Sarafu ya Kilwa inapotaka kuandika upya historia ya Australia

AUSTRALIA ni eneo pekee duniani lenye sifa zote tatu za kuwa nchi, bara na kisiwa. Ni bara dogo kuliko yote duniani, pia ni kisiwa kikubwa kuliko vyote katika sayari hii na ni nchi ya sita kwa ukubwa duniani.
Kwa mujibu ya sensa ya 2014 iko kusini kwa Indonesia na Magharibi kwa New Zealand. Ikiwa na eneo la 7.682.300 km² na wakazi milioni 23.
Mara nyingi visiwa vya New Zealand huhesabiwa kuwa sehemu ya Bara la Australia.
Aidha, Australia huangaliwa pamoja na visiwa vya Pasifiki katika orodha ya mabara ya dunia kama ‘Australia na Pasifiki.’
Historia inaonesha kuwa Australia ilivumbuliwa na Mwingereza Kapteni James Cook, ambaye ndiye chanzo cha kuitangazia dunia kuwa eneo hilo ni koloni la Uingereza miaka ile na ndiyo huwezi kuitaja nchi hiyo bila Uingereza yenye ushawishi hadi leo hii.
Hata hivyo, ugunduzi mpya umebainisha huenda ukabadili historia, ambayo Waingereza wamekuwa wakijivunia nayo. Kwanini?
Huenda Wareno walikuwa wa kwanza kutua humo kabla ya wengine wa Ulaya, wakiwasili miaka zaidi ya 250 kabla ya Kapteni wao James Cook.
Hiyo ni moja ya nadharia inayofanyiwa kazi sasa na wanasayansi nchini Australia wakati wakiendelea na juhudi za kubaini asili ya sarafu ya Kiafrika, ambayo iliokotwa ufukweni mwaka jana.
Sarafu hiyo ya shaba, ambayo ni moja ya gunduzi kadhaa mpya, inaaminika kuwa ni ya Kilwa, kutoka eneo, ambalo leo hii linajulikana kama Tanzania na inarudi nyuma miaka karibu
Magofu ya Kilwa 1000 iliyopita.
Kwa maana hiyo, zilikuwa sarafu za dola la kisultani la Kilwa, ambalo kwa sasa ni magofu yanayotambulika kama Urithi wa Dunia.
Awali, Kilwa ilikuwa bandari iliyostawi kibiashara ikiunganisha na India katika karne za 13 na 16. Biashara za dhahabu, fedha, marashi, lulu, marumaru kutoka Persia na vyombo vya udongo kutoka China vililifanya jiji hilo moja ya miji maarufu kabisa Afrika Mashariki kipindi hicho.
Lakini namna sarafu hiyo ilivyoishia katika Visiwa Wessel vilivyopo kaskazini mwa Australia, kilomita 10,000 kutoka Tanzania ndiyo kitendawili kinachotafuta mteguzi.
Moja ya maelezo yanayopewa nafasi kubwa, ni kwamba Wareno, ambao waliivamia Kilwa mwaka 1505, huenda waliiacha nyuma sarafu hiyo wakati wa safari yao Kusini Mashariki mwa Asia.
Wasafiri wa Kireno walifika Timor Mashariki mwaka 1515 na kuna uwezekano waliweza kufika nchi kavu Australia.
Iwapo ni kweli hilo litawafanya kuwa kuwa watu wa kwanza wa Ulaya kutua nchi kavu Australia.
Hiyo inamaanisha kuwa wao walikuwa pale miaka 250 kabla ya Kapteni James Cook kuitangazia dunia kuwa eneo hilo ni koloni la Uingereza.
Akizungumza na gazeti la the Guardian, mtaalamu wa mambo ya kale, Mike Hermes anasema: Wareno walikuwa Timor mwaka 1514, 1515 na hivyo kudhani kwamba hawakwenda kwa siku tatu zaidi mashariki kutokana na pepo zenye nguvu za monsoon ni upuuzi.
Kuhusu sarafu anasema: “Tumeipima uzito na kuichambua, inaonekana wazi kuwa kitu kutoka Kilwa, yaani sarafu zilizotumika pale zama zile. Na iwapo ndiyo hivyo, basi hilo litabadili kila kitu kuhusu Australia.”
