Wakati watu wakihojiwa na kuteswa bara, huko Zanzibar mambo yalikwishatayarishwa kwa ajili ya kesi ya kimaonyesho ya wafuasi wa siasa za mrengo wa kushoto iliyokuwa iendeshwe katika mahakama ya wananchi. Miezi michache kabla ya kesi hiyo vyombo vya habari na wananchi walitayarishwa kwa ajili ya kesi hiyo. Mkutano mkuu wa kwanza wa Chama cha ASP katika kipindi cha miaka kumi, uliofanyika mwezi Disemba 1972 chini ya uongozi wa Jumbe ulitamka kuwa itakuwa ndiyo kesi. Mbele ya Nyerere na viongozi wengine wa TANU waliokuwepo, yalipitishwa maazimio manne, kila azimio likithibitisha ajenda ya kibaguzi ya kikabila ya wafuasi wa siasa za mrengo wa kulia yenye nia ya kulipiza kisasi. Maazimio mawili ya kwanza yalieleza kuwa wale wote waliokuwa wanachama wa vyama vya ZNP, ZPPP na Chama cha Umma Party watapigwa marufuku kushika nafasi yoyote katika serikali ya visiwani au kuwa wanachama kamili wa Chama cha ASP. Azimio la tatu liliwapiga marufuku wale wasiokuwa wanachama wa Chama cha ASP kufanyakazi katika polisi na jeshi, na la mwisho lilitaka iendeshwe kesi na kuuliwa hadharani wote wale watakaopatikana na hatia katika kile kinachotuhumiwa kuwa ni njama dhidi ya Karume:
Kesi
Kesi yenyewe hasa ilianza tarehe 5 Mei, 1973 takriban mwaka mmoja baada ya kamatakamata za kiholela. Miongoni mwa wale walioshitakiwa, 81 walishitakiwa kwa kosa la uhaini wakiwa ni pamoja na 18 waliowekwa kizuizini bara. Wakati Jumbe alijaribu kutaka 18 hawa, pamoja na Babu, warudishwe Zanzibar, Nyerere aliendelea kukataa kufanya hivyo labda kwasababu alihisi kuwa kufanya hivyo kungelizusha lawama na hasira za kimataifa. Matokeo yake, watu hawa walishitakiwa wakiwa wenyewe hawapo. Nyerere hakufanya lolote lile kuzuia kile ambacho kilikuwa sio tu kitendo cha ukiukwaji mkubwa wa haki bali pia ni kitendo batili kwasababu, kwa mujibu wa sheria za Tanzania kesi za kumuhukumu mtu wakati mwenyewe akiwa hayupo haziruhusiwi na pia kwasababu kumuhukumu mtu wakati mwenyewe akiwa hayupo kunaleta dhana kuwa mtu huyo amekataa kufika mahakamani.
Kitendo cha Nyerere cha kuchukua au kutochukua hatua kuhusu suala hili na kushindwa kwake kuwasimamia watu wasiokuwa na hatia kama ilivyokuwa katika mahusiano yake na Uingereza na Marekani kabla ya Muungano, kunaonyesha dhahiri hali yake ya kukosa ujasiri na kutokuwa na uwezo wa kuwa na msimamo thabiti dhidi ya shinikizo la wafuasi wa siasa za mrengo wa kulia.
Kesi ilifanyika katika Mahakama za Wananchi za Zanzibar, Khamis anakumbuka:
Jaji alikuwa muuza samaki. Hakujua sheria. Hapo mahakamani akitwambia, ‘Nyinyi ni kama samaki ndani ya kikapu changu, naweza kumchukua nimtakaye na kumwacha nisiyemtaka.’ Hayo akiyasema mahakamani! Hao ndio majaji wa wananchi – walitakiwa wayaangalie mambo kwa mtazamo wa Afro-Shirazi. (Mahojiano na Khamis Ameir, 2009)
Kwa wale walioshitakiwa wakiwa wenyewe hawapo, kesi hiyo ilikuwa ni zoezi la kuwapaka matope kwa kutumia hadithi za kubuni zilizorudiwa mara kwa mara. Kesi ilichukua takriban mwaka mmoja na kuchapishwa takriban katika magazeti yote nchini. Kama Babu alivyomwandikia mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa.
