Katika historia ya Taifa hili tunaona kwamba Wajerumani walipata upinzania wa kutosha kutoka kwa watawala mbalimbali wa Kiafrika. Upinzani huo ni matokeo ya utawala katili wa Wajerumani dhidi ya Waafrika.
Mpelelezi wa Kijerumani, Karl Peters na wenzake akina Juhlke, Pfeil na Otto walifika Zanzibar mnamo tarehe 4 mwezi Novemba mwaka 1884. Kwa mujibu wa I.N.Kimambo na A.J.Temu ambao ni waandishi wa kitabu cha “A HISTORY OF TANZANIA,” Wajerumani hao hawakukaa sana Zanzibar bali walisafiri na kuelekea ndani ya Tanganyika.
Wanasema kuwa katika kusafiri kwao, walipita Uzigua kufuata Mto Wami hadi kufika Uluguru. Wakiwa njiani, waliweza pia kuingia mikataba ya uongo (bogus treaties) na machifu wa maeneo hayo. Moja kati ya mikataba maaruf ni ule uliowekwa kati ya Mjerumani Karl Peters na Sultani Mangungo wa Msovero katika Usagara.
Kwa kuwa Machifu hawakuwa na uwezo wa kusoma wala kuandika Kijerumani, ili bidi watumike wakalimani katika kusaini mikataba hiyo. Kimambo na Temu wanasema kuwa mkalimani maarufu ambaye Karl Peters alimtumia alikuwa akijulikana kwa jina la Ramazan. Huyo alikuwa akipokea tu maagizo kutoka kwa Karl Peters.
Kwa kupitia mikataba hiyo, Wajerumani walionekana kuwa na haki na uhalali wa kuitawala Tanganyika na maeneo mengine ya Afrika. Hadi kufikia mwaka 1891, Tanganyika ilikuwa chini ya Utawala wa Wajerumani.
Kwa kupitia mikataba hiyo, Wajerumani walionekana kuwa na haki na uhalali wa kuitawala Tanganyika na maeneo mengine ya Afrika. Hadi kufikia mwaka 1891, Tanganyika ilikuwa chini ya Utawala wa Wajerumani.
Katika kutawala kwao, Wajerumani waliwanyang’anya Waafrika ardhi yao na kufungua mashamba makubwa kama vile mashamba ya mkonge pale Morogoro na mashamba ya pamba kule Umatumbini. Waafrika walilazimishwa kufanya kazi katika mashamba hayo na shughuli zingine kama vile ujenzi wa barabara na reli.
Kazi hiyo ilikuwa ngumu kwani iliambatana na vipigo na hata kuuawa pia. Ukatili wa aina hii ndio uliowafanya waafrika kumpa Karl Peters jina la “Mkona wa damu” (the man with bloodstained hands).
Hivyo, Watawala wa Kiafrika katika makabila mbalimbali, na kwa nyakati tofauti waliamua kupinga uvamizi na utawala wa wakoloni na hivyo walianza kupigania haki yao ya kujitawala.
Temu na Kimambo wanasema kuwa upinzani uliosababisha mapigano dhidi ya wakoloni wa Wakijerumani uligawanyika katika sehemu kuu nne, yaan Ukanda wa Pwani , Kaskazini, Magharibi na Kusini, lakini baadaye ikafuatiwa na vita vya Maji Maji.
Kwa ukanda wa Pwani, Abushiri bin Salim na Bwana Heri walipinga uvamizi wa Wajerumani kwenye mwaka wa 1888 kule Pangani na Sadani. Mapigano hayo yalidumu hadi mwaka 1889 wakati ambapo Abushiri aliuawawa kwa kunyongwa pale Bagamoyo, na Bwana Heri alitorokea Bara.
Baada ya Abushiri na Bwana Heri kushindwa katika vita ile, mwaka 1894 ndipo Hassan bin Omari Makunganya alipoongoza mapambano dhidi ya Wajerumani pale Kilwa. Naye aliuawawa kwa kunyongwa kwenye mwaka 1891 kwenye mti wa mwembe uliokuwa ukijulikana kama Mwembe Kinyonga (hangman’s mango tree) ambao Wajerumani waliutumia sana kunyongea Waafrika.
Kwa upande wa Kaskazini, Kimambo na Temu wanasema kuwa wakati Wajerumani walipofika Kilimanjaro, Chifu Rindi (Mandara) wa Moshi aliungana nao kupigana dhidi ya Chifu Sina wa Kibosho kwenye mwaka 1891.
Katika vita hivyo, Sina wa Kibosho alishindwa na alifanikiwa kuwatoroka Wajerumani. Kama ilivyokuwa kwa Chifu Rindi, Chifu Marealle wa Marangu naye aliungana na Wajerumani dhidi ya Chifu Meli wa Moshi.
Kwa upande wa Magharibi, waandishi hao wanasema kuwa hakukuwa na upinzania mkali sana isipokuwa Tabora. Wanasema hadi mwaka 1885, Isike Chifu wa Wanyamwezi alikuwa na jeshi lenye nguvu na hivyo aliweza kufaidika kutokana na njia kuu ya biashara iliyokuwa inaunganisha Mwanza, Ujiji na Pwani kupita katika Himaya yake.
