Image result for utumwa


INGAWA utumwa ulimalizika rasmi mwaka 1919 katika Tanganyika (Tanzania Bara) na mwaka 1904 kwa Kenya, upande wa Zanzibar, ulichukua muda mrefu ingawa kisheria ulipigwa marufuku 1873.
Pamoja na ukweli huo, ishara za kufadhaisha binadamu zipo wazi katika maeneo kadhaa ya Zanzibar huku Mangapwani kukiongoza kwa fadhaa za kawaida. Wanazuoni pamoja na kuendelea kubishana kuhusu njia zilizotumika kuficha, kuhifadhi na kusafirisha binadamu kama wanyama baada ya marufuku ya mwaka 1873, ipo njia rahisi ya kutafakari mambo haya.
Nilitembelea Zanzibar na kufika katika eneo ambalo lina maswali na majibu yasiyofurahisha au kuthibitisha juu ya simulizi kwamba hapakuwapo utumwa wenye adha katika eneo la Mangapwani. Ni rahisi kujifunza dhiki na adha ya utumwa kwa kuangalia mapango na maeneo ya hifadhi ya watumwa yaliyokuwapo Zanzibar katika maeneo ya Mangapwani yaliyopo kilometa 25, Kaskazini mwa mji wa Zanzibar. Zipo ishara mbili kubwa ambazo ukizitembelea unasisimka kutokana na mazingira yaliyopo.
Ishara hizo ni pango la Mangapwani ambalo lilikuwa linatumika kusafirisha watumwa na makazi yaliyowahifadhi ambayo yalikuwa na vyumba viwili katika mstatili. Mangapwani ambayo maana yake ni ‘ufukwe wa Kiarabu’, una simulizi zinazokinaisha moyo japo wanazuoni wanasema hakuna kitu chochote kinachoonesha kwamba kulikuwa na mlundikano mkubwa wa watumwa wakisubiri kusafirishwa.
Ikumbukwe kwamba baada ya mapinduzi ya viwanda na uchumi wa dunia kukua, Ulaya ilipiga marufuku biashara ya utumwa. Manowari za Kiingereza zilifanya doria hali iliyofanya wafanyabiashara ya utumwa kubuni njia ya kusafirisha watumwa wao kiusalama zaidi, bila kuacha ishara nyuma yake. Mwaka 1873 Sultan Barghash alilazimika kuzuia utumwa baada ya tishio la kupigwa mizinga na Waingereza na huku akilazimishwa tena mwaka 1887 kuumaliza utumwa kisheria Zanzibar.
Hata hivyo, uliendelea kwa staili ya kutumiwa kwa mapango hayo na maeneo hayo ya hifadhi ambayo ni mawili yaliyokatwa katika mwamba na katika kila hifadhi, inaonekana walikuwapo watumwa 50. Inaelezwa kuwa pango la Mangapwani ni la asili na kwamba lilitumika kuficha watumwa katika raundi ya pili ya usafirishaji ukitoka katika eneo la hifadhi . Binadamu walisafirishwa usiku na waliwekwa katika majahazi usiku kukwepa kukamatwa na doria za Kiingereza.
Simulizi zinasema kwamba kabla ya kupita katika njia hiyo ya pango la asili, watumwa waliofikishwa katika pwani hiyo, walihifadhiwa katika jengo lililojengwa kwa kutumia mawe yaliyokatwa katika mwamba huku likiwa na mlango mdogo sana wa kuingilia. Pango hili lilimilikiwa na Mwarabu aliyejulikana kwa jina la Hamed Salim el Hathy ambaye alimiliki watumwa wengi zaidi wakati wa biashara ya utumwa Visiwani Zanzibar.
Sehemu ya kuhifadhia watumwa ya Mangapwani ipo kilometa kadhaa kutoka kwenye mwamba wa Bahari ya Hindi . Ndiyo maana wakati mwingine, eneo hilo linatajwa kwa jina la Pango la watumwa. Hili ni eneo lilojengwa juu ya mwamba huku likiwa na paa kwa juu . Inaelezwa kwamba, ujenzi wa eneo hilo ulibuniwa na Mohammed bin Nassor Al-Alwi. Pango hilo lilijengwa baada ya mwaka 1873, wakati Sultan Barghash alipotia saini mkataba wa usitishwaji wa biashara ya watumwa wa Anglo–Zanzibar .
