Kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali vya habari, Bibi Titi alikuwa mmoja wa wananchi walioonekana katika mapambano ya kudai uhuru wa Tanganyika miaka ya 1950.
Bibi Titi alipewa kitengo cha wanawake ndani ya TANU ambapo baada ya miezi mitatu ya uteuzi huo aliweza kuwashawishi maelfu ya wanawake kujiunga na chama hicho katika utawala wa Rais wa kwanza nchini mwalimu Julius Nyerere 1954.
Kuzaliwa kwa UWT
Historia ya Umoja wa wanawake (UWT) haiwezi kutenganishwa na historia ya mapambano ya Ukombozi wa Tanganyika na Zanzibar ambapo kitengo cha wanawake ndani ya TANU kiliundwa mwaka 1955, chini ya Uongozi wa Bibi Titi Mohamed.
Kuwapo kwa chama cha TANU ni matokeo ya kuvunjwa kwa Tanganyika African Association (TAA) na kwa upande wa Zanzibar, kuvunjwa kwa Afro Shirazi Party ni muunganiko wa vyama viwili African Association (AA) na Shirazi Association (SA).
Madhumuni ya TANU yalikuwa ni kung’oa ukoloni wa Kiingereza ndani ya Tanganyika wakati madhumuni ya ASP yalikuwa ni kung’oa Usultani wa Kiarabu na Ukoloni wa Kiingereza Zanzibar.
Nafasi ya UWT kudai uhuru
Umoja wa Wanawake wa Tanganyika (UWT) kama ilivyokuwa kwa Jumuiya za Umoja wa Vijana na Wazazi, ulifanya kazi kubwa ya kueneza na kuimarisha TANU.
Baada ya  kuundwa TANU, ilianzishwa kitengo cha  wanawake katika TANU kwa ajili ya  kupambana na ukoloni.
Umoja huo ulikusanya wanawake wanyonge wa mijini na vijijini ili washirikiane na wanaume katika harakati za kudai Uhuru.

Mchango wa Wanawake katika Mapambano ya Uhuru
Sehemu ya Katiba ya kwanza ya TANU (1964) ilitambua nafasi ya wanawake, “Kutakuwa na upande wa wanawake katika Chama, Mwanamke akishaingia katika Chama atakuwa mwanachama, kila tawi la Chama litakuwa na upande wa wanawake na litakuwa katika Chama chini ya Uongozi wa Halmashauri ya Tawi.  Wanachama wanawake na wanaume wote watakuwa sawa”.
Majukumu ya kitengo cha wanawake
Majukumu ya kitengo cha wanawake yalikuwa ni pamoja na, kuhamasisha wanawake kujiunga na TANU,  Kueneza TANU mijini na vijijini kwa kujitolea.

Kulinda viongozi wa TANU  Katika hali ya kulinda Chama dhidi ya maadui pamoja na kuimarisha TANU kifedha kupitia shughuli halali mbalimbali ikiwa ni pamoja na dansi, kuendeleza wanachama wanawake kijamii na kiuchumi.

Uchaguzi UWT
Umoja wa Wanawake wa Tanganyika (UWT) uliundwa na TANU Novemba 2, 1962 ambapo  katika mkutano wa uchaguzi wa viongozi Novemba 7 hadi 10, 1962 Bibi Titi alichaguliwa kuwa mwenyekiti, Kanasia Mtenga (Makamu mwenyekiti), huku rais wa TANU Mwalimu Nyerere akichaguliwa kuwa Mlezi wa UWT.

Kwa nini TANU iliunda UWT
TANU iliunda UWT kama ishara ya kutambua mchango waliotoa wanawake katika mapambano ya kudai uhuru, kuwawezesha wanawake kuwa na chombo chao cha kuendeleza ukombozi wao.

Sababu nyingine ni kuondoa vyama mbalimbali vya wanawake na Baraza la Wanawake wa Tanganyika ambalo lilikuwa linapingana na sehemu ya wanawake katika TANU.

Harakati za Bibi Titi
Wakati Tanganyika ikipata uhuru wake na hata baada ya tukio hilo, Bibi Titi alikuwa mmoja wa wanachama wa TANU waliopewa nafasi ya kuzungumza mambo mbalimbali jukwaani kabla ya kuzungumza Mwalimu Nyerere.
Mwaka 1969 Bibi Titi alikamatwa na mwaka uliofuata alifikishwa mahakamani kwa kosa la kula njama ya kutaka kupindua serikali ya Mwalimu Nyerere.
Katika kesi hiyo, Bibi Titi alikuwa ni mwanamke pekee katika washtakiwa 7. Baada ya kesi kusikilizwa alipatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo cha maisha.
Hata hivyo, mwaka 1972 alisamehewa na rais  Nyerere ambapo baada ya kutoka jela Bibi Titi aliendelea na harakati zake huku akiwa na maisha ya upweke baada ya kutelekezwa na mume wake wakati kesi hiyo ikisikilizwa.

Ushiriki wake katika siasa ulishuka na kukimbiwa na watu wake wa karibu.
Mwaka 1991 wakati Tanzania ikisherekea miaka 30 ya uhuru, Bibi Titi alionekana  kwenye mabango ya Chama cha Mapinduzi (CCM) kama mwanamke shujaa aliyepigania uhuru.Bibi Titi alifariki dunia katika  hospitali ya Net Care, Afrika Kusini alikokuwa akitibiwa.
Kumbukumbu
Kutokana na mchango wake kabla na baada ya Tanganyika kupata uhuru moja ya barabara za jiji la Dar es Salaam ilipewa jina lake.