Wanaongeza kuwa Isike alitumia nafasi hiyo kwa kuwatoza watu waliokuwa wanapita kwenye Himaya yake ushuru uliokuwa unajulikana kwa jina la hongo. Kitendo hicho kilipingwa na Wajerumani hivyo vita vikazuka dhidi ya Isike kwenye mwaka 1892. Mapigano hayo yalidumu hadi mwaka 1893 ambapo Isike alipigwa, kwa kukataa kukamatwa na Wajerumani, Isike aliamua kujiua.
Kwa upande wa Kusini mwa Tanzania, Machemba Chifu wa Wayao, aliwashinda Wajerumani mara nyingi kwenye mwaka 1890 kwani alipinga kuwalipa Wajerumani kodi ya nyumba (hut tax). Ilipofika mwaka 1899, ndipo Wajerumani walipopigana vita dhidi ya Machemba na kumshinda, wafuasi wake walikamatwa na kufungwa, lakini yeye Machemba alitoroka na kukimbilia Msumbiji.
Baada ya hapo, Wajerumani pia walikutana na upinzani mkali kutoka kwa Wahehe. Wakati huo Wahehe walikuwa imara sana chini ya kiongozi wao Mkwawa. Kama ilivyokuwa kwa Isike wa Tabora, Mkwawa naye aliwatoza hongo wale wote waliokuwa wakifanya biashara katika Himaya yake au waliokuwa wakipita hapo. Kitendo hicho kiliwaudhi wakoloni wa Kijerumani.
Baadaye, Mkwawa aligundua kuwa Wajerumani hawakuwa tayari kutii amri au maagizo yake kitu ambacho Mkwawa alikitafsiri kuwa ni dharau na matusi kwake kama Mtawala. Hivyo Mkwawa aliamua kufunga njia ya biashara kati ya Bagamoyo na Tabora kama kisasi dhidi ya Wajerumani.
Ndipo mwaka 1894 Wajerumani walipoamua kuishambulia Ngome ya Mkwawa (Kalenga) kutokea upande wa Tosamaganga. Mapigano hayo yalidumu kwa siku tatu na Wajerumani walifanikiwa kuiteka Ngome hiyo.
Hata hivyo, Mkwawa alitoroka na kuanzisha vita vya msituni (guerilla war) kwa miaka mine. Wajerumani walijaribu kumkamata lakini walishindwa, ndipo Gavana wa Ujerumani von Liebert alipotoa ofa ya rupia 5,000 kwa mtu yeyote ambaye angeweza kumpatia kichwa cha Mkwawa. Ilipofika mwaka 1898, Mkwawa alijua mwenyewe kwa kujipiga risasi.
Kwa hiyo upinzani dhidi ya utawala wa kikoloni uliendelea katika maeneo mbalimbali hadi kufikia vita vya Maji Maji mwaka 1905 hadi 1907.
Kimambo na Temu wanasema kuwa vita hivi vya Maji Maji vilikuwa tofauti na vita vilivyotangulia katika maeneo mengi. Vita hivi vilihusisha makabila mengi yaliyoungana dhidi ya Wajerumani. Vita hivyo vya Maji Maji vinachukuliwa kama ndio mwanzo wa mapambano ya kupigania uhuru.
Jujila (Jwiywila) yalikuwa mawasiliano ya siri ambayo waafrika waliyatumia kuelezana kuwa kule Ngalambe kuna mganga mwenye nguvu na dawa yenye nguvu ya kuweza kuwashinda wazungu.
Mganga huyo alikuwa Kinjikitile Ngware ambaye aliwapatia watu hao dawa na kuwataka warudi kila mtu alikotoka na kuendelea kufanya kazi kwa Wajerumani mpaka hapo atakapowatangazia siku rasmi ya kuanza vita. Lakini Wamatumbi hawakuwa na subira, bali waliwaudhi Wajerumani walipovamia mashamba ya pamba na kuanza kung’oa miche ya pamba kwenye mashamba yaliyopo Nandette, hapo ndipo vita ilipoanza.
Vita hivyo vilienea katika maeneo mbalimbali kama vile Mohoro, Utete, Namatewa, Muhinje, Njinjo, Kilosa, Ziwa Malawi, Liwale, Mahenge, Lukuledi na hatimaye Wangoni nao wakaingia kupigana dhidi ya Wajerumani. Wajerumani walishinda vita hivyo mwezi Agosti mwaka 1907.
K wa hiyo waafrika walipinga na kupigana dhidi ya Utawala wa kikoloni wa Wajerumani katika maeneo mbalimbali, walikuwa wanapigania haki yao ya kujitawala. Kwa hiyo miaka 50 ya uhuru iwe ni sehemu ya kutafakari tulipotoka, tulipo na kuandaa mazingira mazuri ya tunakotaka kufika kwa miaka 50 mingine ijayo.
0 Comments