Mwishoni mwa miaka ya 1950 na mwanzoni mwa miaka ya 1960, kulikuwa na harakati za aina mbalimbali za nchi za Afrika kutaka kujikomboa, kuutokomeza ukoloni na tawala za kibaguzi hasa Kusini mwa Afrika.
Wakoloni hasa Waingereza, Wafaransa, Wajerumani, Wareno na Wabelgiji wamekuwa wakizitawala karibu nchi zote za Afrika na mku-tano wa Berlin, Ujerumani wa mwaka 1884 hadi 1885 ndio ulipiga muhuri wa wakoloni hao kugawana Afrika na kujua kila mmoja atashika wapi. Ilikuwa ni kama vile mnyama mkub-wa na aliyenona, Afrika, amewindwa na kupatikana na hivyo wawindaji hao wanagawana nani anachukua paja, nani mguu, nani kifua, nani mkono na kadhalika.
Isitoshe, Afrika Kusini na Zimbabwe zikawa zimeshikiliwa na tawala za watu wachache za kiba-guzi. Afrika Kusini ikiwa na makaburu waliowanyima haki zote Waafrika walio wengi katika nchi yao wenyewe. Zimbabwe nako kulikuwa na utawala wa Wazungu wachache, uliowakan-damiza Waafrika wengi.
Wanahistoria wanatuambia kuwa wakoloni na wabaguzi hao hawakuja kama ajali, bali walikuwa wanatekeleza mipango ya muda mrefu ya kupanua himaya za kiuchumi. Wali-tumwa watu kutafiti na wakaingia Afrika kwa namna mbalimbali. Waliku-wepo walioitwa wavumbuzi, waeneza dini na ustaarabu na wafanyabiashara, ili mradi kutafiti mambo gani yapo Afrika, yatapatikanaje, vipi, lini na kwa namna gani.
Taarifa za makundi ya watu hawa zilipelekwa makwao na ndizo zilizo-saidia na kusababisha kutengene-zwa kwa mikakati ya namna gani ya kuishinda na kuitawala Afrika. Historia pia inatueleza hara-kati mbalimbali za mababu zetu za kupinga, siyo ujio wa wageni au ushirikiano wa kibiashara na kupeana maarifa na uzoefu, bali kutawaliwa kwa nguvu. Mapambano mbalimbali yalitokea sehemu mbalimbali za Afrika, lakini maguvu ya wavamizi hawa yakata-malaki na hivyo wakaweza kuitawala Afrika, kupora rasilimali zake kwa ajili ya matumizi ya watu wao huko kwao.
Mwalimu Nyerere alipata kusema kuwa utajiri walionao Wazungu una uhusiano mkubwa na umaskini ulio-kithiri wa Waafrika. Haya yote tuli-fundishwa katika historia, kuan-zia katika shule za msingi na baadaye sekondari hadi vyuoni. Ila hapa ni kukumbushana tu.
Madhila ya ukoloni, ndiyo yaliyosababisha Waafrika kutafuta njia ya kujinasua na janga hili. Viongozi wa Afrika, kuanzia Mfalme Haile Sellasie wa Ethiopia, Patrice Lumumba wa Congo, Kwame Nkurumah wa Ghana, Julius Nyerere wa Tanzania, Jomo Kenyatta wa Kenya na Nelson Mandela wa Afrika Kusini kwa kuwataja wachache kila mmoja kwa namna yake, na wakati mwingine kwa umoja wao na kushirikiana, walitengeneza mipango wa kulikomboa bara hili.
Harakati hizo zilifanikiwa na katika miaka ya 1960 nchi kadhaa za Afrika zilikombolewa na sasa nchi zote 54 za Afrika ziko huru. Ya hivi karibuni ni Sudan Kusini mwaka 2011, lakini kabla ya hapo ilikuwa ni Afrika Kusini mwaka 1994.
Je, harakati hizo zilifanywa vipi na kina nani waliunga mkono mapambano hayo na hivyo kusaidia juhudi zake, hasa kutoka nje ya Afrika?
Kipindi cha harakati za ukombozi wa Afrika kilikuwa kipindi kinachoitwa cha “Vita Baridi” au “Vita vya Maneno” (Cold War). Yaani mashindano ya mataifa makubwa kupingana bila ya kupigana kati ya Magharibi yaliyoongozwa na Marekani na yale ya Mashariki yanayofuata siasa za kisoshalisti yaliyoongozwa na Urusi.
Hicho ni kipindi kilichokuja baada ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia ya mwaka 1939 mpaka 1945. Vita hiyo, kama ile Kuu ya Kwanza ya mwaka 1914 hadi 1918, ilihusisha wakoloni hao hao kutaka kujipanua zaidi.
