Image result for biashara YA UTUMWA

Kama ilivyokuwa Afrika ya Magharibi, biashara ya watumwa katika Afrika ya Mashariki ilikuwa mashuhuri na ilianzishwa kikamilifu na kutokana na maendeleo na jitihada za nchi za Kikristo za Ulaya. Bwana E. A. Alpers anaandika kwenye “African Slave-Trade (Biashara ya Utumwa ya Afrika):
Ushahidi zaidi kwamba biashara ya watumwa kwa vyovyote vile ilikuwa mashuhuri katika Afrika ya Mashariki kabla ya karne ya kumi na nane, imeletwa na Wareno. Hakika Wareno, wakiwa ndiyo waasisi (waanzilishi) wa Atlantic Slave-Trade, wangejaribu kuendeleza biashara ya watumwa katika Afrika ya Mashariki kama wangeikuta tayari ipo na imekwisha shamiri. Lakini maandiko ya mwanzo ya Wareno yanataja tu biashara ya watumwa kwa kupitia tu.
Lililokuwa muhimu zaidi ni wale wafanyabiashara za dhahabu na pembe za ndovu walizipeleka Arabuni na India. Wavamizi wa Kireno walielekeza juhudi zao kwenye bidhaa hizo wakati wa karne ya kumi na sita na kumi na saba, sio tu kwenye pwani ya Kenya na Tanzania, bali pia katika Msumbiji na Zimbabwe. Hata nta na ambari zinaonyesha zilikuwa bidhaa muhimu zaidi kuzidi watumwa wakati mrefu sana wa kipindi hiki. Kwani tofauti na wakoloni katika nchi ya Amerika, Wareno kamwe hawakuanzisha uchumi wowote wa kilimo huko India.
Biashara ya watumwa ya Wareno kutoka Msumbiji kwenda India kwa nadra sana ili- fika idadi ya watu elfu moja katika kipindi cha mwaka mmoja wowote ule, na kwa kawaida ilikuwa chini ya nusu ya idadi hiyo. Huko Brazil ilikuwa haramu kufanya biashara ya watumwa hadi mwaka 1645, na kamwe haikulitiliwa maanani hadi mwanzoni mwa karne ya kumi na tisa. Hadi mwaka wa 1753, wakati misingi ya biashara mpya ya watumwa ilikuwa inawekwa Afrika ya Mashariki, palikuwepo na jumla ya watumwa 4399 tu wa Kiafrika katika India yote ya Wareno.
“Misingi hii ni ipi? Licha ya mahusiano ya muda mrefu baina ya Waarabu na Afrika ya Mashariki, biashara ya watumwa haikutiliwa matumaini na Wafaransa. Kwa mujibu wa tarakimu rasimi, zaidi ya watumwa 1,000 walikuwa wanasafirishwa kila mwaka. Wafaransa, wakifanya magendo kwa ajili ya kukwepa kodi ambazo zilitozwa Msumbiji, labda waliongeza idadi na kufika angalau 1,500. Inawezekana ni idadi ile ile ilichukuliwa kutoka Ibo wakati wa muongo huu. Kwa hiyo Wareno kule Msumbiji na Ibo (na baadaye Quelimane, karibu na mdomo wa mto Zambezi unapoingilia baharini) walijishughulisha na sera ya biashara ya watumwa na hawakurudi nyuma, wakaendelea nayo hadi kukomeshwa kwake.
Biashara ya watumwa ilizidi kupamba moto mnamo miaka ya themanini, hasa zaidi baada ya kumalizika vita ya uhuru wan chi ya Amerika.
Katika miaka ya sabini, wafanya biashara ya utumwa wachache wa Kifaransa walichukua mizigo kutoka Msumbiji kwenda visiwa vya West-Indies, kwa sababu waliiona hasara ilikuwa inaongezeka katika wakati wa kutafuta bidhaa zao zinazohamashika kwenye pwani ya Guinea. Sasa, wakati wa amani, kwa mashindano makubwa zaidi ya kutafuta watumwa katika Afrika ya Magharibi, ilifunguliwa njia kwa ajili ya upanuzi mkubwa wa biashara ya watumwa ya Waamerika kutoka Afrika ya Mashariki.
