Muda mfupi baada ya Rais Julius Nyerere kulitangazia Taifa jijini Dar es Salaam kuhusu uvamizi wa Idi Amin na uamuzi wa Tanzania kumpiga, Alhamisi ya Novemba 2, 1978, alipanda ndege kwenda Beira, Msumbiji kwenye mkutano na mwenyeji wake, Rais Samora Machel.



Ilikuwa aahirishe safari hiyo lakini alilazimika kwenda kwa sababu alikuwa mwenyekiti wa Nchi za Mstari wa Mbele (FLS) katika ukombozi. Nchi nyingine ni Angola, Botswana, Msumbiji, Tanzania, Zambia na Zimbabwe.
Wakati huo pia kulikuwa na mgogoro wa mpaka kati ya Zambia na Zimbabwe (zamani Rhodesia) uliosababishwa na Rais Kenneth Kaunda wa Zambia. Nyerere ndiye aliyekuwa ameitisha mkutano wa kushughulikia mgogoro huo.
Kaunda alikuwa amefungua mpaka wake na Zimbabwe, jambo lililomkera sana Nyerere na Samora.
Nchini Rhodesia, mwanasiasa aliyeitwa Ndabaningi Sithole, ambaye ni mwanzilishi wa chama cha Zimbabwe African National Union (Zanu) kabla ya kuangushwa na Robert Mugabe, alikuwa mshirika wa karibu sana wa Idi Amin.
Kwa hiyo kufunguliwa kwa mpaka huo kulimfadhaisha Mwalimu Nyerere, hasa wakati huo ambao tayari alikuwa na mgogoro na Uganda. Kwa namna fulani Rhodesia ilikuwa na uhusiano wa kijeshi na utawala wa Idi Amin wa Uganda.
Katika ukurasa wa 114 wa kitabu chake cha For the Sake of Argument: Essays and Minority Reports, mwandishi Christopher Hitchens anasema wakati fulani “akiwa ofisini, (Sithole) aliomba msaada wa Idi Amin wa kuunda jeshi lake binafsi”.
Jumatatu ya Julai 17, 1978, ikiwa ni miezi minne kabla ya kuzuka kwa Vita vya Uganda, jarida la Facts and Reports (volume 8), katika habari iliyoandikwa na David Martin iliyokuwa na kichwa kilichosomeka “Sithole Guerrillas Fly to Amin for Training”, kulikuwa na tuhuma za uhusiano huo wa kijeshi.
“Dikteta Idi Amin ameshutumiwa vikali kwa kutoa mafunzo ya kijeshi kwa maelfu ya vijana wa washirika wa Ian Smith (wa Rhodesia) kwa madhumuni ya kuwatumia kuvuruga harakati za ukombozi nchini Zimbabwe,” aliandika mwandishi huyo.
Jarida jingine la International Bulletin (volume 4) la Julai 1978, lilizungumzia suala hilo.
“Mshirika mweusi wa Ian Smith, Mchungaji Ndabaningi Sithole anafundisha jeshi lake binafsi nchini Uganda,” liliandika jarida hilo. Pia, jarida la Africa Research Bulletin’ likaripoti kuwa “Mchungaji Ndabaningi Sithole amepokea idadi kubwa ya wapiganaji kutoka Uganda kwa Idi Amin pamoja na vifaa vya mafunzo”.
Zilikuwapo pia habari kwamba ndege za Rhodesia zilikuwa zikitua katika viwanja vya ndege vya Uganda—Entebbe na Nakosongola.
Habari hizo na nyinginezo za ushirika wa Idi Amin na Sithole, zikijumlishwa na ile ya Zambia kufungua mpaka wake na Rhodesia, zilimfanya Mwalimu Nyerere kwenda Beira, Msumbiji, kujadili jambo hilo haraka kadri ilivyowezekana.
Nyerere na Samora walikutana jioni ya Novemba 2, 1978 kujadili jambo hilo na kuridhika kuwa Idi Amin alitumiwa na mataifa mengine kuivamia Tanzania kwa lengo la kumuondoa Nyerere katika harakati zake za ukombozi wa Zimbabwe dhidi ya akina Ian Smith na mshirika wake, Mchungaji Ndabaningi Sithole, na kwamba huenda Uingereza ilikuwa nyuma ya mpango huo.
Baadhi ya wanazuoni wanaamini kuwa halikuwa jambo la bahati mbaya kwamba vita vya Kagera kuzuka wakati huo muhimu wa mazungumzo kati ya vikosi vya ukombozi na serikali ya wachache ya Ian Smith nchini Zimbabwe.
Walisema wapinzani wa ukombozi walitaka kudhoofisha jitihada za Mwalimu Nyerere “kwa gharama zozote”.
Baada ya kutafakari yote hayo, Nyerere alimhakikishia Samora kwamba Tanzania ingeweza kupambana na Idi Amin bila kupoteza lengo lake la harakati za ukombozi wa Zimbabwe.