Hermes aliiokota sarafu hiyo ikiwa ufukweni mwa Visiwa Wessel mwaka jana, akisema haina thamani ya madini ndani ya sarafu hiyo. Hermes anasema visiwa vya Wessel ni mahali pekee nje ya Kilwa na peninsula ya Arabia, ambako sarafu aina hizo zimeonekana.
Hermes alikuwa akijenga rada Maurie Isenberg ya Jeshi la Anga la Australia.
Kwa taarifa huyu Isenberg, ambaye kituo hicho cha rada kimepewa jina lake kwa heshima yake, ni askari wa zamani wa Australia, ambaye pia aliokota eneo hilo sarafu nne za Kilwa mwaka 1944.
Alizitunza sarafu za Kiafrika kwa kuzificha kwa miongo kadhaa hadi mwishowe aliamua kuzitoa makumbusho ya Sydney mwaka 1983.
Sarafu hizo zilisababisha minong’ono iwapo Wareno walikuwa wakoloni wa kwanza wa Ulaya kutua Australia.
Ilikuwa ikidhaniwa kwamba wafanyabiashara wa Kilwa wangeweza kuleta sarafu kutoka Ulaya wenyewe, au ikatiokea vinginevyo.
Sarafu hizo pia zinaweza pengine zilisombwa hadi ufukweni kutoka mahali kwingine.
Watafiti wanasema kwamba njia ya baharini kutoka Kilwa mashariki mwa Afrika hadi Oman na kisha India, Malaysia na Indonesia ilikuwa imeshaanzishwa kufikia miaka ya 1500.
Mwaka 2013, Professa Ian McIntosh alisema sanaa kwenye miamba ziligunduliwa katika Visiwa vya Wessel, pamoja na taswira moja inayoonesha chombo cha kusafiria majini cha Ulaya.
Mwongozaji wa baharini wa Kifaransa, Binot Paulmier de Gonneville alidai kutua mashariki mwa Cape of Good Hope’ mwaka 1504, baada ya kusombwa na upepo.
Lakini mahali hapo alipofukulia, ambapo baadhi waliamini ni Australia, pamethibitika kuwa ni Brazil.
Mwingereza wa kwanza anayefahamika kutua nchi kavu Australia alikuwa William Dampier, haramia wa zamani.
Alifika pwani ya kaskazini magharibi karibu na King Sound, Januari 1688 baada ya meli yake ndogo ya biashara- the Cygnet, kutia nanga hapo.
Hata hivyo, ilifahamika baadaye mtu wa kwanza wa Ulaya anayefahamika kutua Australia alikuwa msafiri Mholanzi Willem Janszoon mwaka 1606.
Waholanzi wengine walisafiri pwani za magharibi na kusini katika karne ya 17, wakiliita bara hilo ‘Uholanzi Mpya.’
Lakini alikuwa Kapteni James Cook aliyekuwa wa kwanza kuitangazia dunia baada ya kufika Botany Bay, Sydney mwaka 1770 na kuweka dai la Uingereza katika bara hilo.
Watu wa asili wa Aboriginal wa Australia, ambao ni wakazi wa kwanza kuishi eneo hilo, wanadhaniwa waliwasili mara ya kwanza Australian kwa boti kutoka Kisiwa Malay kati ya miaka 40,000 na 60,000 iliyopita.
Kisha koloni la Uingereza kwa mara ya kwanza likaanzishwa Botany Bay Januari 1788, ikiwa ni matokeo ya ugunduzi wa Kapteni Cook.
Wakati wa karne iliyofuata, Waingereza walianzisa makoloni mengine katika bara hilo na wafungwa kutoka Uingereza walipelekwa hapa katika karne ya 19. Baadaye walifika pia walowezi huru.
Idadi ya Waustralia asilia imepungua sana kutokana na magonjwa mapya wakiambukizwa na Wazungu, pia walitendewa vibaya na kufukuzwa katika sehemu kubwa ya nchi yao.
Australia ilipata uhuru wake mwaka 1901 lakini inaendelea kumkubali Malkia ya Uingereza kama Mkuu wa Dola akiwasilishwa na Gavana Mkuu. Mamlaka imo mikononi mwa waziri mkuu na serikali yake.

Post a Comment

0 Comments