Wakati tukiwa tumenyimwa haki ya kujitetea, au hata kuwepo katika kesi … majina yetu yalipakwa matope na kukashifiwa hadharani, tukiitwa kila aina ya majina ambayo kinywa kichafu cha mwendesha mashtaka kiliweza kuyatema na wakati wote huo tukiwa tumenyamazishwa nyuma ya kuta za gereza. (Babu, 1975: 5)
Familia za washtakiwa tayari zilikuwa zikiteseka sana. Katika kila hali zilikumbana na shida za kiuchumi wakati watafutaji wao wa riziki wakiwa wamefungwa gerezani. Sasa, wakati kesi ikijikongoja, familia hizo ziliendelea kuishi katika hali ya uonevu na kupata maumivu ya ziada.
‘Ushahidi’ ambao Wolfgang Dourado, mwendesha mashtaka, aliuwasilisha dhidi ya washtakiwa unajieleza wenyewe. Ulikuwa ni ushahidi wa maelezo ya watu tisa waliokiri kosa na kuhukumiwa kifo na wakisubiri matokeo ya ombi la msamaha. Watu hawa waliambiwa kuwa kukiri kosa kutawahakikishia hukumu yenye tahafifu, ijapokuwa hilo lilidhihirika kuwa ni uongo. Maelezo yao yaliwataja washitakiwa wote isipokuwa sita tu. Zaidi ya maelezo hayo yalikuwepo maelezo ya wale waliokiri wenyewe ambayo yote yalikanwa na washitakiwa wote waliokamatwa visiwani na sita wengine ambao hawakutolewa ushahidi wowote. Katika kila hali, ‘ushahidi’ huu ulipatikana kwa njia za utesaji.
‘Ushahidi’ mwengine uliochukuliwa ulihusu mahusiano binafsi na ya kisiasa kati ya washtakiwa na Babu, uhusiano ambao hawakuukana. Mwisho ulikuwepo ushahidi usio na ithibati kuhusu mahali Babu na washitakiwa wengine walipokuwepo wakati wa mauaji:
[Kwa] kuyakubali maelezo ya watu hao tisa na maelezo mengine ya kukiri yaliyotolewa na washtakiwa wengine wote, upande wa mashtaka uliweza kuthibitisha tu yale yanayojulikana vizuri na yeyote yule anaeyajua kwa juu juu mambo ya Tanzania/Zanzibar, kuwa Babu alikuwa ni mpinzani mkubwa wa namna ASP ilivyokuwa ikiitawala Zanzibar, kuwa yeye na washtakiwa wengine wengi walikuwa ni wakomunisti wanaojitangaza wenyewe na kuwa wote walikuwa wakikutana mara kwa mara kwenye mikusanyiko ya kiburudani. (Chase, 1976: 25)
Khamis aliniambia kuwa aliulizwa na Mwendesha Mashtaka Dourado “Unajua kuwa Marx alisema kwamba dini ni kasumba kwa watu?” Nilimwuliza, “Kwani mimi ninashtakiwa kwa kuwa mfuasi wa Marx au kwa mauaji ya rais?” Dourado alitaka kuwafurahisha Wamarekani.