Walikubaliana kuwa kikosi cha jeshi la Tanzania kilichokuwa katika mpaka wa Msumbiji na Rhodesia kirejee Tanzania na, zaidi ya hilo, Samora naye akaahidi kutoa kikosi chake kuja kusaidiana na Tanzania.
Ndani ya siku chache, wanajeshi wa Msumbiji wakawa wamewasili Kagera tayari kwa mapigano. Hakuna chombo chochote cha habari cha Tanzania kilichoandika taarifa zozote za wapiganaji wa Msumbiji kuwasili Kagera.
Hata hivyo, kitabu cha War in Uganda cha Tony Avirgan na ‎Martha Honey kinasema “ushahidi mdogo sana kwamba wapiganaji wa Msumbiji walikuwa Tanzania ni nakala ya gazeti Noticias iliyoachwa kwenye ukumbi wa mapumziko wa Uwanja wa Ndege wa Mwanza.”
Waandishi wa kitabu hicho, ambao walikuwa uwanja wa vita, wamesema mbali na wapiganaji hao 800 kutoka Msumbiji, hakukuwa na wapiganaji wengine kutoka taifa jingine lolote duniani waliokuwa wakipigana bega kwa bega na wapiganaji wa Tanzania dhidi ya majeshi ya Idi Amin.
Katika lile juma la pili la Novemba 1978, pamoja na magumu yote waliyokumbana nayo kama mvua, Tanzania iliweza kuwaandaa vyema wapiganaji wake.
Juma hilo ndipo alipowasili Meja Jenerali Tumainieli Kiwelu kuongoza mapambano. Pamoja na kwamba Tanzania ilisikitishwa sana na kuvunjwa kwa daraja la Mto Kagera, ilipata nafasi ya kufanya maandalizi ya kutosha bila hofu ya kuvamiwa na majeshi ya Idi Amin ambayo yangeweza kulitumia daraja hilo kushambulia upande wa pili.

JWTZ waingia Uganda kwa mashua




Usiku wa Jumanne ya kuamkia Novemba 15, 1978, kikosi cha kwanza cha askari wa Tanzania, kikiwa chini ya Luteni Kanali Benjamin Noah Msuya, kilivuka Mto Kagera kwa mashua ndogo na kuingia ng’ambo ya pili.


Hadi kufikia wakati huo (wa kuvuka mto), zaidi ya Watanzania 1,000 walikuwa wameuawa, alisema Msuya katika mahojiano na gazeti The Monitor la Uganda la Jumamosi ya Mei 3, 2014 nyumbani kwake Kunduchi, Dar es Salaam.
Msuya aliongoza batalioni ya 19 ya JWTZ iliyokuwa chini ya Brigedi ya 208 iliyoongozwa na Brigedia Jenerali Mwita Marwa. Kazi yake ilikuwa ni kuivamia na kuitwaa Kampala, lengo ambalo hatimaye lilifikiwa Jumanne ya Aprili 10, 1979.
Baada ya kufanikiwa, Luteni Kanali Msuya akaitawala Kampala kama meya wake na pia kama rais wa Uganda kwa siku tatu hadi nchi hiyo ilipompata Yusuf Kironde Lule kuwa rais.
Alfajiri ya Jumapili ya Novemba 19, Luteni Kanali Msuya alituma kikosi kingine cha askari kwenda ng’ambo ya Mto Kagera, kikitumia mashua nyingine ndogo. Huko walishangazwa sana kuona uporaji na mauaji yaliyofanywa na askari wa Idi Amin.
Miili ya Watanzania waliouawa na majeshi ya uvamizi ilikuwa imeshaanza kuoza. Kikosi hicho kiligundua kuwa miili mingine ilikuwa imekatwa viungo, ishara kwamba wengi wao waliteswa kabla ya kuuawa.
Serikali ya Tanzania ilisema kiasi cha wakazi 40,000 walivuka Mto Kagera kukimbia majeshi ya Uganda, wakiacha kiasi cha raia kati ya 5,000 na 10,000 wakihofiwa kuuawa.
Miongoni mwao, kwa mujibu wa gazeti la Serikali la Daily News, walikuwako Watanzania 485 waliopelekwa gereza la Mutukula upande wa Uganda, ambako waliuawa kwa kulipuliwa kwa baruti.
Habari iliyoandikwa na John Darntonnov kwenye gazeti The New York Times la Alhamisi ya Novemba 23, 1978 inasema katika maeneo yaliyovamiwa na majeshi ya Idi Amin, hasa ya biashara, “kitu pekee chenye uhai kilichoonekana (baada ya uvamizi) ni mbwa mweusi aliyekonda” baada ya raia Watanzania wengi kuyakimbia majeshi ya Idi Amin.
Maduka yote, kwa mujibu wa The New York Times, yaliporwa.
“Katika duka moja lililoporwa, kilichokuwa kimesalia dukani hapo ni picha ya harusi ya mmiliki wa duka, Zaharan Salum na bibi harusi wake, ambayo ilikuwa inaning’inia ukutani,” liliandika gazeti hilo.
