Matukio ya wiki mbili kabla ya Muungano ni ya kuvutia, kwasababu kama tutakavyoona, nyaraka zilizowekwa wazi za Shirika la Ujasusi la Marekani na Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje ya Marekani zinavyotudokozea njia zilizotumiwa na Marekani, nyingi katika hizo zikiwa bado zinatumika hivi sasa. Simu hizi za upepo zinaonyesha vile vile ni namna gani Tanganyika na Zanzibar zilivyokuwa zimewekwa katika dira ya wabeberu ya Afrika ya Mashariki.
Wamarekani na Waingereza walikuwa wakifikiria mipango na mikakati tofauti ya namna mbalimbali. Kwa mfano, ulikuwepo uwezekano wa kuziunganisha serikali zenye kufuata sera za ‘wastani’ za Kenya, Uganda na Tanganyika na kuunda Shirikisho la Afrika ya Mashariki na kuijumuisha Zanzibar ili kuidhibiti. Hili lilikuwa bado likifikiriwa hadi ilipofika katikati ya mwezi April 1964, lakini lilionekana kutowezekana.
Vile vile, ulikuwepo uwezekano wa uvamizi wa kijeshi wa Uingereza, uliojadiliwa katika waraka wa Ofisi ya Ujasusi na Utafiti.
Katika kipindi cha miezi sita Zanzibar inaweza kuwa nchi ya kwanza katika Afrika yenye kufungamana na Ukomunisti kikwelikweli na siyo kwa jina tu. Hatua hiyo ya dharura inaweza kushitukizwa na kikosi cha Uingereza na kumwondoa Babu na nafasi yake kushikwa na watu ambao kwa dhati ni wafuasi wa siasa za wastani watakaokubalika na Chama cha Afro-Shirazi cha Zanzibar. Hata hivyo, haitoyumkinika … kwa Rais Karume kuomba ufanyike uvamizi … na ukimwacha Karume, hakuna mtu aliye mfuasi wa siasa za wastani ambaye angeliweza kupatikana ili kuchukua nafasi ya Babu na kikundi chake cha wafuasi wa siasa za mrengo wa kushoto ambao wanaungwa mkono na wananchi weusi wa Zanzibar, na wakati huo huo kuepukana na fedheha ya upinzani wa mapinduzi. (Imenukuliwa katika Wilson, 1989: 65).
Halafu palikuwepo na uwezekano, kama alivyoripoti William Leonhart, balozi wa Marekani nchini Tanganyika kwenye Wizara ya Mambo ya nje ya Marekani siku chache baadae, kuwa ‘kwa mujibu wa minong’ono ya huko London … Babu hataruhusiwa kurudi Zanzibar’ (imenukuliwa katika Wilson, 1989: 73).
Vile vile lilikuwepo wazo la ‘kumwangamiza’ Babu, wazo ambalo lilizungumzwa na William Attwood, balozi wa Marekani nchini Kenya na Colin Legum, mwanahabari wa gazeti la Observer ambaye Marekani wakishauriana naye mara kwa mara. Attwood aliripoti Washington kuwa Legum alimwambia kuwa ‘kumwangamiza Babu ndiyo suluhisho la pekee’ (imenukuliwa katika Wilson, 1989: 71).
Hata hivyo, tarehe 19 April Leonhart aliripoti kuwa mambo yamekwenda haraka kwa namna ambayo haikueleweka. Ilitolewa amri ya kukodi ndege ili kuwaondoa kutoka Zanzibar polisi waliokuwepo huko kwa msaada wa Serikali ya Tanganyika na kuwapeleka Dar es Salaam. Hili lilifuatiwa na msafara wa Karume kwenda Dar es Salaam, kwa ziara ya siri, kwa kuwa vyombo vya habari vilikuwa havikuarifiwa. Baada ya muda mfupi amri ya kukodi ndege ilifutwa. Ni jambo la kushangaza kuwa alikuwa Colin Legum aliyeweza kufafanua sababu hasa ya haya yaliyokuwa yakiendelea katika makala yake kwenye gazeti la Observer mjini London: Uingiliaji kati wa kwanza wa [Nyerere] ulikuwa pale … katika juhudi za kumwamsha Karume ili aelewe juu ya yaliyokuwa yakijiri, alitishia kuondoa polisi 300 wa kutoka Tanganyika … Karume alitaharaki kwa onyo hilo. Kwa hiari yake, alikubali kufanya mazungumzo na Nyerere (imenukuliwa kutoka Wilson; 1989: 74).