Ama kwa Babu, mawazo yake ya kikomunisti ndiyo yaliyoitawala kesi yote. Alilaaniwa katika maelezo ya Dourado na kuitwa shetani mwenye umbo la binadamu. Kwa mfano, Dourado alieleza:
Ili kuyaelewa vizuri mazingira ya upande wa mashtaka ni vizuri kuielewa tabia ya adui wa mchezo wote, Abdulrahman Mohamed Babu. Kama inavyotuhumiwa na upande wa mashtaka, yeye amekuwa ndiye kiongozi wa mpango huu … yeye ndiye aliyeuzaa mpango huu wa kuipindua serikali ya Chama cha Afro-Shirazi tokea mwaka 1968. Alikuwa ndiye mbunifu mkuu na mchochezi mkubwa wa mpango huu.… Babu na makomred wenzake wanataka kuanzisha sera gani Zanzibar? Uzito wote wa ushahidi unaonyesha kuwa walitaka kuanzisha usoshalisti wa kisayansi. Mashahidi kama Miraji Mpatani, Qullatein Badawi na mshtakiwa mwenza Ali Sultan (anayeonekana kuzielewa siasa zao) walieleza kuwa usoshalisti wa kisayansi ni ukomunisti … Kama kuna mtu anayemwelewa Babu basi yeye si mtu anayeweza kuheshimu matakwa ya umma. Akiwa kiongozi wa Chama cha Umma Party, alizungumzia juu ya chama ‘Kiongozi’. Hii ina maana kuwa kikundi cha madhalimu kujifanya kuwa ni masoshalisti wa kisayansi kulazimisha matakwa yao kwa umma. (Chase, 1976: 25 -7)
Ukiacha mbali mazingira yaliyoshitadi ya kupinga ukomunisti yaliyoizunguka kesi hiyo, kesi hiyo ilikuwa imejaa mambo ya kipuuzi yasiyokuwa na mantiki. Hatimaye, Dourado aliiomba mahakama iamini hadithi ya kuchekesha ambayo hata mpumbavu wa namna gani angeliona shida kukubali.
[Kuwa huo unaoitwa mpango] ulioasisiwa na mmoja wa viongozi wakuu wa kisiasa wa mapinduzi ya 1964 (Babu) ukijumuisha viongozi wa kijeshi wa mapinduzi ya kutumia silaha ya 1964, pamoja na Mkuu wa Uendeshaji wa Jeshi la Tanzania (Mahfoudh) na kuandaliwa kwa makini katika kipindi cha zaidi ya miaka minne ulikuwa ni kumpeleka mtu mmoja, (Ahmada) kuiteka kambi ya Bavuai, Makao Makuu ya Jeshi na Chuo cha Radio cha Jeshi, mtu mmoja (Dugheshi) kumkamata Karume, kumpeleka kwenye stesheni ya radio na … [ baadae] … Kuiteka Ikulu … Mtu mmoja (Baramia) kuyadhibiti Makao Makuu ya Umoja wa Vijana, ambayo ni kituo kilichokuwa cha kijeshi chini ya kiongozi mkuu wa usalama wa ndani wa Karume, Seif Bakari, na bila shaka kuwepo mtu mmoja wa akiba (Ameir) ili kushughulikia shambulizi lolote la upinzani … washitakiwa wengi ambao walituhumiwa kupangiwa majukumu ya kijeshi hawakuwa wanajeshi katika jeshi la Zanzibar. (Chase, 1976: 29)
Kwa majaji, uongo huu wa kipuuzi ulitosha. Katika watu 18 waliowekwa kizuizini bara 14 walipatikana na hatia na halikadhalika 40 wengine waliokuwa kizuizini Zanzibar. Adhabu za kifo zilitolewa bila ya kizuizi.
Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binadamu Amnesty International lililofanya kampeni kubwa ya kutaka waliokuwa kizuizini waachiliwe- likimchukua Babu na kumfanya kuwa ni mfungwa wa kifikra – lilielezea katika waraka wake juu ya adhabu ya kifo Tanzania (ambao ulishughulikia kipindi cha 1973-76, ijapokuwa uligusia vile vile mwaka 1977) kuwa kwa jumla:
Adhabu za kifo 42 zilitolewa na Mahakama ya Wananchi. Kumi na tatu ya hukumu hizo zilitolewa wenyewe wakiwa hawapo, kwa watu ambao waliowekwa kizuizini bara lakini hawakukabidhiwa kwa serikali ya Zanzibar ikitiliwa maanani kuwa washtakiwa hao wasingelifanyiwa kesi ya haki. (Amnesty International, 1979: 1)
Hamed aliniambia kuwa:
Mwezi mmoja baada ya kesi iliyofanyika katika mahakama ya bandia nchini Zanzibar kumalizika na hukumu kutolewa, tulihamishiwa katika magereza mengine. Baadhi yetu, Salim Saleh, Shaaban na Badru Said, Haji Othman na mimi mwenyewe, tulihamishiwa Dodoma; Ahmed Tony na Tahir Ali walipelekwa Tabora na Amour Dugheish na Abdalla Juma walipelekwa Mbeya; Suleiman Sisi alipelekwa Mwanza na Hashil alipelekwa Tanga. Babu na Ali Mahfoudh walibakia Ukonga kwa muda wote. Ali Yusuf aliachiliwa miezi michache baada ya kesi. (Mahojiano na Hamed Hilal, 2011)
Miaka Mingi Gerezani
Makada wa Chama cha Umma Party sasa walionekana kukabiliwa na hukumu isiyokuwa na kikomo. Wafungwa, hasa wale waliokuwepo Zanzibar waliteswa kwa namna mbalimbali. Kwa mfano, chakula walichopewa, si kama kilikuwa kibaya sana tu lakini pia kilichafuliwa makusudi kwa kiasi kidogo cha sumu. Muhogo ulichemshwa katika chombo kilichotumiwa kwa kuwekewa mafuta ya disel na kuwachwa humo kabla ya kugawiwa. Baadhi ya wakati ulikuwa na majani ya muhogo ya sumu au huwepo uji uliopikwa kwa mahindi yaliyooza na maharagwe yenye funza. Hali ya mazingira ilikuwa ya kutisha: Chumbani mlikuwemo na tundu ndogo iliyotumiwa kuwa choo na watu wanane au tisa. ‘Baadhi ya makomred wenzetu walikufa; Khamis aliniambia kuwa ‘kwasababu ya kutokuwepo kwa matibabu ya vidonda vilivyosababishwa na mateso au kwa ugonjwa wa kuharisha … tuligoma kula na hatimaye waliwaruhusu jamaa zetu kutuletea sabuni, dawa za meno na chakula kizuri.’ Siku hizi za baada ya kesi ziliathiri vibaya sana familia na wapendwa wa makada wa kile kilichokuwa Chama cha Umma. ‘Familia zetu nyingi zilisambaratika; Khamis aliniambia. Mtoto wake alipelekwa gerezani wakati yeye mwenyewe akiwemo humo:
Mtoto wangu alikuwa na umri wa miaka 17, mama yake hakuweza kumdhibiti. Walimtia gerezani pamoja na vijana wengine wengi. Tulikuwa tukigawana nao chakula chetu. Baadae ilikatazwa kufanya hivyo. Baadae mtoto wangu aliachiliwa. Alipelekwa katika skuli ya watoto wahalifu ambayo ilianzishwa na serikali. Alikuwemo humo kwa takriban miaka miwili. Nilipotoka jela na yeye alikuwa nje pia. Alikwenda Burundi na mara baada ya hapo alifariki kwa kuaaligongwa na basi Dar es Salaam. Nilikwenda kuichukua maiti yake kutoka katika chumba cha kuhifadhia maiti … Yote haya yalikuwa ni matokeo ya vitendo vya dhahiri au visivyo vya dhahiri vya serikali. Inawezekana kuwa mpango uliokuwepo ni kuwa sisi tufie gerezani. Walikwenda kwa wake zetu na kuwambia, ‘Nenda kwa mume wako aliye gerezani na mwambie kuwa unataka talaka yako. Yeye hatoki.’ Ilikuwa kama kazi waliowapa – ilikubidi utie saini barua ya kutoa talaka. (Mahojiano na Khamis, 2009)
Kwa kuchanganyika na wafungwa wengine waliwaona watu wengi walioathiriwa na ukandamizaji bila ya kujali wa serikali ya Tanzania. Khamis aliniambia.
