Aidha, mji wa Songea una umaarufu wa mashujaa waliopigana vita vya Majimaji kati ya mwaka 1905 hadi 1907. Wanahistoria hawa mashujaa tunawakumbuka kwa minajili gani? Kwamba vikosi na viongozi wa vita vya majiamji walipigania nini? Shabaha ya kuingia vitani
NAKUULIZENI wanahistoria. Ninalo dukuduku dhidi yenu. Nahitaji usahihi juu ya historia ya nchi ya Tanzania iliyotokana na Tanganyika na Zanzibar. Nijibuni, kwa historia ya Tanganyika tunayowarundikia vijana wetu shuleni, ni sahihi? Nitajieleza.
Historia iliyopo sasa inaeleza kuwa mbio za kuwania uhuru wa Tanganyika ulikolezwa zaidi jijkini New York nchini Marekani. Ni jiji la New York ambapo wanaharakati wetu wa uhuru walitumia kila mwanya kuhakikisha wanaweka ushawishi wao ndani ya League of Nations) (baadaye United Nations) kuhakikisha Tanganyika inapatiwa uhuru wake.
Tangu tukiwa shuleni, vyuoni hadi mitaani tunefundishwa kuwa hsitoria ya Tanganyika kupata uhuru ilikuwa bila kumwaga damu. Kwamba wakati Tanganyika ikipigania uhuru tunaambiwa hatukumwaga damu yoyote badala yake tulipata uhuru kwa amani.
Tumeimbishwa nyimbo. Tumekaririshwa kauli mbiu. Tumehamasishwa kwenye mchakachaka. Tumeimba kila aina ya mashairi na ngonjera zenue kusisitiza kuwa Tanganyika ilipata uhuru bila kumwaga damu.
Ndugu wanahistoria wa taifa letu la Tanzania lililozaliwa Aprili 26 mwaka 1964 baada ya muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Ninalo dukuduku. Limenishika kooni. Akilini limenisonga mno. Aghalabu tumeambiwa kuwa ‘Tanganyika ilipata uhuru bila kumwaga damu”. Kauli hii inanitatiza maradufu.
Kwa muda mrefu sana natatizwa sana hiyo kauli. Nimefundishwa shuleni na vyuoni lakini bado napata tabu; Kivipi Tanganyika (baadaye Tanzania) haikumwaga damu?
Naeleza kidogo. Kwamba ukoloni wa Tanganyika umeanza muda mrefu na palikuwepo upinzani tangu wakati wa Ujerumani. Tunaanza na Ujerumani huku tukiwaacha Waarabu, Wareno na Uingereza.
Historia inatuonyesha kuwa Uingereza ilikabidhiwa kuitawala Tanganyika mara baada ya vita vya kwanza vya dunia. Katika vita vya kwanza vya dunia, Ujerumani ilichakazwa hivyo basi ikaporwa baadhi ya makoloni yake Afrika mashariki.
Je Tanganyika “hatukumwaga damu” baada ya kuwa kipindi cha Uingereza ambacho tulikuwa chini ya uangalizi hadi kupatiwa uhuru mwaka 1961? Kwamba historia ya ukoloni inaanzia hapo?
Au, Tanganyika “hatukumwaga damu” katika kipindi cha ukoloni wa Ujerumani? Nyongeza ni kwamba historia yetu dhidi ya ukoloni haimtambui mkoloni Mjerumani?
Je katika “resistance” zote zilizoendeshwa dhidi ya ukoloni hakuwepo raia wala wapiganaji wa kutoka vikosi vya watanganyika wenzetu hivyo “hatukumwaga damu” hadi tukapewa uhuru?
Ndiyo kusema akina Mangi Meli, Chifu Rumanyika, Mtemi Kimweri, Kinjekitile Ngware, Mirambo, Nduna Songea Mbano, Isike, Mangungo na Chifu Mkwawa kwa kuwataja wachache, hawakumwaga damu katika vita vyao dhidi ya wageni (wakoloni) wa Waarabu, Wareno,Wajerumani na baadaye Waingereza?
Muungwana mmoja aliwahi kujibu kuwa wazee hao walipambana dhidi ya utumwa sio ukoloni wa mwafrika. Hilo ni jibu ambalo halikati kiu. Jibu la kuremba tu katika hoja ya msingi ya usahihi wa historia ya Tanganyika na baadaye Tanzania.
Ninavyoona kulikuwa na awamu za mapambano ya uhuru wa Majimbo (yale yaliyokuwa chini ya machifu/ ufalme) lakini yakiimarisha utaifa wa Tanganyika.
