MIAKA 20 BILA NYERERE: Maisha ya utotoni ya Kambarage Nyerere-1





Mtemi Nyerere Burito (1860-1942) wa kabila la Wazanaki na mkewe, bibi Christina Mugaya wa Nyang’ombe, miaka 97 iliyopita walipomzaa mtoto waliyemwita Kambarage, hawakujua kama mtoto wao huyo angekuja kuwa Rais wa Tanganyika miaka 39 baadaye.
Kambarage Nyerere, kama ambavyo alivyojulikana kabla ya kubatizwa kwake mwaka 1943, alizaliwa Aprili 13, 1922 katika Kijiji cha Butiama karibu na Pwani ya Ziwa Victoria.
Kwa mujibu wa historia ya maisha yake, wakati wa utoto wake Kambarage alikuwa akiwasaidia wazazi wake kazi za shambani ikiwa ni pamoja na kuchunga mifugo.
Baadaye Kambarage alikumbuka maisha yake ya ujanani. Alimwambia mwandishi Marie-Aude Fouere wa kitabu cha ‘Remembering Julius Nyerere in Tanzania: History, Memory, Legacy’ “nililelewa sawasawa na watoto wengine pale kijijini. Sikupata upendeleo wowote eti kwa sababu tu baba yangu alikuwa chifu.”
Mama yake Kambarage, Christina Mugaya alikuwa mke wa tano wa Mzee Burito kati ya wake zake 22. Kwa mujibu wa Marie-Aude Fouere, wakati Mzee Burito akiwa na miaka 47 ndipo alipomuoa Mugaya akiwa na miaka 15. Mama Mugaya alimzalia Mzee Burito watoto wanane, wanne wa kiume (Kambarage akiwa wa pili) na wanne wa kike.
Kwa kadri alivyokiri mwenyewe, Kambarage alisema maisha yake yaliathiriwa sana na baba yake. Alipohojiwa na mwandishi William Smith wa kitabu cha ‘Nyerere of Tanzania’ miaka ya 60 alisema “kiwango cha ubinadamu nilichonacho nilirithi kwa baba yangu,” alisema Kambarage.
Burito hakuwa mwepesi wa kuamua mambo. Alikuwa mwangalifu sana kabla ya kuchukua hatua na alisisitiza kila wakati kuwapa watu wake haki zao. Simulizi fulani zinadai kuwa utamaduni wa Wazanaki ndio uliokuwa na ushawishi mkubwa zaidi tangu utotoni katika uwezo wa uongozi wa Nyerere kuliko hata elimu aliyoipata baadaye ukubwani.
Katikati ya Aprili 1934, Kambarage ambaye baadaye aliitwa Julius alilazimika kutembea zaidi ya maili 25 kutoka Butiama kwenda Musoma, akisindikizwa na mmoja wa walinzi wa Mzee Burito aliyeitwa Kitira Buhoro.
Katika ukurasa wa 46 wa kitabu chake, ‘Nyerere: The Early Years’, mwandishi Tom Molony anaandika kuwa baada ya kutembea muda mrefu na kwa kuwa magari yalikuwa yakipita kwa nadra njia hiyo, hatimaye lilitokea lori ambalo Kitira alilisimamisha, likasimama, “hapo Kambarage akapanda gari kwa mara ya kwanza” katika maisha yake.
Ingawa ada ya shule alilipiwa na baba yake, fedha ya kujikimu alipewa na kaka yake aliyeitwa Edward Wanzagi Nyerere. Wanzagi ndiye aliyekuja kuwa chifu wa mwisho wa Butiama (1952-61).
Ijumaa ya Aprili 20, 1934, Kambarage alianza rasmi, Shule ya Msingi Mwisenge iliyoko Musoma na kupewa usajili namba 308. Kati ya walimu waliomfundisha ni James Zangara Irenge. Mvulana wa kwanza kabisa kukutana na Kambarage shuleni hapo aliitwa Selemani Kitundu.
Kitundu ndiye baadaye alikuwa mhamasishaji mkuu wa Chama cha Tanu (Tanganyika African National Union) tawi la Musoma, ambalo hadi Novemba 1955, kwa mujibu wa kitabu cha ‘Historia ya Tanu,’ kulikuwa na wanachama 110 tu katika wilaya yote ya Musoma.
Baadaye Kitundu alikumbuka alivyokutana na Kambarage. Kwa mujibu wa Molony, Kitundu alikumbuka alipokutana na Kambarage alikuwa amevaa ‘rubega’ na kaptula iliyochanika. “Alikuwa mwembamba, mwenye macho ‘makali’ na alikuwa mcheshi,” alisema Kitundu.
