Brigedia Jenerali Hashim Mbita, bado anaendelea kuheshimika kama shujaa wa harakati za ukombozi barani Afrika. Anaheshimika sana Afrika nzima kutokana na uaminifu wake na kujitolea katika kuhakikisha
mataifa ya Afrika yaliyokuwa bado chini ya utawala wa kikoloni yanapata uhuru.
Jina la Hashim Mbita ni lenye kuheshimika ndani na nje ya mipaka ya Bara la Afrika kuanzia Msumbiji, Sao Tome na Principe, Zimbabwe, Angola na Afrika Kusini.
Maisha ya Hashim Mbita yanamgusa kila mtu anayeishi katika mataifa hayo ama awe anajua au hajui. Uaminifu na kujituma kwa Mtanzania huyu, mzaliwa wa Mkoa wa Tabora katika harakati za ukombozi barani Afrika, kuliifanya Tanzania kujivunia na hata kutembea kifua mbele kama moja wapo ya nchi zilizotoa mchango mkubwa katika ukombozi wa bara hili.
Jenerali (mstaafu) Mbita alikuwa Katibu Mtendaji, Kamati ya Ukombozi ya Umoja wa Nchi za Huru za Afrika (OAU), kwa miaka 22, kuanzia 1972 hadi 1994, pale harakati za ukombozi zilipokamilika baada ya kufanyika uchaguzi wa kidemokrasia nchini Afrika Kusini—uchaguzi uliowapa Wafrika Weusi wakiongozwa na Nelson Rolihlahla Mandela, uwezo wa kushika hatamu ya uongozi.
Alitunukiwa medali ya Seretse Khama (Sir Seretse Khama Medal) na Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC), tuzo ya Mtoto wa Africa (Son of Africa Award) kutoka Umoja wa Afrika (AU) mwaka 2014, na tuzo ya Munhumutapa, ambayo ni ya heshima ya juu ya Taifa la Zimbabwe anayoweza kupewa raia wa kigeni.
Hashim Mbita alipewa tuzo hiyo kwenye mkutano wa SADC uliofanyika kwenye Mji wa Victoria Falls nchini Zimbabwe mwaka 2014, ikiwa ni kutambua mchango wake katika mapambano ya ukombozi wa Bara la Afrika. Kwa kupewa tuzo hiyo, aliingia katika orodha ya watu sita pekee kuwahi kutunukiwa tuzo hiyo.
Ukimtoa Mbita wengine ni Rais Mwalimu Julius Nyerere (Tanzania), Rais Augustino Neto (Angola), Rais Sir Seretse Khama (Botswana), Rais Samora Machel (Mozambique) na Rais Kenneth Kaunda (Zambia). Maandishi katika tuzo ya Munhumutapa aliyotunukiwa Mbita yanasomeka hivi:
“Kwa jukumu muhimu alilotekeleza katika ukombozi wa kikanda pamoja na ushirikiano wakati wa uongozi wake wa miaka 20 kama Katibu Mtendaji wa Kamati ya Ukombozi ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) - mtangulizi wa Umoja wa Afrika (AU).”
Kamati hiyo ya Ukombozi ya Umoja wa Afrika, iliendesha shughuli zake ikitokea jijini Dar es Salaam kwa mwaliko wa Rais wa kwanza wa Tanzania, Julius Kambarage Nyerere, ambaye alikuwa mwalimu, mshauri na kamanda wa Hashimu Mbita.
Kamati hiyo ya ukombozi ilifanya kazi ya kuratibu misaada ya vifaa kwa ajili ya wanapigania uhuru kwa kipindi cha miaka 30 kuanzia 1963 hadi 1994, ambapo inaelezwa kuwa bila misaada hiyo, baadhi ya nchi za Kusini mwa Afrika zingeendelea kuwa chini ya utawala wa kikoloni.
Mara baada ya kuteuliwa kuongoza Kamati ya Ukombozi, ambayo moja ya kazi zake ilikuwa ni kutafuta vikundi vya ukombozi katika mataifa ya Afrika yaliyokuwa yakitawaliwa na wakoloni, Brigedia Jenerali Mbita, alishiriki kuvijenga vikosi vya SWAPO (Namibia), MOLINACO (Comoro), PAIGC (Guinea Bissau na Cape Verde), Frelimo (Msumbiji), ANC (Afrika Kusini), ZANU-PF (Zimbabwe) na MPLA (Angola).
Aliviandaa vikosi hivi kupambana na majeshi makubwa yenye silaha nzito za kisasa kwa wakati huo. Alichochea hamasa kubwa katika mapambano ya ukombozi Kusini mwa Afrika kwa kutembelea maeneo yaliyokombolewa Kaskazini ya Msumbiji yaliyokuwa chini ya Frente de Libertação de Moçambique (FRELIMO), akitaka kushuhudia kwa macho yake hali ilivyokuwa katika uwanja wa mapambano na kuangalia ni aina gani ya mahitaji yaliyokuwa yakihitajika.