Tulikuwa na kijana kutoka Malawi. Walimkamata kwasababu yeye alikuwa ni Mngazija tu. Alikuwa gerezani kwa muda mrefu pamoja na mimi. Baadhi ya wakati watu walikamatwa kwasababu ya chuki tu. Baadhi ya wakati kwasababu za kiitikadi na baadhi ya wakati kwa hisia tu. (Mahojiano na Khamis, 2009)
Bara, Babu na makomred wenzake walikutana na makundi ya wapigania uhuru kutoka katika Chama cha Kupigania Uhuru cha Msumbiji, FRELIMO, Chama cha Kupigania Uhuru cha Angola (MPLA), Chama cha Kupigania Uhuru cha Zimbabwe (ZAPU), Vyama vya Kupigania Uhuru wa Afrika ya Kusini vya ANC na PAC na Chama cha Kupigania Uhuru cha Kusini Magharibi ya Afrika (SWAPO), wafuasi wa Lumumba na Mulele kutoka Zaire – wote hao wakiwa wamewekwa gerezani kwa amri za viongozi wao. Walikuwa ni pamoja na Andreas Shipanga, aliyekuwa katibu mwenezi wa SWAPO, Andreas Nuukwawo, aliyekuwa mwanaharakati wa umoja wa vijana aliyewekwa kizuizini na kuchapwa viboko Namibia, na wengine tisa waliokuwa wanachama wa SWAPO ambao waliwekwa kizuizini kwa ‘kuhatarisha usalama wa Tanzania’ (Amnsety International, 1978: 3). Waliwekwa gerezani kwa amri ya viongozi wa vyama vyao ambavyo vilikaribishwa na Tanzania ikiwa makao makuu ya Kamati ya Ukombozi ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika. Wao, pamoja na waliokuwa wanachama wa ANC, PAC na ZAPU walikuwa wakitumikia vifungo vya hadi miaka saba.
Babu aliazimia kutokiruhusu kipindi kirefu cha kuwa kwake gerezani kiivize ari yake. Kama vitabu vingi vya nukuu zake za gerezani vinavyoeleza, alijifunza falsafa ya Marx, akiangalia uwili wa uwezo na udhaifu wa nguvu za ari ya mtu, furaha na majonzi, haki na batili, tafsiri yao ya ulinganifu na mfumo wa utoaji haki uliolenga katika kumwendeleza mtu mmoja na kumkandamiza mtu mwengine’ (Babu, 1996: 332). Pia, aliendesha mafunzo juu ya nadharia ya Marx na misingi ya siasa ya uchumi kwa wafungwa wa kisiasa waliofikia kiasi cha 119 (wengi wao wakiwa hawahusiani na kesi ya Zanzibar) waliokuwepo Ukonga wakati yeye akiwa hapo. Ilikuwa ni kutokana na majadiliano yaliyoibuliwa na mihadhara yake ndipo alipokiandaa kitabu chake mashuhuri cha African Socialism or Socialist Africa. Kilikuwa ni uhakiki wa uzoefu wa Tanzania katika kipindi cha baada ya uhuru, na kutaka kuwepo kwa mfumo wa usoshalisti wa kidemokrasia wenye kuongozwa na umma wenye kutilia maanani hali halisi ya Afrika. Kitabu hiki kilitoka mwaka 1981 na kuchapishwa na Zed Press na kutokea kuwa ni kitabu kimojawapo kilichokuwa na ushawishi mkubwa kwa vijana wapenda maendeleo wa kiafrika katika miaka ya 1980 na 1990.
Kampeni ya Kudai Kuachiliwa kwa Babu na Wafungwa Wote wa Kisiasa.
Mwaka 1975, kipindi ambacho washtakiwa wamekuwa gerezani kwa zaidi ya miaka mitatu, kipindi ambacho vifo na mateso yakitokea na baadhi ya washtakiwa wakiwa wametengwa katika hali ya upweke kwa zaidi ya mwaka mmoja, adhabu za kifo 18 kati ya 42 zilifutwa kutokana na rufaa kwenye Mahakama Kuu ya Zanzibar. Baada ya miaka miwili mengine, tarehe 9 Februari, 1977, Baraza Kuu la Chama cha Afro-Shirazi lilitangaza matokeo ya rufaa ya mwisho ya mahakama kwa Kesi ya Uhaini ya Zanzibar. Adhabu za kifo saba zilithibitishwa (nne wenyewe wakiwa hawapo kwa waliokuwa kizuizini bara) na 17 zilifutwa na kuwa adhabu za kifungo za miaka 30 au 35, sita kati ya hizo wenyewe wakiwa hawapo. Adhabu nyengine za kifo zilikuwa zikisubiri kupitiwa tena na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Aboud Jumbe.
Hata hivyo, kama lilivyoeleza Shirika la Amnesty International, ‘hayakutangaza matokeo yoyote hadi kufikia mwisho wa 1977’ (Amnesty International, 1979). Wanne waliohukumia kifo bara walikuwa Babu, Ali Mahfoudh, Tahir Ali na Hamed Hilal.