Aliyekuwa rafiki wa karibu na Kambarage shuleni Mwisenge ni kijana mwingine wa Kizanaki, Oswald Mang’ombe Marwa. Kambarage na Mwang’ombe walifahamiana kabla ya kukutana shuleni kwa sababu baba yake alikuwa ni Chifu Marwa wa Butuguri na rafiki wa Mzee Burito.
Mang’ombe Marwa, kinasema kitabu cha ‘Peter DM Bwimbo: Mlinzi Mkuu wa Mwalimu Nyerere,’ baada ya hapo alikuja kuwa “…mmoja wa walimu wa useremala hapo Bwiru na kwao palikuwa Butugiri, karibu na Butiama.” Mwang’ombe alifariki dunia Jumapili ya Januari 25, 1970 wakati Kambarage akiwa Rais wa nchi.
Aliyekuwa mshirika mwingine wa karibu na Kambarage shuleni Mwisenge ni John Nyambeho na Marwa Ihunyo kutoka Busegwe.
Ihuyo alimwambia Molony jinsi alivyokumbuka namna kila mwisho wa juma walivyokwenda na Kambarage kuwinda, na siku moja wote wawili wakamlenga ndege mmoja na wakapata shabaha yao kwa kumuua, na kwa sababu hiyo “tulianza kuitana binamu ... na kama tulikuwa na fedha tulikuwa tunakwenda mjini kunywa chai na maandazi.”
Mei 1934, mwezi mmoja baada ya Kambarage kujiunga na shule hiyo, wavulana walipewa sare yao ya kwanza ya shule. Kitundu alimwambia Molony kuwa anakumbuka Kambarage alikuwa mwepesi sana kujibu maswali kwa kasi kubwa.
Baada ya miezi sita shuleni hapo wanafunzi walifanya mtihani wao wa kwanza. Walioongoza kwa ufaulu ni Kambarage na Kitundu kiasi kwamba walivushwa darasa, wakitolewa darasa la kwanza na kuingizwa moja kwa moja darasa la tatu.
Wakiwa darasa la tatu walifundishwa na walimu Joshua Gunza, James Irenge na Daniel Kirigini. Walimu wawili miongoni mwa hao watatu, Daniel Kirigini na James Irenge walikuwa hai wakati wa kifo cha Nyerere Alhamisi ya Oktoba 14, 1999. Kirigini alifariki dunia mwaka 2002, miaka mitatu baada ya kifo cha Mwalimu akiwa na miaka 104.
Baada ya kifo cha Kirigini, mwalimu pekee wa Kambarage aliyebaki hai ni Irenge, ambaye mwaka 2002 alikuwa na miaka 91 wakati wa maadhimisho ya miaka mitatu ya kifo cha Mwalimu Nyerere. Hata hivyo naye alifariki dunia Julai 2012 na kuzikwa Butiama Julai 26, 2012.
Ingawa simulizi fulani zinadokeza kuwa Kambarage hakuwa mtukutu, alipambana na aliyekuwa mkuu wa shule, Herman Abdallah kutoka Lindi, ambaye alichukua fedha za wanafunzi bila ridhaa yao, zikiwamo shilingi mbili za Kambarage. Ingawa aliadhibiwa kwa kilichodaiwa kuwa ni kumkosea mwalimu wake nidhamu, fedha zake zilirejeshwa.
Historia ya utotoni inaonyesha kuwa Kambarage hakupenda michezo. Kwake ilikuwa afadhali ashinde bwenini akijisomea vitabu kuliko kwenda kucheza. Hata hivyo akiwa anajisomea bwenini, mara kwa mara alikuwa akibughudhiwa na kaka mkuu wa shule, Nyamuhanga Mageta, huku akimdhihaki kwa wembamba wake. Kwa sababu hiyo aliamua kujitafutia mahali pengine ambako angeweza kusoma kwa utulivu wakati wengine wakiwa michezoni.
Kambarage na Mang’ombe Marwa walijiunga na kituo cha Nyigena Mission ambako walikuwa wakitembea maili nne kila siku kwa ajili ya mafunzo ya kidini. Ingawa Mang’ombe hakuendelea na masomo hayo, alibatizwa na kuitwa Oswald Mang’ombe Marwa.
Kambarage alimaliza elimu ya msingi mwaka 1936 katika Shule ya Msingi Mwisenge. Kwa mujibu wa mwandishi Godfrey Mwakikagile, katika mitihani yake ya kumaliza shule ya msingi, alikuwa wa kwanza miongoni mwa wanafunzi wote wa Kanda ya Ziwa na Magharibi.

