mapendekezo yake rasmi. Kwa kuwa Iran imetia saini Mkataba wa Kutosambaza Silaha za Nyuklia (NPT) … Hatua za kuwahi na kukiuka makubaliono ya mkataba huo zinaweza kuikasirisha Iran na kusababisha kujitoa kutoka kwenye mkataba huo, kama ilivyofanya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea mwaka 2003. (Ubalozi wa Marekani, 2006a)
Simu hiyo imezidi kueleza kuwa Mulamula alisema waziwazi kuwa, hafurahishwi na mtazamo wa kibabe wa Marekani kuwa Serikali ya Tanzania ambayo hivi sasa ni mwenyekiti wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ielezwe juu ya maendeleo kuhusiana na mtazamo wa Marekani pamoja na hatua nyengine tunazodhamiria kuchukua. “Msishangae, tafadhali twambieni mnapanga kufanya nini.”
Simu nyengine iliyopelekwa Washington miaka michache baadae, mwezi Disemba 2007 ilimbaini naibu wa ubalozi Purnell Delly akimkemea naibu waziri wa mambo ya nje wa Tanzania Seif Ali Idi kuwa ‘ikiwa masuala ya nyuklia hayakujadiliwa wakati wa ziara ya hivi karibuni ya [ Makamu wa Rais Shein] huko Teheran basi ilibidi iwe hivyo’, pamoja na kutaka litolewe tamko la hadharani ‘kuitaka Iran kuacha mpango wake wa kutengeneza silaha za nyuklia na kushirikiana kikamilifu na Shirika la Kimataifa la Nguvu za Nyuklia’. Idi alijibu kuwa Tanzania imesisitiza kwa serikali ya Iran kuwa ‘wajisafishe’ na vile vile kuwa Tanzania imekuwa na mazungumzo juu ya msamaha wa deni na serikali ya Iran (Ubalozi wa Marekani, 2007b). Tanzania bado ina deni lisilolipwa kwa Iran ambayo inahitaji kutoa msamaha wa deni (Munte, 2012).
Simu za siri kutoka kwa wanadiplomasia wa Marekani walio Dar es Salaam juu ya suala la Iran zinadhihirisha imani yao kwa Rais wa hivi sasa wa Tanzania Jakaya Kikwete. Kwa mfano mwezi Januari 2009 balozi mdogo Larry Andre’ alieleza hofu yake juu ya ziara ya waziri wa ulinzi Hussein Ali Mwinyi huko Teheran na kutia saini kwake mkataba wa maelewano kuhusiana na kubadilishana uzoefu wa mambo ya kijeshi na ya ulinzi. Alieleza vile vile kuwa, kwa mujibu wa waziri wa mambo ya ndani Lawrence Masha, mkataba huo wa maelewano si kama ‘hauonyeshi mabadiliko katika uhusiano wa Tanzania na Iran tu au upatikanaji wa silaha na vifaa vya kijeshi’, mabadiliko kama hayo ya kisera ‘yangelihitaji kibali cha chombo cha mamlaka mbalimbali ambacho mwenyekiti wake ni Rais Kikwete’ (Ubalozi wa Marekani, 2009). Jakaya Kikwete, kama tutakavyoona, ni mtu wa Wamarekani, ambaye labda yupo tayari zaidi kutekeleza maagizo yao kuliko rais yeyote yule katika waliomtangulia.
0 Comments