Kutokana na Vita Baridi hiyo, Urusi, ambayo ilishinda Vita ya Pili ya Dunia kwa kuyafurusha majeshi ya Ujerumani ya Hitler hadi Berlin, ilipoamua kusaidia katika mapambano ya ukombozi wa Kusini mwa Afrika ilionekana na mataifa ya Magharibi ambayo miongoni mwao ndio wakoloni hao wakubwa, kuwa ilikuwa na njama za kutaka kueneza ukomunisti duniani au labda baadaye “kupora” rasilimali na maliasili za Afrika.
Lakini, baada ya ushindi mkubwa wa mafanikio katika ukombozi wa Kusini mwa Afrika matokeo ni kinyume na dhana za nchi za Magharibi. Nchi huru za Kiafrika siyo za kikomunisti na wala siyo Warusi, zaidi ya hao wakoloni wa zamani wanaofaidi rasilimali na maliasili za Afrika hivi sasa, kwa mtindo mwingine ambao siyo tena ukoloni, ila ukoloni mamboleo kupitia unyonyaji wa biashara isiyo ya haki.
Mandela alivyopinga dhana hii
Dhana hii ya nchi za Magharibi kuwa harakati za ukombozi wa Kusini mwa Afrika ni kueneza ukomunisti ilipingwa vikali Afrika na hata kwingineko duniani. Kwa mfano, Mandela aliielezea kwa ufasaha katika utetezi wake kwenye kesi ya Rivonia.
Mandela alieleza hayo alipofikishwa mahakamani jijini Pretoria baada ya kukamatwa na kushtakiwa na utawala wa makaburu wa Afrika Kusini kwa kula njama za kuuhujumu na kuupindua utawala huo, kwa kushirikiana na jeshi la chama chake cha ANC (African National Congress), lililojulikana kama Umkhonto we Sizwe (Mkuki wa Taifa).
Shauri la akina Mandela liliitwa kesi ya Rivonia ikiwakilisha jina la kitongoji cha Rivonia jijini Johannesburg kilichokuwa na eneo lililotumika kuwa maficho ya viongozi wa ANC iliyokuwa imepigwa marufuku nchini Afrika Kusini.
“Kwa kuanzia,” Mandela alisema katika maelezo yake ya saa tatu mahakamani mbele ya majaji wa kikaburu, “nataka kusema wazi kuwa mawazo yaliyotolewa na upande wa utawala katika maelezo yao ya awali kwamba harakati za ukombozi wa Afrika Kusini zinatokana na kushinikizwa na watu wa nje au wakomunisti, siyo sahihi kabisa.
“Nimeyapanga na kuyafanya yale yoyote niliyoyafanya nikiwa mtu binafsi na kiongozi wa watu wangu kwa sababu ya uzoefu nilionao wa Afrika Kusini na Uafrika wangu ninaojivunia kwa dhati na siyo kwa sababu ya jambo lolote lile mtu wa nje ameweza kulitamka.”
Aliongeza, “wakati wa ujana wangu nikiwa katika Jimbo la Transkei, nilikuwa nawasikiliza wazee wetu wakisimulia hadithi za zamani. Miongoni mwa hadithi walizonisimulia ni zile za vita vilivyopiganwa na mababu zetu wakitetea nchi yao… nilitumaini na kushawishika wakati huo kuwa maisha nitakayoishi yatanipa fursa ya kuwatumikia watu wangu na kutoa mchango wangu kwenye harakati za ukombozi. Jambo hili ndilo lililonitia moyo kuyafanya yote niliyoyafanya kuhusiana na mashtaka ninayokabiliwa nayo katika kesi hii”.
Hivyo ni dhahiri Mandela, ambaye katika kesi hiyo Aprili 1964 yeye na wenzake walihukumiwa kifungo cha maisha na kuachiliwa huru Februari 1990 baada ya kuwa kifungoni kwa takriban miaka 27, alithibitisha harakati hizo siyo ukomunisti.
Baada ya utawala wa makaburu kusambaratika, katika uchaguzi huru wa kwanza wa Afrika Kusini isiyo ya kibaguzi, Mandela alichaguliwa kuwa Rais wa kwanza wa nchi hiyo na wala hakuendesha nchi ya kikomunisti.
Alistaafu urais baada ya miaka mitano na kufariki dunia baadaye Desemba 5, 2013 akiwa na umri wa miaka 95 na kuzikwa kwa heshima kubwa.
Ng’wanakilala aligusia ukomunisti
Kuhusu msaada wa Urusi katika ukombozi wa Kusini mwa Afrika, Nkwabi Ng’wanakilala (marehemu), aliyewahi kuwa mkurugenzi wa Shirika la Habari Tanzania (Shihata) na mkurugenzi wa Redio Tanzania, aliitaja kuwa ni moja ya nchi zilizosaidia kijeshi katika harakati za ukombozi Kusini mwa Afrika na kwamba misaada hiyo siyo kueneza ukomunisti.