MIAKA 20 BILA NYERERE: Mwalimu Nyerere awa waziri mkuu kwa siku 266 tu -2


By William Shao
Baada ya Chama cha Tanu (Tanganyika African National Union) kushinda katika uchaguzi na kupata idadi kubwa ya wajumbe katika Baraza la Kutunga Sheria (Legco au Tanganyika Legislative Council), Mwalimu Julius Nyerere aliteuliwa na Gavana Richard Gordon Turnbull kushika wadhifa wa waziri kiongozi (chief minister). Nyerere alianza kuutumikia wadhifa huo kuanzia Ijumaa ya Septemba 2, 1960 na alidumu katika wadhifa huo kwa siku 241 hadi cheo kilipopanda tena.
Alipanda cheo na kuwa waziri mkuu kuanzia Jumatatu ya Mei Mei, 1961. Hiyo ndiyo siku aliyoapishwa kuwa waziri mkuu baada ya Tanganyika kupewa serikali ya mambo ya ndani (Internal Self Government) kabla ya uhuru kamili. Hata hivyo, Jumatatu Januari 22, 1962 Nyerere alijiuzulu nafasi ya uwaziri mkuu.
Kwa vipindi tofauti mwaka 1955 na 1956, Nyerere alikwenda New York, Marekani, kuhutubia Umoja wa Mataifa kuhusu uhuru wa Tanganyika. Mwaka baadaye, 1957, alitangaza kuwa Tanu ingeshiriki uchaguzi mwaka 1958 ikiwa tu ungekuwa uhuru na wa haki. Serikali ya kikoloni iliuhakikishia Umoja wa Mataifa kuwa uchaguzi huo utakuwa huru. Huo ndio ulikuwa uchaguzi mkuu wa kwanza Tanganyika.
Kwa mujibu wa kitabu ‘Elections in Africa: A Data Handbook’ © 1999, uchaguzi wa kuwapata wabunge ulifanyika Jumatatu Septemba 8 na Ijumaa ya Septemba 12, 1958. Mwaka uliofuata uchaguzi wa majimbo yaliyobakia ukafanyika Jumatatu ya Februari 9 na Jumapili ya Februari 15, 1959, kisha ukafanyika mwingine Jumanne ya Agosti 30, 1960.
Jarida la ‘Black World/Negro Digest’ la Machi 1962 liliripoti kuwa katika uchaguzi wa 1958, wapiga kura waliojiandikisha kupiga kura walikuwa 885,000. Hadi mwishoni mwa Julai, wagombea 58 wa Tanu walipita bila kupingwa na 39 miongoni mwa hao ni Waafrika.
Tanu ilipata viti 12 kati ya 13 vilivyogombewa katika Baraza la Kutunga Sheria. Mgombea mmoja wa Tanu, Chief Amri Dodo alishindwa na mgombea binafsi aliyeitwa Herman Elias Sarwatt katika jimbo la Mbulu.
Katika hotuba yake ya Mei Mosi 1995 katika Uwanja wa Sokoine Mbeya, Nyerere alikiri: “Sasa, mfano mmoja ninaoutumia mwisho kabisa kabisa, mwaka 1970 sijui 1971 sijui 1972, eeh! Akatupinga kijana wetu mmoja anaitwa Sarawati katika uchaguzi wa vyama vingi.
“Ulikuwa uchaguzi wa vyama vingi eeh? Ndiyo. Ilikuwa uchaguzi wa vyama vingi. Ilikuwa ni katika uchaguzi wa vyama vingi. Viti vingi sana tulivichukua bila kupingwa. Nadhani hivyo ndivyo ilivyokuwa.
“Katika kiti cha Mbulu tumemweka mtu mmoja anaitwa Chifu (Amri) Dodo. Mwanachama wetu mmoja pale anaitwa Herman Sarawati akasema aaah, hiki chama changu hakina akili hata kidogo. Au viongozi wangu hawana akili…Huyu akiwa na mkoloni ndiye aliyetaka kutufunga sisi ndiye wameonelea awe mbunge wetu katika Jimbo la Mbulu?
“Kijana yule akatupinga. Mimi nikatoka Mbeya. Nimesafiri kutoka Mbeya hapa kwenda kumpinga. Kwenda kumtetea yule candidate (mgombea) wa Tanu nikashindwa. Wananchi wa Mbulu na wanachama wengi tu, wakasema Tanu wamekosea. Wakampa kura Sarawati. Mwanachama wa Tanu wakafanya hivyo.
“Anasimama mwenyewe tu. Akatupinga. Ilikuwa haki yake. Mimi nilidhani sasa tunarudisha vyama vingi, tunarudisha na haki zote zile zilizokuwapo za raia, pamoja na haki, si haki ya kuunda vyama tu pamoja na haki ya private candidate (mgombea binafsi) kusimama akafanya kama chama kinavyofanya.”