Nyerere Mpenda Maendeleo

Kwa kuwa Nyerere alionekana dhahiri kwamba alikabiliwa na chagizo la Wamarekani na Waingereza ili asaidie katika kuidhibiti Zanzibar, na kuwa na hisia za kuwa na wajibu wa kulipa fadhila kwa nchi za magharibi kwa kumnusuru na uasi uliotokea Colito, ilikuwa ni vigumu sana kuweza kuonekana kama mhusika huru juu ya suala la Zanzibar.
Hili linathibitishwa mara kadha katika nyaraka za Marekani. Kwa mfano, balozi wa Marekani Tanganyika, Leonhart, katika simu ya upepo kwa Wizara ya Mambo ya Nje tarehe 27 April, alieleza, ‘nadhani kuwa ni muhimu kuwa Nyerere apewe msaada mkubwa wa kimyakimya tokea mwanzoni pamoja na tarehe 29 April:
Kukubali kwa Nyerere kutawezekana kulibeba tatizo lote la Zanzibar na kutajenga imani juu ya nia ya usalama wa Tanganyika na uwezo wa nchi za Magharibi …Pendekezo langu la kwanza ni kwamba tumpatie Nyerere kauli thabiti ya kumuunga mkono kabla ya mwisho wa wiki kuhusu mambo aliyoyazungumza leo. Ili iwepo athari kubwa itabidi iwe … kumhakikishia kuwa Dunia Huru itaipatia Jamhuri ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, kwa ajili ya maendeleo ya Zanzibar hadi Dola milioni 2 ili kugharamia miradi tuliyokubaliana [pesa hizi kamwe hazikutolewa]. Michango kutoka kwa wafadhili wengine, hasa Uingereza na Shirikisho la Jamhuri ya Ujarumani ni muhimu kwa ajili ya upatikanaji wa fedha na kuepuka mwonekano wa kuwepo kwa uvamizi wa Marekani. (Imenukuliwa katika Wilson, 1989: 81)
Kuuelezea muungano kati ya Zanzibar na Tanganyika kuwa ni wazo la Nyerere la kujenga Umoja wa Umajumui wa Afrika, kama baadhi ya waandishi walivyofanya ni jambo la kipuuzi. Wakati huo vita baridi, kama vilivyo vita dhidi ya ugaidi hivi sasa, vilisababisha uingiliaji kati wa mara kwa mara wa Marekani ili kujaribu kuwashawishi na kuwachezea viongozi wa nchi za Afrika, na pale ambapo hawakuweza kufanya hivyo, waliandaa ‘mageuzi ya serikali’. Nyerere alinusurika na hilo na siku zote amekuwa mtu mwenye mawazo ya kiliberali. Kama alivyonieleza Gora Ebrahim, mpigania uhuru wa Afrika ya Kusini na kiongozi wa Chama cha Pan Africanist Congress, ambaye ameishi Tanzania kwa miaka mingi, katika mahojiano yetu ya 1988:
Nyerere alibaini kuwa ili aendelee kubaki madarakani akitilia maanani mazingira ya matukio yaliyomzunguka wakati ule—kwa mfano, kupinduliwa kwa Nkrumah- ilimbidi ajiimarishe madarakani na wakati huo huo, akibakia kuwa tegemezi kwa nchi za Magharibi, na asionekane kuwa ni kibaraka wa nchi yoyote ya kigeni.
Katika hali hii, Nyerere vile vile alikuwa ni tofauti na Kenyatta, ambaye kabla ya uhuru alikuwa maarufu zaidi na mpiganaji madhubuti wa haki ambaye baada ya uhuru alisalim amri moja kwa moja. Nyerere hakuwa maarufu sana kama Kenyatta lakini alijijengea taswira ya kuwa mpenda maendeleo.
Nyerere alikuwa ni kiongozi mwenye siasa za wastani wa TANU, chama ambacho kilijadiliana bia ya kupigana juu ya upatikanaji wa uhuru kutoka kwa Waingereza. Baadaye alikuwa rais wa Tanganyika aliyependelea nchi za magharibi na akiwa Rais wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar alikuwa na deni kubwa zaidi la kulipa kwa nchi hizo za Magharibi. Kwa historia kama hii angeliwezaje kuioanisha hali hii na jukumu lake jipya la kuwa kiongozi mzalendo wa Afrika ya Mashariki na rais wa nchi huru, inayojitawala? Uasi wa Colito ulimsaidia Nyerere kuelewa kuwa ni lazima aache kuwa kiongozi mpya wa serikali iliyo chini ya utawala wa ukoloni mambo leo. Ni katika mukhtadha huu ndipo umoja wa Umajumui wa Afrika ulipokuwa muhimu. Hii ilifungua njia ya kuujenga upya wasifu wa Nyerere. Hii inawezekana kuwa ndiyo sababu ambayo ilimfanya Nyerere akubali vile vile kusaidia mapambano ya ukombozi na kutoa kauli kali za kisiasa na baadhi ya wakati hata kuchukua msimamo wa siasa kali lakini bila ya kuathiri uhusiano wake na nchi za Mgharibi.
Hata wakati wa migogoro, kwa mfano tarehe 15 Januari 1965 baada ya Kamati ya Ukombozi ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika kufichua siri kuwa Carlucci na rafiki yake mwanadiplomasia wa Kimarekani Robert Gordon wanahusika na njama za chini kwa chini nchini Tanzania na Nyerere kulazimika kuwafukuza, aliweza kuendelea kuwa na uhusiano wa ‘kirafiki’ na Marekani. Ili kulipiza kisasi kwa kufukuzwa Carlucci na Gordons serikali ya Marekani si kama ilimfukuza balozi mdogo wa Tanzania nchini Marekani tu bali pia ilitishia kufuta misaada kwa miradi mbalimbali. Hata hivyo, kama ilivyoeleza simu moja ya upepo ya ubalozi wa Marekani wiki chache baadae, ni jambo la ‘ kushangaza kuona kuwa ushirikiano wa kila siku kati ya wawakilishi wa Shirika la Ujasusi la Marekani wa hapa nchini na wenzao wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania umekuwa ukiendelea kama kawaida’ (imenukuliwa katika Wilson, 1989: 107).