Wakati huo huo meli za Wareno pia zilianza sehemu ya kufaa (ingawa ilikuwa bado ni ya kufuata) katika biashara ya watumwa kwenda kisiwa cha Mascarene. Tarakimu rasimi kutoka Msumbiji peke yake zinaonyesha kwamba tangu 1781 hadi 1794 jumla ya watumwa 46,461 walipakiwa kwenye meli za Kireno na za kigeni, ambazo karibu zote zilikuwa za Wafaransa. Ikijumlishwa na idadi ndogo ya magendo, angalau watumwa 4,000 lazima walikuwa wanaondoka Msumbiji wakati wa kipindi hiki kila mwaka.” 1
Ilikuwa katika hali hii ambayo Waarabu walipanua msaada wao kuwasaidia hawa wafanyabiashara ya utumwa wa Kikristo. Mwandishi huyo huyo anasema: “Baada ya Waarabu wa Oman kuitika wito wa baadhi ya watawala wa Kiswahili wa miji ya pwani na kwa msaada wao waliwatoa Wareno kutoka Mombasa mnamo 1698 na sehemu zingine muhimu za mbali, wao wenyewe walikuwa wanyonge sana kushughulika na jambo lingine zaidi ya kuwasumbua na kuwaibia watu hao hao waliowaomba msaada wao; lakini baada ya familia ya Busaid ilipowapindua Yarubi na kuanzisha utawala wao katika Oman mnamo 1744, wali- weza kuanza unyonyaji wa kiuchumi wenye faida kutoka kwa watu wa Afrika ya Mashariki. Kama walivyofanya wafanya biashara wote wa zamani sehemu ya pwani, lengo lao kubwa na la msingi ni kupata pembe za ndovu, lakini kuanzia hapo pia tunaweza kuona ongezeko katika biashara ya watumwa.
“Hata hivyo, hakuna takwimu sahihi zozote zile zenye kuonyesha kuhusu ukubwa wa biashara ya utumwa iliyofanywa na Waarabu katika karne ya kumi na nane. Dalili ya kwanza iliopo inatoka kwa mfanya biashara ya watumwa wa Kifaransa aitwaye Jean Vincent Morice, ambaye alifanya biashara Zanzibar na Kilwa, ambayo ilikuwa bandari muhimu ya watumwa katika pwani, mnamo miaka ya 1770. Mnamo tarehe 14, September, 1776, Morice alifanya mkataba na Sultani wa Kilwa kwa ununuzi wa angalau watumwa
1,000 kwa mwaka. Katika misafara mitatu kabla ya kuutia sahihi mkataba huu, Morice alikwisha nunua watumwa 2325 kwa ajili ya kuwasafirisha nje. Morice hatuambii Waarabu walikuwa wakiwachukua watumwa wangapi kutoka pwani kila mwaka, lakini kwa wazi aliona kuwa ilikuwa biashara kubwa kwa viwango vya Kifaransa.
Inaonekana ni sawa kusema kwamba angalau watumwa 2000 walikuwa wanachukuliwa kwa mwaka katika kipindi hicho. Kwa hiyo, licha ya kwamba Wafaransa hawakutawala biashara ya watumwa hapa kama walivyofanya Msumbiji, walikuwa kichocheo kwa mahitaji ya soko la watumwa katika kipindi ambacho biashara ya Waarabu ilikuwa bado ndiyo inakua katika uchanga wake. Juhudi za Ufaransa ziliendelea hadi miaka ya 1780, lakini mnamo mwishoni mwa karne hiyo, juhudi hizi zilionyesha zilikwisha pungua sana umuhimu wake kuliko biashara ya Waarabu.
Mambo kadhaa mapya yalisababisha kuongezeka mahitaji ya watumwa kutoka Afrika ya Mashariki wakati wa karne ya kumi na tisa. Katika eneo la mamlaka la pwani ya Ureno, palikuwepo na ongezeko la juu sana katika biashara ya utumwa kwenda Brazil. Hii ilisababishwa na kuondolewa kwa familia ya kifalme ya Kireno kutoka Lisbon kupelekwa Brazil wakati wa Vita za Napoleon. Ruhusa maalum zilitolewa kwa Wabrazil na mara biashara inayoshamiri katika watumwa ikawa inaendeshwa kupitia Rasi ya Tumaini Jema huko Afrika ya kusini.2
“Sasa ni ukweli unaokubalika miongoni mwa wataalam wa historia makini wa Afrika ya Mashariki kwamba njia ndefu za biashara kati ya bara na pwani zilianzishwa hasa zaidi kwa kutumia ujasiri na moyo wa kujituma wa Waafrika. Kwa maneno mengine njia za biashara zilibuniwa na Waafrika kutoka bara kwenda pwani, wala si Waarabu, au Waswahili, ambao walisafiri kutoka pwani kwenda bara kupitia sehemu zisizojulikana.