Kutokana na ushindi wa Tanu katika uchaguzi wa Septemba 1960, Nyerere akawa waziri kiongozi wa Tanganyika, akamteua Derek Bryceson kuwa makamu wake. Serikali ya kikoloni iliweka masharti kadhaa kwa wale ambao wangekuwa wapiga kura katika uchaguzi huo wa 1958. Mojawapo ni lile la kuwataka wapigakura kuwapigia kura (tatu) kutoka kundi la Waafrika, Wahindi na Wazungu.
Legco iliyoundwa na Waingereza tangu mwaka 1926, ilikusudiwa kuwajumuisha Wazungu, Wahindi na Waafrika. Vyama vingine vya siasa vilivyoshindana na Tanu katika uchaguzi huo ni Tanganyika United Party (UTP). Hiki kilikuwa chama cha walowezi lakini kiliungwa mkono na Wahindi wachache na baadhi ya Waafrika.
Kwa kuona utata wa masharti yaliyowekwa na wakoloni kuhusu uchaguzi huo, Tanu iliitisha mkutano wake wa mwaka uliofanyika Tabora kuanzia Januari 21 hadi 26, 1958, ikiwa ni miezi michache kabla ya uchaguzi huo. Ajenda kuu ilihusu uchaguzi huo. Mkutano huo uliitwa kutafakari juu ya ama kushiriki au kuususia uchaguzi.
Masharti mengine ambayo Waingereza waliyaweka ni kwamba ili upige kura lazima kwanza uthibitishe una kipato cha pauni 400 za Uingereza kwa mwaka, uwe na elimu isiyopungua darasa la 12 na ajira ya muda wote ambayo inathibitishwa na serikali ya kikoloni. Masharti yote haya na mengine yalikuwa na lengo la kuwazuia Waafrika wengi kupiga kura katika uchaguzi huo. Kushiriki au kutoshiriki uchaguzi huo kuliwagonganisha sana wajumbe wa mkutano. Hali hiyo iliwafanya wajumbe hao wa Tanu na hivyo kugawanyika makundi mawili, kundi la kwanza likisisitiza chama kishiriki, la pili likitaka kuususia.
Mmoja wa waliosisitiza kuususia uchaguzi huo ni Sheikh Suleiman Takadir, aliyekuwa mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Tanu, na mwingine ni Zuberi Mtemvu, katibu mwenezi wa Tanu. Hawa walikaribia kabisa kukipasua chama na walielekea kufanikiwa kama Nyerere asingeingilia kati kuwashawishi wakubali chama kishiriki uchaguzi.
Ubishani wa Nyerere na Sheikh Takadir kuhusu kushiriki au kutoshiriki uchaguzi ulizidi hadi wawili hao kufikia mahali pa kutoelewana. Matokeo ya hilo Sheikh Takadir alivuliwa uanachama wa Tanu.
Wengine waliopinga vikali Tanu kushiriki uchaguzi huo ni Jumanne Abdallah na Bhoke Munanka. Lakini baada ya siku kadhaa za malumbano makali, Nyerere aliungwa mkono na wengi wakiwamo Abdallah Rashidi Sembe, Hamisi Heri, Mwalimu Kihere, Ng’azi Mohammed, Mustafa Shauri na Abdallah Makata waliokuwa viongozi wa Tanu kutoka Tanga.
Mkutano huo ulitoa tamko kuwa endapo Serikali ya kikoloni haitahakikisha Tanganyika inapewa uhuru bila kuchelewa, Tanu ingewahamasisha wananchi wote wagome. Kwa kauli moja tamko hilo likaitwa “Positive Action”. Pia mkutano huo uliazimia kupinga pendekezo la serikali ya kikoloni la kuitaka Tanu ikubali mpango wa kila mpigakura awapigie watu watatu; Mzungu, Mhindi na Mwafrika ili kushindana na chama kingine cha siasa cha UTP kilichokuwa na matajiri wa Kizungu na Kihindi.
Tanu iliibuka na ushindi baada ya kupata viti 28 kati ya 30 vilivyokuwa vinagombewa. Miaka miwili baadaye, ulipofanyika uchaguzi wa wabunge, Tanu ilipata viti 70 kati ya 71 vilivyogombewa. Kutokana na ushindi huo, Rais wa Tanu, Mwalimu Julius Nyerere, akateuliwa kuwa waziri kiongozi wa Tanganyika Ijumaa ya Septemba 2, 1960. Hata hivyo alidumu katika wadhifa huo kwa siku 241 hadi alipoteuliwa kuwa waziri mkuu wa Tanganyika Jumatatu ya Mei Mosi, 1961.
Hata hivyo, Jumatatu ya Januari 22, 1962 Nyerere alijiuzulu nafasi ya uwaziri mkuu ikiwa ni miezi minane baada ya kuteuliwa kuwa waziri mkuu? Ni kweli alijiuzulu kwenda kukijenga chama cha Tanu kama ilivyodaiwa?

Post a Comment

0 Comments