Karume Aitoa Sadaka Jamhuri ya Watu wa Zanzibar

Habari za kina juu ya nani alijua au nani hakujua kuhusu mipango ya Muungano, au nani alithibitisha au nani hakuthibitisha ni kitendawili kigumu kukitegua hivi leo kwasababu ya kutokuwepo ushahidi madhubuti wa nyaraka na hili ndilo tatizo la baadhi ya masimulizi yanayotaka kufanywa hivi sasa kuhusiana na wakati huo. Hapa, nimetumia mahojiano ambapo watu wanaelezea mawazo yao na hatua zao walizochukua lakini nimeepuka kutumia maelezo yale ambayo wenye kuhojiwa wanajaribu kukumbuka siyo nini watu wengine walisema lakini nini wao hivi sasa wanadhani watu wengine walifikiri.
Tunachokijua ni kuwa muungano ulikubaliwa wakati Babu akiwa hayupo nchini, kuwa ulipangwa na mambo yake kuandaliwa wakati akiwa hayupo, na kuwa hayo yalifanywa kwa makusudi. Tunajua vile vile kuwa alishtushwa na kukasirishwa na hali iliyojitokeza na isiyozuilika ambayo ilimkabili aliporudi kutoka Indonesia (angalia ukurasa wa 72). Alijua kuwa hakuwa na njia nyengine ila kuukubali Muungano. Hata hivyo, katika kutafuta cheche za matumaini, alitafuta njia chanya za kuikabili hali hii ya kukatisha tamaa na kuwaambia baadhi ya wenzake kuwa muungano na Tanganyika utapanua wigo wa mapambano yao ya kujenga usoshalisti (mawasiliano binafsi na Babu, Disemba 1989).
Tarehe 22 April Mkataba wa Muungano ulitiwa saini kati ya Nyerere na Karume. Walikubaliana kujenga mahusiano ya ukoloni mdogo kati ya Zanzibar na Tanganyika. Zanzibar ilipewa kiasi fulani cha uhuru wa eneo lake kuhusiana na kilimo, polisi na mahakama lakini mamlaka kamili kuhusu mambo ya nje, ulinzi, vyama vya wafanyakazi, udhibiti wa fedha za kigeni na kadhalika – yalikuwa chini ya serikali kuu iliyokuwepo Tanganyika.
Lakini lililo muhimu ni kuwa Mkataba huu ulioidhinisha udhibiti wa Serikali ya Muungano kwa Visiwa vya Zanzibar, haukuridhiwa na Baraza la Mapinduzi la Zanzibar. Karume alipouwasilisha kwenye Baraza la Mapinduzi, Khamis alisema kuwa ‘kwasababu ya umuhimu wake, suala hili ni lazima wananchi waachiwe kuamua kwa kupitia kura ya maoni’. Khamis aliniambia kuwa Karume alijibu kwamba, “ikiwa hamuutaki basi nitaurudisha kwake [Nyerere].” Hakuna mwengine aliyesema jambo lolote zaidi’ (mahojiano na Khamis Ameir, 2009).
Ikiwa Karume alielewa vilivyo kuhusu matokeo na athari za Muungano ni jambo lisiloeleweka. Nyaraka za Kimarekani zinaeleza kuwa hakuelewa. Kuhusu uhalali wa utaratibu huo, Shivji anaandika:
Ushahidi wote unaonyesha dhahiri kuwa hiyo inayodaiwa kuwa ni Sheria ya Zanzibar ambayo iliridhia Mkataba wa Muungano ilitengenezwa na kuandikwa na maafisa wa sheria wa Tanganyika nchini Tanganyika …Baraza la Mapinduzi kwa ujumla wake halikuukubali Muungano. Hakuna shaka kuwa Muungano ‘uliburuzwa’ … maafisa wa sheria wa kigeni wa Serikali ya Tanganyika (ambao katika suala hili walitokezea kuwa ni marafiki wa Nyerere) walitumia hila za kisheria kuchapisha katika gazeti la serikali la Jamhuri ya Muungano Sheria ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ya mwaka 1964 ambayo waliitengeneza wenyewe na kuwa ni taarifa iliyotiwa saini na Fifoot [mmoja wa maafisa wa sheria wa kigeni]. (Shivji, 2008: 93)
Wakati huo huo, Leonhart alituma simu Washington akipeleka ombi la Nyerere kuwa ‘kwa kiasi chochote kile iwezekanavyo’ liepukwe tamko lolote lile la wazi la Marekani kuhusu serikali ya muungano wa Tanganyika- Zanzibar … alipendekeza kwa nguvu zote kuwa msimamo wa tamko lolote la wazi uwe … Kuwa mradi huo ni kwa watu wa Tanganyika na Zanzibar wenyewe kuamua’ (ilinukuliwa kutoka Wilson, 1989: 77). Attwood, balozi wa Marekani nchini Kenya, aliongeza kuwa katibu wa Nyerere alimwambia kuwa ‘madaraka makubwa yatakuwa ni ya serikali kuu. Sheria za Tanganyika ndizo zitakazotawala kote … Aliliona hili kuwa ni muhimu sana kwa kuwa Sheria ya Kuweka Watu Kizuizini ingeliweza kutumika kuwakamata wale wenye siasa kali wa Zanizibar (msisitizo wangu) (imenukuliwa katika Wilson, 1989: 78).