Kati ya ng’ombe 12,000 waliokuwa ranchi ya Narco, ni ng’ombe 100 tu walisalia baada ya wengine kuporwa. Wamiliki wa ranchi hiyo, ambao ni raia wa Australia, hawakuonekana baada ya uporaji huo na ilihofiwa kuwa nao waliuawa. Kiwanda ha sukari cha Kagera na shamba la miwa, viliteketezwa.
Doria ya Luteni Kanali Msuya ilifika hadi mpakani mwa Uganda Jumatano ya Novemba 22. Kwa wakati wote huo askari wa Amin hawakuonekana. Lakini doria hiyo ilipofika eneo la Minziro, iliona kiasi cha askari 30 wa Amin na vifaru viwili vikiwa eneo la kanisa. Askari hao wa doria hawakufanya shambulio lolote bali walirudi hadi Kyaka.
Ijumaa ya Novemba 24, vikosi kadhaa vya JWTZ, vikiongozwa na mabrigedia watatu; James Luhanga, Mwita Chacha Marwa na Silas Mayunga vikawa vimetanda kuzingira maeneo yaliyotekwa.
Siku hiyo hiyo daraja la dharura la Mto Kagera likaanza kujengwa kwa ajili ya kuvusha vifaru na zana nyingine za kivita. Kazi hiyo ilikamilika na siku iliyofuata na zana za kivita zikaanza kuvushwa.
Wakati daraja la dharura likijengwa, Rais Nyerere alizuru eneo hilo. Ingawa awali makamanda wa JWTZ walitaka kumzuia. Akiwa uwanja wa vita, alitumia darubini kutazama wapiganaji wa Amin wakiwa vilimani, umbali wa kilometa kumi kutoka mpakani, tayari kuishambulia Tanzania.
Ziara hiyo ya Nyerere ilimshawishi kukubaliana na makamanda wa JWTZ kuwa eneo la Kagera haliko salama na kwamba ili usalama uwepo, ilikuwa ni lazima jeshi la Tanzania livuke mpaka.
Usiku wa Jumapili ya Novemba 21, 1971 askari wa Tanzania walivuka mpaka na kuingia Uganda. Kikosi cha kwanza kilisaidiwa na vifaru na kiliongozwa na Luteni Kanali Salim Hassan Boma.
Vikosi kadhaa vilijizatiti maeneo ya misitu kuzunguka mji wa Mutukula. Kabla ya kupambazuka, kikosi kimojawapo kilichoongozwa na Luteni Kanali Salim Hassan Boma, kikisaidiwa na vifaru, kilitembea katika barabara kuu ya kuelekea Mutukula. Hii ilikuwa ni mbinu ya kuwavuta adui na ilifanikiwa.
Wakati majeshi ya Idi Amin yakifuatilia nyendo za kikosi cha Luteni Kanali Boma kilichokuwa mbele yao, yalishtukiwa yakishambuliwa na kikosi kingine cha JWTZ kutoka nyuma yao. Kwa jinsi askari wa Idi Amin walivyopagawa, walilazimika kukimbia na kutelekeza silaha zao.
Kwa njia hiyo JWTZ ikajipatia silaha mbalimbali kuanzia vifaru hadi bunduki za kawaida. Katika mapambano hayo, kikosi cha Luteni Kanali Boma kilipoteza wanajeshi watatu na wengine kadhaa kujeruhiwa. Hata hivyo, bila ujasiri huo ilikuwa ni vigumu kuvunja ngome ya jeshi la Uganda katika vilima vya eneo hilo.
Kwenye mapigano ya Mutukula, idadi kubwa ya raia waliuawa.
“Kila kitu kiliharibiwa na kila kilichokuwa na uhai kiliuawa,” imeandikwa katika kitabu cha War in Uganda.
“Mabuldoza yalifukia nyumba zote za udongo. Vikongwe ambao hawakuweza kukimbia waliuawa kwa kupigwa risasi. Kufikia mchana (Jumatano ya Novemba 22, 1978) Mutukula haikuwapo tena isipokuwa kwenye ramani.”
Jeshi la Tanzania “lilianza kulipiza kisasi kwa namna isiyotofautiana na ile ya Idi Amin” wakati akiteka eneo la Kagera.
Habari za ushindi wa kuitwaa Kagera zilimfariji Mwalimu Nyerere, lakini inasemekana, hakufurahishwa na habari za mauaji yaliyofanywa na jeshi lake.
Baadaye Nyerere alitoa amri ya maandishi kwa jeshi lake litofautishe jeshi na raia na mali zao. Vyovyote iwavyo, ushindi wa kwanza ukawa umepatikana kwa kuikomboa Mutukula.
Siku JWTZ ilipovuka mpaka, Serikali ya Uganda ilitangaza kuwa wanajeshi zaidi ya 1,000 wa Tanzania wameingia maili 100 ndani ya Uganda na kuteka miji mitatu ya Kyotera, Kakuto na Kalisizo.
Itaendelea