Wakati huo huo, kampeni ya kudai kuachiliwa kwa washitakiwa wa kesi ya uhaini ilipamba moto katika medani ya kimataifa. Ilikuwa ikiendeshwa na Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binaadamu (Amnesty International), wanafunzi wa Zanzibar walokuwepo nchi za nje na wakikiunga mkono Chama cha Umma Party na wasomi wengi na wanaharakati waliomjua Babu katika miaka ya 1950 na kubaki kuwa rafiki zake. Muhimu katika hawa walikuwa mwanaharakati mkongwe wa kampeni za kisiasa Fenner Brockway, muasisi wa Vuguvugu la Kupigania Uhuru wa Nchi Zilizotawaliwa na Wakoloni na Katibu Mkuu wake na mshajiishaji mkubwa, Barbara Haq. Barbara alikuwa mwanamke mashuhuri aliyejitolea maisha yake katika kuunga mkono vuguvugu la kupigania uhuru dhidi ya ukoloni. Alianzisha mfuko wa Kesi wa Zanzibar uliofanya kampeni bila ya kuchoka ili Babu na makomred wake waachiliwe na kutoa gazeti la kufanya kampeni Habusu – lililoingizwa Zanzibar kwa magendo.
Katika barua aliyomwandikia Barbara kutoka gerezani tarehe 25 Desemba 1976, Babu aliandika:
Habusu kimekuwa ni chombo muhimu cha mapambano. Litakuwa muhimu sana kama mungeliweza kulitoa kwa uchache kila mwezi. Hivi sasa hiyo ni silaha pekee inayoweza kutuletea ukombozi wetu. Lina uwezo wa kuwa kama ‘jukwaa’ maarufu kwa ajili ya ‘ujenzi wa nyumba’. Tafadhali hakikisheni kuwa nakala nyingi iwezekanavyo zinafika Tanzania, hasa Zanzibar.[1]
Tarehe 30 Machi, 1978, Aboud Jumbe alizifuta tatu katika jumla ya hukumu za kifo, zilizotolewa kwa washtakiwa, na tarehe 26 April, 1978, wakati wa sherehe za kuadhimisha miaka 13 ya Muungano, hatimaye Nyerere aliamuru kuachiwa kwa Babu na wengine kumi na mbili waliokuwa kizuizini bara. Ijapokuwa wote waliokuwa kizuizini bara waliachiliwa, hukumu za kifo kwa wanne wao – Babu, Ali Mahfoudh, Tahir Ali Salim na Hamed Hilal – kamwe hazikufutwa.
Katikati ya shangwe za kufurahia kuachiwa kwao, ndugu na marafiki, wengi wao wakiwa wamekusanyika katika nyumba ya Babu, walielewa fika mateso ambayo watu hawa walipambana nayo. Kiwango cha dhulma, mateso ya kimwili na ya kisaikolojia na maonevu ya kila siku yaliacha kovu kwao. Badru na Tahir Ali walikufa miaka michache tu baadae. Shirika la Kimataifa la Kutetea Haki za Binadamu(Amnesty) lilifanya mpango wa kuwapatia hadhi ya ukimbizi Hamed na Hashil, na hatimaye waliondoka kwenda Denmark. Huko, Hamed aliniambia ‘baada ya uchunguzi wa kitabibu na tiba, ndipo tulipoweza kurudisha imani na ari yetu’. Ali Mahfoudh aliondoka Tanzania kwenda kuishi Msumbiji.
Babu alibaki Dar es Salaam kwa miezi michache. Lakini hukumu ya kifo ikiwa bado imemwandama, marafiki na makomred kutoka kote duniani walimtaka aondoke nchini. Mwaka 1979 aliondoka Tanzania kwenda kufanya kazi ya ualimu Marekani, kwanza katika Chuo Kikuu cha Serikali cha San Francisco na Chuo Kikuu cha California, na baadae katika Chuo cha Amherst, Massachusetts mwaka 1981. Mwaka 1984 alihamia London na kupafanya hapo kuwa ndiyo kituo chake. Alisomesha katika Chuo cha Birkbeck na kuandika makala katika machapisho mengi kuanzia Pacific News Service hadi African Concord, Africa Events, New African na Africa Now. Alishirikishwa katika majarida kama vile Review of African Political Economy (ROAPE), the Journal of African Marxist na Africa World Review na asasi kama vile Africa Research and Information Bureau.