Siku za awali za Tanzania-Bara

Washauri wa Nyerere ‘Tahadhari na’ wafuasi wa Siasa za Mrengo wa Kushoto

Wakati nyaraka za kisheria zilipotayarishwa na kutiwa saini na maafisa wa Kiingereza, mgawanyo wa nyadhifa katika serikali mpya tarehe 27 April vile vile uliidhinishwa na maafisa wa Kimarekani. Kama alivyoeleza Leonhart tarehe 29 April:
Jamhuri ya Muungano ya Nyerere imetupa mfumo wa awali wa kisiasa ambao tunaweza kufanya nao kazi. Madaraka muhimu ya mambo ya nje, fedha, jeshi na polisi yote yapo Dar es Salaam na watu madhubuti kabisa wa Nyerere ndio wanaoshikilia kila moja ya nafasi hizo … [Wazanzibari] wanashikilia nyadhifa ndogo ndogo na wanadhibitiwa na Watanganyika katika wizara zinazohusiana kwa karibu na nyadhifa wanazozishikilia. (Imenukuliwa katika Wilson, 1989: 83)
Ushirikishwaji wa wafanyakazi wa kigeni wa Kiingereza na maafisa wa Kimarekani ulikuwa ni onyo la mapema kuwa mtindo wa kuomba kibali mara kwa mara na kutaka ushauri kutoka nchi za Magharibi ungelikuwa ndiyo utaratibu wa kawaida katika miaka ifuatayo mbele.
Katika baraza la kwanza la mawaziri la Tanzania Karume alikuwa makamu wa kwanza wa rais na Rashidi Kawawa makamu wa pili wa rais. Wazanzibari walikuwa ni pamoja na Aboud Jumbe, waziri wa nchi katika ofisi ya Makamu wa kwanza wa Rais; Abdulla Hanga, waziri wa viwanda, migodi na nishati; Babu, waziri wa nchi katika Ofisi ya Rais na Kurugenzi ya Mipango; Hassan Nassor Moyo, waziri wa sheria na Idrisa Abdul Wakil, waziri wa habari na utalii.
Kama alivyoeleza Babu katika mahojiano ya 1988:
Nyerere aliutumia uteuzi huo kudhoofisha kambi ya wapenda maendeleo. Kwa msaada wa Marekani … tulipelekwa katika wizara zisizokuwa na umuhimu wowote – kwa mfano, mimi mwenyewe, nilipewa Wizara ya Mipango ya Uchumi. Lakini sikuwa na madaraka. Walikuwepo mawaziri wa nchi watatu. Sote watatu tulikuwa chini ya Rais. Hakuna lolote ambalo tungeliweza kufanya. Sikuweza kuandaa sera au kuzitekeleza sera hizo. Sikujua hata huo mpango ulihusu nini —nilichokishuhudia ni yale yaliyokuwa yakifanywa na watu wengine. Alikuwepo mkurugenzi wa mipango Mfaransa. Yeye ndiye aliyekuwa na madaraka ya mipango. Athari ya baraza kama hili la mawaziri ilikuwa ni kutudhoofisha. Tulipewa majumba makubwa na magari lakini hatukuwa na shughuli yoyote Zanzibar wala hatukuwa na shughuli yoyote Bara [Babu binafsi alizikataa fursa hizi na aliishi maisha ya kawaida kama namna aliyokuwa akiishi kabla na kuendesha gari yake mwenyewe.]
Udhibiti mkubwa wa kila aliyedhaniwa kuwa ni muumini wa sera za mrengo wa kushoto ulithibitishwa kwa masimulizi ya siku hizo ya Al Noor Kassam. Kassam, mtu wa Nyerere wa karibu alieleza juu ya namna gani Hanga ‘alidhibitiwa’.
Waziri wangu alikuwa Abdulla Hanga kutoka Zanzibar … Kabla ya kubadilishwa wizara, Mwalimu Nyerere aliniita na kunieleza kuwa nilikuwa na jukumu mahasusi la kulitekeleza katika Wizara. ‘Hapo unahitajiwa ili kumdhibiti Hanga’, alisema. Baada ya muda mfupi ilionekana wazi kuwa Mwalimu alikuwa sahihi katika kuwa na hadhari. Waziri ilimbidi awasilishe bajeti yake katika Bunge na baada ya kuandika hotuba yake ya bajeti aliileta kwangu ili nitoe maoni yangu. Baada ya kuisoma, nilijikuta nipo njia panda kwa kuwa ilijaa mawazo ya kimsimamo wa siasa kali. Kwa hivyo nilikwenda kwa Mwalimu na kumweleza juu ya hali ilivyo. ‘Naweza kuibadilisha kwa kiasi fulani lakini nadhani itakuwa shida sana. Kwa kweli inahitaji kuandikwa upya,’ nilimwambia. Hapo Mwalimu alipendekeza suluhisho: ‘Kwanini humwambii Bwana Hanga kuwa kwasababu hii ni mara ya kwanza kuwasilisha bajeti hii, Rais mwenyewe angelipenda kuiona hotuba yako ya bajeti …‘ Kwa hivyo mimi na Hanga tulikwenda Ikulu na kukaa na Mwalimu. Baada ya kuisoma hotuba hiyo, alimwambia Hanga. ‘ Hii ni hotuba nzuri sana lakini inahitaji marekebisho kidogo …’ (Kassam, 2007: 45)
Baada ya marekebisho hayo kufanywa, alieleza Al Noor Kassam, ‘ilikuwa ni hotuba nyengine kabisa.’
Juu ya hali hii, Babu aliendelea kutaka iwepo mikakati ambayo aliamini kuwa ingelisaidia katika kuleta maendeleo ya Tanzania. Ukiacha mambo machache tu (angalia hapo chini) yote hayo yalipingwa. Alipewa uhamisho wa mfululizo kutoka wizara moja hadi wizara nyengine huku sera za maendeleo ziliendelea kubaki, kama ilivyokuwa hapo awali, mikononi mwa wageni.
Hata hivyo, kuwepo kwa Babu na Wazanzibari wengine wapenda maendeleo katika baraza la mawaziri kulimsaidia Nyerere kwa kuwa waliipa Tanzania, na kwa hivyo Rais wake, sura ya kuwa ni nchi iliyokuwa na mwelekeo wa kimapinduzi.
Katika medani ya Umajumui wa Afrika na medani pana zaidi ya mapambano dhidi ya ubeberu, Babu aliweza kuendelea kuimarisha baadhi ya mahusiano yake ya zamani katika miezi iliyofuata baada ya muungano. Moja ya hayo yalikuwa ni kuhusu mapambano ya Wamarekani wenye asili ya Kiafrika na hasa Malcolm X. Amekuwa akiwasiliana na Malcolm X mara baada ya mapinduzi na alikutana naye tena Kairo mwezi julai 1964 pale wote walipohudhuria Mkutano wa Pili wa Wakuu wa Nchi za Afrika na Mkutano wa Wakuu wa Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote. Kama Babu alivyosema katika hotuba aliyoitoa katika mkutano juu ya Malcolm X : Mila ya kuwa na msimamo wa siasa kali na urithi wa mapambano jijini New York mwaka 1990 ‘siasa za Malcolm zimekuwa zikiendelea, alikuwa na dira ya kuliona tishio la muungano wa nchi za Dunia ya Tatu kwa ubeberu’. Malcolm X aliitembelea Tanzania mwezi Oktoba mwaka huo huo, wakati ambao yeye na Babu wamekuwa marafiki wakubwa. Baadaye mwaka huo huo walihutubia kwa pamoja mkutano wa hadhara uliofanyika Harlem. Hapana shaka yoyote kuwa Babu alikuwa na ushawishi mkubwa kwa Malcolm X na kumfanya awe na mtazamo thabiti wa kimataifa dhidi ya ubeberu.
Malcolm X na Babu katika Hadhara ya Mkutano wa Umoja wa Wamarekani wenye Asili ya Afrika, New York, Disemba 13 1964.
Malcolm X na Babu katika Hadhara ya Mkutano wa Umoja wa Wamarekani wenye Asili ya Afrika, New York, Disemba 13 1964.