Ndiyo kusema, awamu nyingine ilikuwa kuanzisha vita vya moja kwa moja dhidi ya wakoloni. Vita hivi ni kama vile Majimaji kwa upande wa Tanganyika ama jirani zetu Kenya walivyopambana kwenye viota vya Maumau.
Awamu nyingine ikawa ya wanazuoni walisomeshwa na wakoloni wakidai uhuru na kupinga utumwa wa mwafrika. Kundi hili ndimo walimo akina Julius Nyerere, Kenneth Kaunda, Robert Mugabe na wale wa wanachama waliohudhuria London Conference ya mwaka 1900 pamoja na Paris Conference ya mwaka 1919. Hizo na nyinginezo za mapambano ya uhuru.
Aidha, mji wa Songea una umaarufu wa mashujaa waliopigana vita vya Majimaji kati ya mwaka 1905 hadi 1907. Wanahistoria hawa mashujaa tunawakumbuka kwa minajili gani? Kwamba vikosi na viongozi wa vita vya majiamji walipigania nini? Shabaha ya kuingia vitani dhidi ya mkoloni ilikuwa ni ipi nje ya mapambano ya uhuru?
Vilevile damu zao zilimwagika wakipigania nini ndani ya Tanganyika ya Tanzania ya leo? Wanahistoria nakualikeni. Nakuulizeni swali hili. Nielimisheni.
Mnamo Julai 13 mwaka 1897 mjino Songea ulifanyika mkutano kati ya utawala wa Ujerumani na Machifu na Manduna chini ya Mkuu wa jeshi la Ujerumani eneo la Ungoni, Luteni Englhardt kutishia kuwaua viongozi wasiotii amri ya wakoloni hao. Kilichotokea ni umwagaji damu.
Sasa ilikuwaje Tanganyika ikapata uhuru bila kumwaga damu kisa tu “chini ya uangalizi’ wa Uingereza? Sijaridhishwa.
Ama baada ya kuzaliwa jina ‘Tanzania’ na historia yote ya Tanganyika ilifutwa? Kama jibu ni ndiyo, ni kwanini tunaadhimisha historia ya uhuru wa Tanganyika wa Disemba 9 mwaka 1961 badala ya Aprili 26 ya kuzaliwa nchi ya Tanzania?
Kama Disemba 9 mwaka 1961 muhimu, ni kwanini vipindi vyake vimeachwa na kusema “hatukumwaga damu” wakati vifo, maafa na kila kona ya taifa kulitapakaa mapigano ya kudai uhuru? Yote hayo ni sehemu ya historia ya yaliyotokea katika ardhi ya Tanganyika, viweje haviwekwi kwenye usahihi wake? Tangu wafanyakazi walipoanzisha chama Tanganyika African Associations mwaka 1929 na baadaye kuanzishwa Tanganyika African National Union (TANU) mnamo mwaka 1954, ni kipindi kifupi sana.
Je si jambo la aibu kujivisha historia nzima ya mapambano ya uhuru dhidi ya ukoloni na wakoloni ikijinasibisha “hatukumwaga damu” ya disemba 9 mwaka 1961?
Je, hii ina maana tangu mwaka 1885 hadi 1929 kilipoanzishwa chama cha TAA, Tanganyika haikumwaga damu?
Je ina maana tangu mwaka 1920 hadi 1961 Tanganyika ilipokuwa chini ya Uingereza hakuna watu watanganyika waliopigana dhidi ya ukoloni hadi kumwaga damu?
Tunaambiwa Tanganyika “hatukumwaga damu’ lakini wakati huo huo sababu ya kushindwa katika vita vyao dhidi ya wakoloni ilikuwa ni zana duni, usaliti miongoni mwa waafrika na uongozi mbovu. Natatizwa.
Katika kipindi tulichokuwa chini ya uangalizi, ndicho vilizaliwa vyama vya TAA kisha TANU. Ina maana historia ya Tanganyika kisha Tanzania inaanzia pale ilipozaliwa TAA na TANU? Hii ndiyo historia ya taifa la Tanzania ya leo?
Kimsingi hawa nao waliendeleza kudai uhuru (kuendeleza yaleyale ya mababu na wazee wetu). Sasa viweje hawa wa mwisho watuambie “hatukumwaga damu” wakati zoezi walilikuta na wakaliendeleza?
Huu uhuru ni ule wa kuteremsha bendera ya mkoloni Mwingereza na kupandisha ya Mtanganyika? Au ya kukabidhiwa cheti cha uhuru? Kwani huyu mkoloni alianzia wapi na wapinzani wake walianza lini na wapi?
Natatizwa. Nielimisheni. Nina mengi. Leo naishi hapa.