Alibaini kikwazo kikubwa kilichokuwa kinawasumbua wapiganaji wa Frelimo ni mashambulizi ya anga kutoka ndege za kivita za wakoloni wa Kireno. Hivyo alifanya juhudi za kuwapatia wapiganaji silaha zilizowawezesha kukabiliana na mashambulizi hayo na kuviwezesha
kuwa vikosi vya Frelimo kusonga mbele zaidi—hatua iliyofanya maofisa wa kijeshi wa Ureno kutambua kuwa hali katika medani ya vita ilikuwa imebadilika na kwamba wasingeweza tena kushinda vita hivyo.
Hali hii iliwalazimu Wareno kusalimu amri na kuanzisha majadiliano na Frelimo kwa ajili ya kuunda serikali ya mpito iliyochukua madaraka mwaka 1974 na hatimaye kupatikana uhuru kamili Juni, 1975. Mipango madhubuti ya Kamati ya OAU chini ya Mbita, iliziwezesha nchi nyingine kupata uhuru. Nchi hizo ni Sao Tome na Principe (Julai 1975, Angola (November 1975, Zimbabwe (1980), Namibia (1990) na hatimaye uchaguzi wa kidemocrasia huko Afrika ya Kusini (1994).
Kwenye mkutano uliofanyika Arusha mwezi Agosti, mwaka 1994 kwa ajili ya kuhitimisha shughuli za Kamati ya Ukombozi, Jenerali Mbita alisoma hotuba iliyopewa jina “Jukumu limekamilika.” Kupitia hotuba hiyo, Mbita hakusita kuwaenzi mashujaa wenzake katika harakati za ukombozi barani Afrika waliopatwa na umauti kabla ya kushuhudia uhuru katika mataifa waliyokuwa wakiyapigania. Mashujaa hao ni Amilcal Cabral (Guinea Bissau), Herbert Chitepo, Jason Ziyaphapha Moyo, Josiah Tongogara (Zimbabwe), Eduardo Mondlane (Msumbiji), Steve Biko, David Sebeko aliyejulikana kama “Malcolm X” , Solomon Mahlangu, Christ Hani, Duma Nokwe, wote wa Afrika kusini. Nokwe alikuwa Katibu Mkuu wa ANC (1958 hadi 1969). Wengine kutoka Afrika Kusini Johnny Makatini na Oliver Reginald Kaizana Tambo, na Peter Nanyemba wa Namibia.
Hashim Mbita, ambaye baba yake alikuwa karani wa Shirika la Reli la Tanganyika, alizaliwa mwaka 1933, mkoani Tabora na kupata elimu yake ya sekondari Tabora Boys.
Alijiunga na chama cha TANU mwaka 1958 na kuhamia Dar es salaam. Mwaka mmoja kabla ya uhuru wa Tanganyika, wakati huo vijana, hasa wa kiume, wakiajiriwa kwenye mafunzo ya huduma katika utumishi wa kiraia, ikiwa ni katika hatua za maandalizi ya uhuru wa Tanganyika Desemba 1961.
Alipangiwa kazi kwenye Kitengo cha Habari, Wizara ya Habari na muda mfupi baadaye, aliteuliwa kuwa Mwandishi wa Habari wa Rais Julius Nyerere. Pamoja na kazi nyingine, alikuwa akiandaa mikutano na waandishi wa habari, hasa nyakati za ziara rasmi za viongozi kutoka nje ya Tanzania.
Moja wapo ya mikutano yake na waandishi wa habari yenye kukumbukwa sana ni ule alioandaa wakati wa ziara ya Waziri Mkuu wa China, Zhou Enlai (tamka Chou Enlai) mwezi June mwaka 1965.
Mbita aliteuliwa kuwa Katibu Mtendaji Mkuu wa TANU, baadaye Rais Nyerere kumpeleka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kuwa Mkuu wa Kitengo cha Siasa (Political Commissar). Alipata mafunzo ya kijeshi hapa Tanzania na baadaye alipelekwa Uingereza kwa lengo la kusaidia kulijenga Jeshi kuwa la kizalendo baada ya maasi ya mwaka 1964.
Nyerere alimuandaa kwa jukumu muhimu zaidi la kuongoza Kamati ya Ukombozi ya OAU—kazi ambayo aliifanya kwa moyo na kujituma na hatimaye kumtambulisha kitaifa na kimataifa kama alama ya ukombozi (liberation icon) ya Tanzania na Afrika.
Mbita ambaye aliwahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, alifariki siku ya Jumapili, tarehe 26 April, 2015 kwenye Hospitali Kuu ya Jeshi, Lugalo jijini Dar es Salaam akiwa na umri wa miaka 81na kuzikwa Kisutu, jijini Dar es salaam.
Hashim Mbita alipewa tuzo hiyo kwenye mkutano wa SADC uliofanyika kwenye Mji wa Victoria Falls nchini Zimbabwe mwaka 2014, ikiwa ni kutambua mchango wake katika mapambano ya ukombozi wa Bara la Afrika. Kwa kupewa tuzo hiyo, aliingia katika orodha ya watu sita pekee kuwahi kutunukiwa tuzo hiyo.
0 Comments