Reli ya kuunganisha Tanzania na Zambia, TAZARA

Baada ya kufukuzwa Carlucci na juu ya kuendelea kwa uhusiano wake mkubwa na nchi za Magharibi, Nyerere amekuwa na wasiwasi kwamba msaada kutoka nchi za Magharibi unaweza kuwa ni wa matatizo zaidi. Tofauti na alivyokuwa hapo awali, alikuwa tayari kutafuta msaada kutoka mahali pengine, na alivutiwa na msimamo wa China juu ya Zanzibar. Kwa hivyo aliamua kuitembelea China, akitegemea kuendeleza uhusiano wa karibu uliokuwepo kati ya China na Zanzibar, uhusiano uliojengwa na Babu na kuutanua kwa Tanzania nzima. Akiwa na wazo hilo Nyerere alimtaka Babu kwenda China wiki mbili kabla ya ziara yake yeye mwenyewe.
Katika mahojiano ya mwaka 1988, Babu aliikumbuka ziara hiyo:
Katika safari hii ya awali Waziri Mkuu Zhou Enlai aliniuliza nilidhani Rais Nyerere angelipenda kuzungumza nini zaidi. Nilijibu kuwa inawezekana labda Nyerere angelitaka kuzungumza juu ya ujenzi wa reli kati ya Tanzania na Zambia. Lakini Nyerere alipowasili suala la reli hakulitaja kabisa. Mwisho, Zhou Enlai alimwuliza. ‘Bwana Rais, unaweza kutwambia – tunasikia kuna matatizo kati yako na Benki ya Dunia kuhusiana na ujenzi wa reli, unaweza kutueleza kwa ufupi?’ (Mahojiano na Babu, 1988)
Huu ulikuwa ndio mwanzo wa mradi mkubwa sana uliofanikiwa wa mfumo wa usafirishaji katika Afrika, ujenzi wa reli ya kihistoria kati ya Tanzania na Zambia TAZARA.
Tarehe 10 Februari 1965, Babu wakati huo akiwa waziri wa biashara na Lin Hai-yun, kaimu waziri wa biashara za nje wa China walitia saini mkataba wa biashara na itifaki kuhusu ubadilishanaji wa bidhaa mali kwa mali kati ya China na Tanzania. Hapa tunawaona wakibadilishana nyaraka walizozisaini wakati huo, 84
Tarehe 10 Februari 1965, Babu wakati huo akiwa waziri wa biashara na Lin Hai-yun, kaimu waziri wa biashara za nje wa China walitia saini mkataba wa biashara na itifaki kuhusu ubadilishanaji wa bidhaa mali kwa mali kati ya China na Tanzania. Hapa tunawaona wakibadilishana nyaraka walizozisaini wakati huo
Reli hiyo ya kuziunganisha nchi mbili hizo ilikuwa na madhumuni ya kuziimarisha Tanzania na Zambia, nchi ambazo zote zilikuwa za Mstari wa Mbele (nchi ambazo wakati huo zikiipinga serikali ya kibaguzi ya Afrika ya Kusini na kuunga mkono vuguvugu la ukombozi). Tanzania ingeliweza kuitumia reli hiyo kuimarisha uchumi wake, kupanua miundombinu yake na kuwezesha kupatikana maendeleo ya vijijini. Wakati huo huo, shaba ya Zambia, bidhaa yake kubwa ya kuuza nchi za nje, isingelipitia tena katika nchi zilizokuwa zikitawaliwa na Wareno za Angola na Msumbiji au Afrika ya Kusini na Rhodesia, kwasababu nchi hiyo ingelipata njia ya kuelekea baharini kwa kupitia bandari ya Dar es Salaam. Matokeo yake ni kuwa Zambia ingeliweza kuchukua msimamo ulio huru zaidi kuhusiana na suala la vuguvugu la kupigania ukombozi kusini mwa Afrika. Mradi huo ulikataliwa na Benki ya Dunia na Serikali ya Marekani.
Mradi huu ulikamilika mwaka 1975, miaka minne kabla ya muda uliopangwa. Ulikuwa ni mradi wa aina yake kwa vile ulikuwa ni mradi uliofadhiliwa na nchi ya kigeni ambao kwa kweli uliwanufaisha wananchi wa Tanzania na Zambia.
Chapter4_3
Babu na Makamo wa Rais Kawawa wakiwa na mashujaa wa matembezi marefu, Januari 1965. (Mpiga picha hajulikani)
Mkopo huu wa kutoka China ulikuwa hauna riba. Ulikuwa na thamani ya Dola za Kimarekani milioni 400, asilimia kumi zikiwa ni gharama za ndani ya nchi ambazo zingelilipwa na Tanzania. Lakini kwa kuwa Tanzania haikuwa na uwezo wa kulipa gharama hizo, Wachina walipendekeza utaratibu wa kifedha ambapo wangelipeleka bidhaa Tanzania na Serikali ya Tanzania ingeliziuza bidhaa hizo ili kupata pesa zilizohitajika. Zaidi ya hilo, Wachina waliweka bei iliyotulia hata pale bei za kimataifa ziliposhuka, na wafanyakazi wa Kichina wakati huo hawakudai vitu vya anasa kama vile nyumba zilizokuwa na viyoyozi.
Hata hivyo, kwasababu ya washauri wa kigeni wa Nyerere, uwezo kamili wa mradi huu haukuweza kutumika kikamilifu, kama alivyosema Babu:
Wachina walituamini; Nyerere hakuwachukulia Watanzania kwa udhati wa nyoyo zao! Wakati huo alidhani kuwa Tanzania ingeliendelea kuwa ni nchi iliyotegemea kilimo milele. Kama ungelimzungumzia kuhusu viwanda, alidhani kuwa ulikuwa ukimzungumzia juu ya safari ya kwenda kwenye mwezi. Wachina waliwafunza mafundi mitambo 3000. Walipoondoka walitwambia kwa nini hamuwatumii hawa pamoja na mitambo yetu ili kujenga mradi mwengine? Nyerere alisema hapana, kwasababu Wachina wanamaliza mradi wao huu na hawana haja ya kuanzisha mradi mwengine. Nchi za Magharibi zitasema nini? Nilisema kinatushughulisha nini watakachosema nchi za magharibi? La muhimu Watanzania watasema nini? Wangelipenda kupata maji? Nyerere hakujali. (Mahojiano na Babu, 1988)