Ukitazama mandhari unajua kwamba kulikuwa na mateso makubwa ya kifizikia na kisaikolojia wakati watu hawa wanasubiri kusafirishwa kwenda wasikokujua. Eneo la kuhifadhia watumwa ndilo linalosikitisha sana ingawa lipo kiasi cha kilometa mbili kutoka katika eneo ambalo watumwa walikuwa wakiingizwa pangoni na kusafiri katika pango kuelekea ughaibuni. Kuna maelezo mengi kuhusiana na eneo hilo ambayo hayako wazi moja kwa moja.
Watafiti wa masuala ya utumwa hawajaweka wazi kuhusiana na fasihi ya eneo hilo ambalo inaaminika lilijengwa na kutumika kati ya mwaka 1880 hadi 1905. Eneo la kuhifadhia pamoja na udogo wake linaonesha ni kwa namna gani utu wa mwanadamu ulidhalilika ingawa wanapofika katika pango la njia ya usafirishaji walikuwa wanakutana na kisima cha maji baridi na huenda walikuwa ndiko wanakopata uhakika wa maji kama watu walikuwa na utu.
Pamoja na kuwapo kwa pango hilo ambalo siku hizi hufanyika matambiko, Mangapwani ni sehemu ambayo inastahili kufanyiwa kazi na kuandikwa ili mabaki yake yaweze kuendelea kuonesha binadamu alivyodhalilika. Ukitazama maandishi ya kawaida wapo watu wanaopinga kwamba pango hili lilitumika kusafirishia watumwa, lakini kiukweli umbali na mfumo wa uoto wa eneo unaonesha kwamba watumwa zaidi ya 100 waliokuwa wakihifadhiwa katika nyumba za ardhini walikuwa wanasafirishwa kupitia njia hii ya pango.
Ingawa ni kazi kupita katika pango hili kuelekea baharini, muundo wa pango uliosheheni mwamba wa chokaa unaruhusu maji ya bahari mpaka eneo linalotoa taswira ya mwizi anavyojaribu kujificha asionwe na mpiga doria. Tarehe za ujenzi wa chumba cha kuhifadhia watumwa na doria iliyokuwa ikifanywa na Waingereza katika pwani ya Zanzibar kabla ya Sultani kulazimishwa kusaini mkataba wa kuondokana na biashara ya watumwa, unaonesha wazi jinsi ambavyo simulizi za kitumwa katika pwani ya Afrika Mashariki zinavyoweza kusahaulika kwa haraka zaidi.
Ni simulizi za Afrika Magharibi ambazo zipo hai labda kutokana na wengi wa watu walioishia ng’ambo ya pili ya Atlantiki kupata nafasi ya kuzaliana na kuongezeka wakati walioishia Mashariki ya Mbali na Kati wakiwa hawana uwezo wa kuongezeka. Inaaminika kwamba, Mohammed bin Nassor Al-Alwi, mfanyabiashara tajiri wa watumwa alikuwa na uwezo wa kuingiza majahazi ya watumwa kutoka Bagamoyo na kuwatenganisha kabla ya kuanza kuwasafirisha kwenda maeneo mbalimbali ya Mashariki ya Kati na Mbali.
Mpaka sasa wataalamu wanaonesha njia iliyofifia inayoonesha kutoka katika vyumba vya kuhifadhia watumwa kwenda katika pango la kuwasafirishia, pango ambalo siku hizi pia watu wanalitumia kufanyia matambiko. Katika maelezo kwenye baadhi ya saiti katika mtandao zinasema kwamba Mohammed bin Nassor aliwaweka watumwa wake katika majumba hayo kwa madai kwamba, alikuwa akiwanenepesha au kuwafanya wapumzike kidogo.
Lengo la kufanya hivyo, inadaiwa ilikuwa ni kulenga kuwauza kwa bei nzuri ama katika soko la watumwa Zanzibar kabla ya marufuku na baadaye kulazimika kuwahifadhi kuendelea na biashara haramu kwa muda mrefu.
Hata hivyo, Waingereza kupitia Mkataba wa Moresby wa mwaka 1822, walimbana Sultani dhidi ya kupeleka watumwa kwenye makoloni yaliyofuata Ukristo zaidi. Bado biashara ya utumwa iliendelea kushika kasi na kushamiri hadi miaka ya 1840. Kwa namna yoyote, pamoja na simulizi mbalimbali zinazogongana juu ya pango la Mangapwani, haiondoi ukweli kwamba dhambi kubwa ilifanyika dhidi ya binadamu katika eneo hilo na wote walioumizwa, wasisahaulike .