Kwa Babu hakuna gazeti lililokuwa halina umuhimu au lililokuwa na wasomaji wachache, kwake yeye hakuweza kukataa asiliandikie makala. Maandishi yake mengi muhimu miongoni mwa yale yaliyokuwa yakisomwa sana yalianza kuwafikia na kuwahamasisha wanaharakati waliopenda maendeleo Afrika na nje ya Afrika.
Akiwa London, mchangamfu kama kawaida, aliendelea kuishi maisha yaliyojaa matumaini mema, mara nyingi akiwa katika majadiliano yaliyochangamka huku akivutia marafiki wengi, makomred, wanafunzi wafuasi na wengi waliomuunga mkono.
Wakati huu wa unyonyaji wa kiuchumi unaozidi kukua na ukiritimba wa kiitikadi wa mashirika ya nchi za magharibi, Babu aliandika juu ya haja ya kuwepo kwa ukombozi wa pili wa Afrika. Kila siku akitafuta cheche za matumaini mema na kuwa tayari kuzichochea, amekuwa mshauri wa karibu wa vyama vyote vya ukombozi vilivyopinga serikali za kijeshi za ukoloni mambo leo na Shirika la Fedha la Dunia, ukandamizaji wa Benki ya Dunia kama ule uliokuwepo wakati ule Eritrea, Uganda na Ethiopia.
Kadhalika, alikuwa mstari wa mbele katika kuufufua Umajumui wa Afrika utakaolingana na hali halisi za wakati huu. Hii ilipelekea kuanzishwa kwa Vuguvugu la Umajumui wa Afrika lililofanya mkutano wake wa kihistoria (Mkutano Mkuu wa Saba wa Vuguvugu la Umajumui wa Afrika) uliofanyika Kampala, Uganda mwezi April 1994 ukiwa na kaulimbiu ‘Pinga kutawaliwa tena na wakoloni!’ na ‘Usisononeke Jiandae Upya!’
Katika mkutano huo kama alivyoandika Tajudeen Abdulraheem, katibu mkuu wa vuguvugu hilo na mmoja wa makomred wa karibu wa Babu wakati akiwa London, ‘katika wakati nyeti yanapokuwepo majadiliano makali…. alitoa miongozo ya kisomi, kisiasa na yake binafsi ambayo ilihakikisha kuwa misingi sahihi inatawala juu ya ubinafsi’ (Abdulraheem, 1996: 342). Hata hivyo, wakati akidhibiti ushawishi wa mitazamo tofauti ya Umajumui wa Afrika katika mkutano huo, mtazamo wake mwenyewe ulibaki kuwa ni ule wa muungano wa Afrika, siyo ulioundwa baina ya nchi lakini ulioundwa kwa nia ya pamoja iliyoungana na ya mshikamano wa wanamapinduzi wa Afrika.
Wakati wote wa maisha yake, Babu alibaki kuwa mkomunisti ambaye falsafa ya Marx kwake si kama ilikuwa ni itikadi tu bali ni nyenzo ya kufanyia uchambuzi. Ilikuwa ni mtazamo wake wa kiyakinifu uliomwezesha kuainisha bila ya imani za upofu au ukabila msukumo wa maendeleo na mabadiliko katika hali yoyote ile na wakati huo huo asipoteze nia yake ya kutaka kuwepo kwa mustakbal wa kisoshaliti kwa Afrika na kwa dunia nzima.
- Babu ananukuu maelezo ya Lenin ya gazeti lenye msimamo mkali kuwa ni ‘ chombo cha pamoja’ kinachoweza kufananishwa na jukwaa lililolizunguka jengo linalojengwa kwasababu linafuata muundo wa jengo hilo na kuwezesha kuwepo mawasiliano kati ya wajenzi, na kuwawezesha kugawanya kazi na kuangalia matokeo ya pamoja yaliopatikana kutokana na kazi yao waliyoiandaa. ↵
0 Comments