Katika kitabu chake alichokiita Muhtasari wa Mapambano ya Ukombozi wa Kusini mwa Afrika, kilichochapishwa kwa Kiswahili mwaka 1982, Ng’wanakilala alisema: “Ilitegemewa kuwa kwa kuwa wapigania uhuru wa Afrika Kusini wanapigania haki kwa niaba ya binadamu wote kwa ujumla, wangepewa msaada wa silaha kiasi wanachohitaji.
“Lakini nchi zenye uwezo ni nchi zilizoendelea kama vile Uingereza, Marekani, Ujerumani ya Magharibi (wakati huo Ujerumani ikiwa nchi mbili Ujerumani Mashariki na Ujerumani Magharibi), Canada, Ufaransa…nchi hizi zina rasilimali yake huko Afrika Kusini. Mara nyingi misaada ya kijeshi inatolewa na nchi za kijamaa kama vile Urusi, China, Cuba na Ujerumani ya Mashariki.
Ng’wanakilala aliongeza, “misaada hii inapotolewa, nchi za Magharibi hupiga kelele kuwa ina lengo la kujenga Serikali za kikomunisti katika Afrika. Hakuna hata nchi moja Kusini mwa Afrika ambayo inaweza kuitwa ya kikomunisti, kama ilivyo Urusi, kwa mfano.
“Nchi nyingi zinazoitwa za kikomunisti na nchi za Magharibi, kwa hakika ni nchi zenye serikali za kijamaa na ujamaa wake unatokana na misingi ya kijamii ya Kiafrika iliyokuwepo tangu zamani”.
Ng’anakilala alimalizia katika eneo hilo la kitabu chake akisema, “suala la ukomunisti linaletwa na nchi za Magharibi ili kutetea hadhi na mali ya nchi hizo na kuleta mgawanyiko katika suala zima la ukombozi.”
Naye Vladimir Shubin wa Idara ya Mambo ya Afrika ya Taasisi ya Masuala ya Kisayansi ya Urusi aliyeshughulikia masuala ya ukombozi wa Kusini mwa Afrika, akitetea hoja hiyo katika kitabu chake kwa lugha ya Kiingereza kiitwacho Hot ‘Cold War (kwa tafsiri yangu ya Kiswahili - Vita Baridi iliyokuwa Moto), alisema misaada hiyo ya Urusi haikuwa kwa minajili ya kueneza ukomunisti.
Ni mtazamo wa Urusi wa kuunga mkono wanyonge kwenye harakati za kuleta maendeleo ya binadamu. Urusi iliunga mkono harakati za ukombozi wa Kusini mwa Afrika siyo kwa sababu ya Vita Baridi. Urusi inayachukulia mapambano haya (ya ukombozi wa Kusini mwa Afrika) kuwa ni sehemu ya harakati za dunia za kupambana na ubeberu zilizokuwa zikiendeshwa na jamii ya kisoshaliti, vyama vya ukombozi vya kitaifa na tabaka la wafanyakazi (hata) katika nchi za kibepari.
Misaada ya Urusi kwa vyama vya ukombozi vya nchi za Kusini mwa Afrika ilikuwa ni pamoja na ile ya kibinadamu na kiraia, ikiwa ni fedha, matibabu, chakula na elimu na mingine ya kijeshi ikiwamo ushauri, mafunzo na upatikanaji wa zana za kivita kadri ilivyohitajika.
Hivyo wakati tunaishangilia Afrika huru kisiasa inayoendeleza awamu nyingine ya mapambano ya ukombozi wa kiuchumi, siyo vizuri kuisahau historia ya ukombozi wa Afrika na waliosaidia katika harakati hizo, wakati ule na wakati huu.
Ndiyo maana Umoja wa Mataifa umeitangaza siku ya jana, Julai 18, kila mwaka kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela kukumbuka mchango wa mwanamapinduzi huyo katika kupigania haki za kijamii duniani na hasa ukombozi wa Afrika Kusini na Kusini mwa Afrika kwa jumla.
Siku ya Kimataifa ya Nelson Mandela ya mwaka huu imeangukia katika kutimiza miaka 100 tangu kuzaliwa kwake, Julai 18, 1918.
Saidi Nguba ni mwandishi mkongwe nchini. Aliwahi kuwa mhariri wa magazeti ya Uhuru, Mzalendo na Mwananchi. Alistaafu rasmi Agosti 2013 akiwa mwandishi wa habari wa Waziri Mkuu.