Fuvu la Zinjanthopus hadharani baada ya miaka 60 kufichwa



Arusha. Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, mwaka huu inaadhimisha miaka 60, tangu kuvumbuliwa fuvu la binaadamu wa kale duniani la Zinjanthropus na kwa mara ya kwanza, tangu kuvumbuliwa mwaka 1959.
Fuvu hilo litakuwa hadharani kuanzia Julai 17, mwaka huu.
Fuvu hilo liligunduliwa katika Bonde la Oldupai ni maarufu duniani kutokana na kufahamika kwake kama chimbuko la binadamu wa kale na historia na umaarufu wa bonde hili unafuatia uvumbuzi wa visukuku vya zamadamu uliofanywa na watafiti Dk Louis Leakey na mkewe Dk Mary Leakey.
 Fuvu hilo la Zinjanthropus lilivumbuliwa kwenye bonde hili pamoja na visukuku vingi vya wanyama wa kale na masalia mengi ya zana za mawe katika bonde hilo  lililo ndani ya hifadhi ya Ngorongoro, mashariki mwa mbuga za Taifa za Serengeti.
Akizungumza katika uzinduzi wa miaka 60 ya makumbusho ya Olduvai leo Jumapili Juni 9,2019, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla amesema Watanzania kwa mara ya kwanza wataliona fuvu hilo ambalo lilikuwa limehifadhiwa sehemu maalum na serikali.
"kwa siku tano kuanzia Julai 17, fuvu litakuwa eneo la makumbusho ya Olduvai hivyo, ni fursa kwa watanzania kutembelea eneo hili kuona historia ya binaadamu na mamlaka ya hifadhi ya ngorongoro imeandaa usafiri kutokea Karatu"amesema
Kamishna Mkuu wa uhifadhi wa Mamlaka ya hifadhi ya Ngorongoro, Dk Freddy Manongi amesema maadhimisho hayo ni fursa kwa watanzania kutembelea ngorongoro na kujua vivutio vilivyopo katika hifadhi hiyo.
Anasema maadhimisho hayo pia yatakutanisha wanasayansi kutoka maeneo mbali mbali duniani, ambao watakutana Arusha na baadaye kutembelea eneo la kihistoria ya Olduvai.
"Tunawakaribisha watanzania Ngorongoro, kutakuwa na usafiri kutoka Karatu, kila siku za kurudi kuanzia julai 17 na tunaimani kampuni za utalii na wadau wengine watajitokeza kusafirisha watalii"amesema
Tangu utafiti wa mambo ya kale uanze kwenye bonde hili  karne iliyopita, ilidhibitika kwamba teknolojia ya mwanzo kabisa duniani ilianzia hapo kutokana na ushahidi wa zana za mawe za muhula wa kwanza.  Ushahidi wa akiolojia na visukuku unaonyesha mabadiliko ya viumbe asilia na maendeleo ya utamaduni wa binadamu wa kale katika nyakati tofauti.

Post a Comment

0 Comments