Wafanya biashara wa Kiswahili walianza tu kutelekeza usalama wa pwani mnamo nusu ya pili ya karne ya kumi na nane, na walisafiri kufuata njia safi ambazo ziliendelezwa kwa miongo mingi kabla yake. Ni baada tu kuanza karne ya kumi na tisa ndipo wafanya biashara wa Kiarabu walijasiri kufuata njia hiyo.” 3
Wayao ambao walikuja kuwa wafanya biashara makini sana wa Kiafrika wa biashara ya watumwa katika Afrika ya Mashariki, hivyo walikuwa na desturi ya muda mrefu ya kubeba pembe za ndovu na bidhaa zingine halali kwenda pwani miongo mingi kabla ya mahitaji ya pamoja ya Wafaransa na Waarabu kutaka watumwa yalipoeleweka.”4
“Katika Afrika Magharibi njia hizi ziliendeshwa kwenda bara kutoka pwani na Waafrika ambao kazi yao hasa ilikuwa kutafuta watumwa. Watumwa walitawala biashara ya Afrika ya Magharibi tangu mwanzo. Katika Afrika ya Mashariki wala hapakuwepo na hali zilizolingana na hiyo. Biashara ya watumwa lazima ionekane kuwepo katika mazingira ya mapema zaidi, iliyokwishajengeka kwa umakini, na biashara yenye faida ya masafa marefu ambayo chimbuko lake ilikuwa ubebaji wa pembe za ndovu. Hii ni muhimu kukumbuka hasa kwa mikoa ya kusini ambalo kila mara ilikuwa hazina kuu ya “Biashara ya Utumwa katika Afrikamashariki.”5
Bwana Alpers anahitimisha, “lazima iwe wazi sasa kwamba fikira ya zamani inayotamkwa kiholela kwamba wengi wa watumwa walikamatwa na wafanya biashara wanyang’anyi wa Kiarabu na Kiswahili ni moja wapo ya mambo ya kubuniwa na ngano tu ambazo zimekuzwa kuhusu biashara ya watumwa ya Afrika mashariki. Lakini lazima tuwe waangalifu tusifanye kosa la kutoa tathmini potofu kuhusu mchango waliotoa watu hawa kwenye biashara hii.” 6
Kwa mara nyingine, lazima nisisitize kwamba lengo langu si kudhihaki juhudi za kundi dogo la waadilifu ambao walikuwa wanashughulika na propaganda dhidi ya utumwa. Ninachotaka kuonyesha ni kwamba juhudi zao hazikufaulu (na hazingefaulu) hadi pale shinikizo la kiuchumi lilipoilaz- imisha kwanza Uingereza ilipolazimika kufuatana na matatizo ya kiuchumi kuanza kuzuia utumwa, biashara ya utumwa na halafu kukomesha utumwa.
Kwa kweli, Uingereza ilipojitokeza kwa ajili ya kutaka kukomesha utumwa haikusimama kwenye mapaa ya nyumba na kutangaza kwamba ilikuwa inakomesha utumwa kushindana dhidi ya wenye viwanda wa Kifaransa. Uingereza ililigeuza jambo hili kuwa suala la kimaadili na kiunyofu kabla haijatumainia kushinikiza serikali zingine kufuata mpango wake. Na ilifanya hivyo. Tunatambua jinsi Uingereza ilivyoanzisha vita si kwa lengo la kulinda maslahi ya himaya yake kiuchumi na kisiasa, lakini ilifanya hivyo ili “kulinda Uhuru wa Watu.”
Ndivyo ilivyokuwa kuhusu vita yake dhidi ya utumwa. Murua na maadili mema lilikuwa suala la waadilifu wachache tu ambao hawakuwa na uwezo. Suala halisi, kama serikali mbali mbali na walowezi na wakoloni walivyohusika, lilikuwa kuhusu uchumi.