Ndani ya Ukumbi Mkuu wa Umma, Beijing, 1965. Mstari wa mbele kutoka kushoto: Mashal Chen Yi, Babu, Rais Liu Shaoqui, Makamo wa Rais wa Tanzania Kawawa, Mwenyekiti Mao Zedong, Silo Swai (Tanzania), Waziri Mkuu Zhou Enlai, George Kahama (Tanzania). (Mpiga picha hajulikani)
Ndani ya Ukumbi Mkuu wa Umma, Beijing, 1965. Mstari wa mbele kutoka kushoto: Mashal Chen Yi, Babu, Rais Liu Shaoqui, Makamo wa Rais wa Tanzania Kawawa, Mwenyekiti Mao Zedong, Silo Swai (Tanzania), Waziri Mkuu Zhou Enlai, George Kahama (Tanzania). (Mpiga picha hajulikani)
Upatikanaji wa maji ulikuwa ni wa shida sana katika sehemu nyingi nchini. Hata mpaka sasa, upatikanaji wa maji unakidhi kwa asilimia 54 tu, na katika sehemu za mbali kabisa wanawake na watoto hutumia saa kadha kila siku kwenda kuchota maji (Wateraid, 2011).

Sera za Kiuchumi: Tofauti kati ya Babu na Nyerere

Nchi za Magharibi zimekuwa zikiitawala Tanganyika kiuchumi mfululizo tokea wakati wa ukoloni. Nchi ilipopata uhuru mwaka 1961 serikali ilimwomba mshauri wa Kimarekani Arthur D. Little kuandaa mkakati wa ujenzi wa viwanda kwa ajili ya nchi hii na katika muda huo huo Benki ya Dunia ilitoa mkakati wa jumla kwa ajili ya maendeleo ya Tanganyika.
Ripoti hizi zilihakikisha kuwa nchi hii inaendelea kufuata njia ile ile. Zilisisitiza kuwa nchi iendelee kuzalisha zaidi kwa ajili ya kusafirisha nchi za nje na wakati huo huo iwaalike wawekezaji kutoka nchi za nje na misaada – sera ambazo kwa maneno mengine zilielekezwa katika kuongeza faida kwa makampuni ya kimataifa na si kwa kuwanufaisha wananchi wa Tanganyika. Sera hizi zilifuatwa katika mpango wa kwanza wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa Tanzania wa 1964, na kama ilivyotabiriwa, zilizidisha matatizo ya kiuchumi ya nchi.
Babu akijaribu kuelezea mtazamo wake wa kiuchumi kea Nyerere
Babu akijaribu kuelezea mtazamo wake wa kiuchumi kea Nyerere. Chanzo: Mohamed Amin/Camerapix
Mwaka 1967, Nyerere alipohisi kuwepo kwa hisia za kutoridhika kutoka kwa wananchi, alijaribu kuja na mtazamo mwengine utakaopendwa zaidi. Akiuacha Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano alitangaza Azimio la Arusha. Azimio hilo lilikuwa ni ishara ya kuachana na utawala wa nchi za Magharibi. Babu aliliunga mkono Azimio hilo lakini mtazamo wake wa kuachana huko ulikuwa ni tofauti na ule wa Nyerere. Kusema kweli, Azimio la Arusha lilibainisha tofauti nyingi muhimu za kisiasa kati ya Babu na Nyerere.

‘Ujamaa wa Kiafrika’ wa Nyerere

Kwa Nyerere kuachana na utawala wa nchi za kigeni kulimaanisha kurudi katika kile alichokiona kuwa ni jamii isiyokuwa na matabaka iliyokuwepo Afrika kabla ya ukoloni, ambayo aliiona kuwa ikiendeshwa kwa misingi ya upendo kati ya binadamu, haki ya kufanyakazi na kugawana kwa usawa kile kinachozalishwa na kuepukana na umiliki binafsi. Hii ilikuwa ni misingi adhimu kwa kuwa inadhaniwa kuwa iliiunganisaha jamii ya Kiafrika katika kipindi cha kabla ya ukoloni na kuvurugwa tu kutokana na uvamizi wa nchi za kigeni ambao ulileta uchumi uliojengwa chini ya misingi ya matumizi ya pesa na dhana za umiliki binafsi wa rasilimali. Kufuatia misingi hii, Nyerere alijenga hoja ya kurudi kwenye njozi za maisha haya ya zamani. Katika sehemu za vijijini za Tanzania – na sehemu kubwa ya Tanzania ilikuwa bado wakati huo na hadi sasa ni ya maisha ya vijijini hoja hiyo ilikuwa itekelewe kwa kupitia sera ya maisha ya vijijini au kuandaliwa upya mipango ya maisha ya jamii za vijijini kwa kuanzisha vijiji kwa kufuata mpango maalumu ambao wakulima wataendelea kulima mazao ya kuuza na kupata fedha kama ilivyokuwa kabla.
Hii pia ilikuwa na maana ya kufungua njia kwa serikali na chama kujipenyeza katika uchumi na kushamirisha ukiritimba wa serikali kuu wa kudhibiti uchumi. Sera hizi ndizo zilizoelezwa kuwa ndiyo ‘ujamaa wa Kiafrika’. Kauli mbiu ilikuwa kujitegemea, lakini kwa kweli zilihusu zaidi udhibiti wa uchumi na ugumu wa maisha. Kusema kweli, mtindo wa vijiji vya ujamaa hatimaye haukuwa na tofauti sana na ule wa wakoloni wa Kiingereza ulioanzishwa mwaka 1922 na sera ya Benki ya Dunia ya mwaka 1959. Tofauti kubwa kati yao ilikuwa ni kwamba, kwa ajili ya mtazamo wa kimaadili wa Nyerere kuhusiana na suala la kujitegemea mpango huu haukugharimiwa kwa fedha za wageni bali kwa dhima ya nguvu za wananchi wenyewe.
Wakati Benki ya Dunia iliwekeza wastani wa Dola za Kimarekani 300,000 kwa kila kijiji kuwa kama ni rasilimali ya kuanzia kwa ajili ya uendelezaji wa miundombinu ya kiuchumi na kijamii, pamoja na vifaa muhimu vya mitambo, chini ya uongozi wa Nyerere kauli mbiu ya ‘Pesa si msingi wa maendeleo’ ilikuwa na maana kuwa wanavijiji walitakiwa wazalishe rasilimali wao wenyewe pale walipo na wabebe jukumu la hasara zozote zitakazoweza kutokea. Maeneo yote ya vijijini yaliwekwa chini ya mpango huu na ilipofika mwaka 1967, asilimia 90 ya wakaazi wa vijijini walihamishwa. Matokeo yake hayakuwa na tija hata kidogo ukichukulia maisha ya wanavijiji wa kawaida wanaohusika. Wakati Tanzania kipindi fulani ilikuwa ikijitosheleza kwa chakula au hata kuwa na ziada wakati wa misimu mizuri, sera zilisababisha mara moja nchi kulazimika kuagiza chakula muhimu kutoka nje.
Wakati akiilazimisha sera ya vijiji vya ujamaa, Nyerere aliahidi kutowa huduma za jamii pia. Tatizo hapa, kama Babu alivyotoa hoja, ni kwamba hapajakuwa na pesa za kulipia huduma hizi, kwasababu nchini Tanzania (na katika makoloni mengi ya zamani) uchumi kwa kiwango karibu chote ulitegemea uzalishaji wa kilimo cha wakulima wadogowadogo tu. Wakati katika nchi za Ulaya uzalishaji ulikuwa mikononi mwa mabepari na serikali za demokrasia ya kisoshalisti ziliwatoza kodi mabepari ili kulipia gharama za huduma za jamii, nchini Tanzania hapakuwepo msingi madhubuti wa kutoza kodi ambao ungelilipia huduma za jamii kwa kawaida na kila wakati. Kujaribu kujenga nchi ya mfumo wa ustawi wa jamii wa wananchi kwa misingi ya uchumi wa aina hii kungelipelekea katika kusababisha balaa na kuiingiza nchi katika umasikini na kuifanya kuwa tegemezi kwa misaada ya kutoka nje.
Mtazamo wa Babu kuhusu ujamaa ulikuwa bila shaka ni tofauti kabisa. Aliamini kuwa fikra ya kwamba jamii za zamani za Kiafrika zilikuwa ni jamii zilizojaa furaha na uvamizi wa nchi za kigeni ulikuwa na ushawishi mwovu ambao kila mtu inambidi apambane nao ni mawazo ya udhanifu juu ya ulimwengu, ambayo hayalingani na ukweli wa mambo yalivyo:
Kuwa siasa na itikadi za zamani ndiyo taswira ya pamoja ya mifumo yao ya uchumi … Hazihusiani na mifumo ya uchumi ya hivi sasa au mifumo ya uchumi ya siku za mbele … wakati waumini wa mapokeo wanazungumzia usawa katika hali ya umasikini, wajamaa wanapendelea kuzungumzia usawa katika hali ya neema. (Babu, 1981: 58)
Kusema kweli, umasikini umekuja kuwa ndiyo urithi mkubwa aliouacha Nyerere. Wakati Tanzania ikiwa imepanda kidogo katika orodha ya Maendeleo ya Binadamu ya Mpango wa Maendeleo wa Umoja wa Mataifa tokea mwaka 2000, hata hivyo bado imebakia ni ya 159 kati ya nchi 177 zilizoshiriki katika mwaka 2007/08 (Shirika la Kazi Duniani, 2011).

Tafsiri ya Babu juu ya Kujitegemea

Kwa mujibu wa maoni ya Babu, kuachana na utawala wa kigeni (jambo ambalo Azimio la Arusha ndilo lililodai kuleta) kungelilazimisha kuwepo kwa mabadiliko kutoka katika mfumo wa uchumi wa kikoloni (uliotegemea moja kwa moja mazao ya biashara) na kujenga uchumi wa kitaifa kwa lengo la uzalishaji wenye kukidhi mahitaji muhimu ya wananchi: chakula, mavazi na makazi. Kujitegemea kunakuja, kwa mujibu wa maoni ya Babu, pale nchi inapozalisha mahitaji haya muhimu kwa juhudi zake yenyewe na kutokuwa tena muathiriwa wa dhuluma zilizojikita ndani ya soko la dunia.
Katika kipindi cha baina ya kutangazwa kwa Azimio la Arusha na utekelezwaji wake, Babu aliandika mfululizo wa makala yaliyokuwa na kichwa cha habari ‘Maana ya Kujitegemea’ katika gazeti la The Nationalist la Dar es Salaam yaliyotoa ufafanuzi juu ya maoni hayo. Katika makala hayo, Babu alizungumzia juu ya udhaifu na uwezo wa Azimio hilo. Alieleza kuwa bila ya kuwepo kwa Mpango wa Utekelezaji madhumuni ya Azimio hilo hayatafikiwa (Babu, 1967).
Mpango huo, Babu aliandika, ni lazima upunguze maeneo yasiyo ya uzalishaji katika mfumo wa serikali na kushughulikia umoja wa kitaifa na kuendeleza maeneo saba muhimu – kilimo; ufugaji na uvuvi; uzalishaji wa viwandani; rasilimali ya madini; mawasiliano; afya ya jamii; elimu; na ujenzi wa nyumba vijijini.
Uwekezaji katika kilimo uwe ni pamoja na uzalishaji wa chakula kwa njia za kisasa kwa kupitia, kwa mfano, mashamba makubwa ya serikali kandokando ya mito, kudhibiti mafuriko na umwagiliaji. Kama alivyoandika hapo baadae, kama haya yangelifanyika ‘Tanzania ingelijiimarisha katika nafasi yake ya kuwa nchi inayozalisha ziada ya chakula kama ilivyokuwa hapo zamani. Majanga ya asili, mafuriko na ukame vingelikuwa na athari ndogo sana za uharibifu’ (Babu, [1981] 2002: 22).
Alisisitiza kuwa, uwekezaji katika viwanda ungelikuwa ni pamoja na uzalishaji wa rasilmali za makaa ya mawe na chuma cha pua na uendelezaji wa maeneo ya viwanda ambayo yangelitoa ustadi wa kazi na ajira. Hapo tena, Tanzania ingeliweza kutengeneza matrekta, magari ya kubebea mizigo, mashine za kusukuma maji, mashine za ujenzi, vifaa vya mashine za viwandani na kukidhi mahitaji yake mengine mengi ya maendeleo yaliyo muhimu.
Ni jambo la kusikitisha kwa Tanzania, kuwa sera ambazo Babu alizipendekeza na kuzitilia mkazo mara kwa mara katika vikao vya Kamati Kuu ya TANU zilipuuzwa. Mwezi Februari 1972, Nyerere alifanya mabadiliko katika Baraza la Mawaziri na kuwaacha mawaziri wengi waliokuwa na uzoefu mkubwa akiwemo Babu. Nafasi zao zilichukuliwa na watu wasiokuwa na uzoefu waliokuwa watiifu bubu kwa Nyerere ambao aliwaita kuwa ni waumini.
Baada ya mabadiliko haya, sera ya vijiji vya ujamaa kwa haraka ilikuwa ya ukali na ukandamizi zaidi kwa wananchi, na kile kilichoanzishwa kuwa ni mpango wa hiari kwa haraka uligeuka kuwa mpango wa lazima. Mwezi Novemba 1973, Nyerere alitangaza kuwa “Kuishi vijijini ni amri” (imenukuliwa katika Havnevik, 1993: 205). Wale waliokataa kuhama walivunjiwa nyumba zao na kuhamishwa kwa nguvu wakisafirishwa kwa magari ya jeshi au magereza. Wakaazi wa vijijini walihamishwa kwa kasi kubwa sana bila ya kujali athari zake upande wa kilimo, mazingira au hata katika maandalizi ya kimipango. Kusema kweli, uzalishaji wa kilimo uliathirika vibaya, wakulima katika maeneo mengi waligeuzwa kuwa wakulima wa kilimo cha kujikimu na upungufu wa chakula ukaikumba nchi nzima.
La kushangaza ni kwamba katika kipindi chote cha miaka ya 1970 watu waliolazimishwa kuhama kutoka katika ardhi ambayo waliishi kwa vizazi na vizazi, na wale waliojaribu kutafuta maisha chini ya mpango mpya, waliondoka vijijini na kumiminika mijini wakitafuta ajira lakini mara nyingi bila ya kupata chochote zaidi ya kibarua cha hapa na pale. Aina hii ya kuhamia mijini iliongezeka kwa haraka sana Tanzania kuliko mahali pengine popote pale duniani (O’Connor, 1988).

Kutaifishwa kwa Biashara ya Jumla

Tofauti nyengine kubwa ya sera za kiuchumi iliyokuwepo kati ya Nyerere na Babu ilihusiana na biashara ya Jumla. Mwaka 1971, Nyerere aliamua kutaifisha biashara ya jumla (ambayo kwa kiasi kikubwa ilikuwa mikononi mwa familia za Kiasia). Hakuna sababu iliyotolewa kuhusiana na utekelezaji huu ila ilikuja katika dhana isiyofahamika vizuri ya ‘ujamaa’. Babu aliipinga dhana hii kwa kutoa hoja kwa urefu kuwa utaifishaji kama huo utaongeza gharama za usambazaji na kuvuruga mfumo wa biashara; kuwa uchumi wa Tanzania kwa wakati huo ulihitaji kuongeza nguvu kazi yake[1] kwa kuambatanisha pamoja rasilimali zote, binafsi na za serikali; na kuwa ‘serikali haikuhitaji kuwa muuzaji wa mkate na siagi’, lakini ilibidi pamoja ‘ibuni maeneo mengine ya maendeleo, ama katika nyanja za kilimo cha mashamba makubwa au viwanda. Katika sehemu hizi ndiko raslimali za serikali zinakotakiwa ziende badala ya kuzijaribu katika biashara ya usambazaji’ (imenukuliwa katika Wilson, 1989: 135).
Siku ya pili yake serikali iliamua kutaifisha biashara. Babu alikiukwa na kikosi kazi mahasusi kilichoteuliwa na Nyerere na kuongozwa na katibu mkuu wake.

  1. Babu aliyachukuliwa maendeleo ya nguvu kazi ya uzalishaji kuwa ni muhimu sana, na katika nchi kama Tanzania ambako nguvu kazi hii ni ya kiwango cha chini sana, alidai kuwa ni lazima iendelezwe kama ni kipaumbele kuliko mahusiano ya uzalishaji.